http://www.swahilihub.com/image/view/-/4798272/medRes/2135565/-/j8pu3hz/-/habubini.jpg

 

Usahihi wa maneno darubini na hadubini, ujumbe na jumbe

Hadubini (mikroskopu)  

Na Erasto Duwe

Imepakiwa - Tuesday, October 9  2018 at  12:32

Kwa Muhtasari

Katika lugha kuna dhana zinazowakanganya watumiaji

 

Katika matumizi ya lugha wakati fulani kuna dhana zinazowakanganya watumiaji wa lugha.

Bila kujua, watumiaji hao huona ni sahihi kutumia maneno fulani hata kama yanazua utata au kukanganya. Hali hii inapojitokeza ni wajibu wetu kupitia safu hii kuwaangazia watumiaji wa Kiswahili ili kutanzua utata na ukanganyifu unaojitokeza.

Katika matumizi ya kila siku ya lugha ya Kiswahili, tumebaini kuwa maneno kama hadubini na darubini; fasili na fasiri, faliji na fariji, mkurupuko na mlipuko na ujumbe na jumbe yanatumiwa kwa kubadilishana nafasi.  

Mathalan, badala ya kutumia neno darubini, mtumiaji wa lugha hutumia hadubini. Kadhalika, katika mazingira ambayo neno kama ‘ujumbe’ hupaswa kutumika, mtumiaji wa lugha hutumia neno ‘jumbe’ akidhani kwamba ndio wingi wa neno ‘ujumbe’.

Lugha ina taratibu na kanuni zake. Taratibu hizi hutawala vipashio mbalimbali vya lugha yakiwamo maneno.

Kwa hiyo, ni wajibu wetu watumiaji wa lugha kuzingatia taratibu hizo hususan tunapotumia lugha katika miktadha rasmi ya kimawasiliano.

‘Hadubini’ na ‘darubini’ yote ni maneno ya Kiswahili fasaha. Ingawa kwa kiasi fulani maana zake zinaelekea kufanana, zina tofauti iliyo dhahiri. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2013) hadubini (mikroskopu) ni chombo cha kukuza vitu vidogo visivyoonekana kwa macho viwe vikubwa na kuweza kutambuliwa umbo na idadi yake.

Darubini ni chombo kinachofanya vitu vilivyo mbali vionekane karibu na vidogo vionekane vikubwa. Maana za istilahi hizo kwa mujibu wa kamusi tajwa zinaonyesha dhahiri utofauti unaojitokeza.

Maneno ‘fasiri’ na ‘fasili’, kadhalika ni ya Kiswahili fasaha. Neno ‘fasiri’ linamaanisha kueleza maana ya maneno kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine (kutafsiri).

Fasiri inahusika na uhawilishaji wa maana kutoka matini ya lugha chanzi kwenda lugha lengwa lakini ‘fasili’ ni kueleza maana ya neno kwa lugha ya mjazo; kufasili ni kutoa maana ya neno katika lugha husika. Kwa hivyo, kuna tofauti kubwa baina ya maneno hayo. Wakati neno ‘fasiri’ linahusika na tafsiri, fasili linahusika na kufafanua/kueleza maana ya neno.

Pia, maneno ‘faliji’ na ‘fariji’ hutumiwa kwa kubanangwa. Ubanangaji huu yamkini hutokana na dosari za kimatamshi za watumiaji wa lugha. Sababu mojawapo yaweza kuwa ni athari za lugha mama.

Itambulike kuwa maneno hayo yote yamo katika orodha ya msamiati wa Kiswahili na kila moja lina maana yake.

‘Faliji’ lina maana ya ganzi au kiharusi (ugonjwa) lakini neno ‘fariji’ lina maana ya kumliwaza mtu wakati wa tabu au huzuni.

Kadhalika, maneno ‘mkurupuko’ na ‘mlipuko’ yamekuwa yakitumiwa kwa namna tofauti hususan kwa watumiaji wa Kiswahili nchini Kenya. Kitenzi ‘kurupuka’ kina maana ya ondoka ghafla baada ya kushtuliwa ilhali ‘lipuka’ kinamaanisha kitu kutoka, kufumuka, kupasuka kwa nguvu au kwa haraka kwa sababu ya moto. Wakati nchini Kenya wakitumia ‘mkurupuko wa kipindupindu’, nchini Tanzania hutumika ‘mlipuko wa kipindupindu’. Kwa kurejelea vitenzi ‘kurupuka’ na ‘lipuka’, neno faafu kwa muktadha wa matumizi hayo ni ‘mlipuko’. Pia, neno ujumbe linatumika lilivyo katika umoja na wingi.