http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927278/medRes/2219194/-/1jdcf9/-/reli.jpg

 

Usafiri wa treni Dar-Moshi huu ndio wakati wake

Reli ya Kaskazini ikifanyiwa matengenezo 

Na Mwandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  10:57

Kwa Muhtasari

Serikali itimize ahadi yake ya kufufua reli ya Kaskazini kutoka Tanga hadi Arusha

 

 

Kila inapofika katikati ya Desemba adha ya usafiri katika maeneo mengi nchini huanza kuwatesa wananchi ambao kipindi hicho wengi huchukua likizo kwa ajili ya sikukuu za mwisho wa mwaka.

Kama ilivyokuwa miaka ya nyuma, safari hii adha kubwa ya usafiri iliripotiwa kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Kaskazini inayojumuisha Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga. Watu waliotaka kusafiri kutoka Dar es Salaam kwenda katika mikoa hiyo, walipata wakati mgumu.

Shida ya usafiri ilitokana na wingi wa abiria ikilinganishwa na idadi ya mabasi hivyo kusababisha wasafiri kutozwa nauli kubwa na wengine kukwama katika Kituo cha Mabasi Ubungo (UBT).

Tatizo la usafiri kati ya maeneo hayo kila msimu wa mwisho wa mwaka unapofika limekuwa la kawaida licha ya mara kadhaa, mamlaka husika kuchukua hatua za kukabiliana nalo. Kimsingi ufumbuzi wa kudumu haujawahi kupatikana.

Kama ilivyokuwa mwaka jana na mingine nyuma, mwaka huu pia Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) iliyapa vibali vya muda mabasi madogo kusafirisha abiria kati ya Dar es Salaam na mikoa hiyo. Kwa mwaka huu mabasi zaidi ya 80 yalipata vibali hivyo lakini tatizo halikumalizika.

Tatizo hilo halijaishia kwenye sikukuu pekee, wiki iliyopita liliibuka tena wakati wanafunzi wakirejea shule baada ya kumalizika kwa likizo.

Kutokana na athari hiyo, wasafiri waliokuwa katika Stendi ya Mabasi ya Moshi ambao kwa zaidi ya wiki moja sasa wamekuwa wakitaabika kupata usafiri kiasi cha baadhi kuamua kulala kituoni hapo, wameiomba Serikali kufufua usafiri wa reli ili kusaidia kupunguza msongamano wa abiria katika mikoa ya Kaskazini hasa katika kipindi cha sikukuu kama hizo.

Wamesema kama Serikali itafufua reli hiyo ambayo imesimama kutoa huduma kwa zaidi ya muongo mmoja na nusu sasa, watasafiri kwa treni bila adha kwa kuwa inabeba abiria wengi kwa wakati mmoja.

Desemba, 2017, Serikali kupitia kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa wakati huo, Profesa Makame Mbarawa iliahidi kufufua reli ya Kaskazini ya kutoka Tanga hadi Arusha baada ya kufa kwa miaka 15 ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo yao.

Licha ya ahadi hiyo, bado hatujaona ikianza kufanya kazi. Hivyo, wito wetu kwa Serikali ni kutekeleza ahadi hiyo ambayo tunaamini kwamba itapunguza gharama za usafiri wa abiria na mizigo hivyo kuwarahisishia maisha wananchi hasa wa kipato cha chini.

Tunasisitiza kwamba usafiri wa treni ukiboreshwa kuanzia Dar es Salaam hadi Moshi kwa kiasi kikubwa utapunguza karibu nusu ya tatizo hili.

Mathalani, ikiwa behewa moja la treni lina uwezo wa kubeba abiria 80 na kwa safari moja treni ikiwa na mabehewa 20, maana yake ni kwamba abiria 1,600 watasafiri kwa wakati mmoja ambao ni sawa na mabasi 32 yenye uwezo wa kubeba abiria 50.

Kwa maana nyingine ni kuwa, safari moja ya treni kama hiyo itasaidia kuondoa usumbufu kwa kiasi kikubwa kwa wasafiri ambao wangekwama ama Ubungo, Dar es Salaam au Arusha na Moshi.

Wakati Serikali ikiendelea na mikakati ya kuboresha huduma ya ni wakati pia wa kuliangalia na kuifanyia kazi hoja hii.