Ushauri huu wa wataalamu wa afya ni muhimu

Imepakiwa - Monday, April 8  2019 at  08:35

 

Jana Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) iliandaa kambi maalumu kwa ajili ya upimaji wa afya bure ambayo ilifanyika katika viwanja vya Klabu ya Leaders, Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya.

Wananchi wengi waliohudhuria walipima magonjwa mbalimbali lakini pia walipata ushauri wa kitaalamu juu ya matatizo yanayowasibu kuhusu afya zao.

Tunaamini kwamba endapo baadhi ya ushauri uliotolewa utazingatiwa na kufanyiwa kazi, wananchi wengi wataepukana na maradhi hasa yasiyoambukiza ambayo mbali na kuweka rehani maisha yao, yanawagharimu fedha nyingi, muda na maumivu ambalo ndilo jambo kubwa zaidi.

Moja ya ushauri uliotolewa katika kambi hiyo unahusu tatizo la uoni hafifu na udumavu kwa watoto linavyoweza kuepukika. Wataalamu wa afya waliwashauri washiriki kwamba njia nyepesi ya kuondokana na tatizo hilo ni kuepuka kuongeza uzito kupita kiasi ambao aghalabu unatokana na kula vyakula vyenye wanga, sukari na mafuta kwa wingi.

Ushauri mwingine uliotolewa uliwalenga wanaotumia vifaa vya mawasiliano ambavyo ni pamoja na kompyuta na simu za mkononi. Hawa wameshauriwa kutumia lenzi maalumu ili kujikinga na mionzi inayoathiri macho.

Katika hilo, wataalamu hao wa afya walisema waathirika wakuu ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano hadi 16. Mbali ya kuwashauri watumiaji kuweka vikinga mionzi, waliwataka wananchi kupima macho mara kwa mara badala ya kusubiri waathirike.

Pia walitoa ushauri mwingine ambao unalenga kundi kubwa katika jamii. Waliwashauri watu kuvaa viatu pindi wanapokuwa katika sakafu zenye marumaru ‘tiles’ wakieleza kwamba kutembea pekupeku ni hatari kwa afya ya miguu na kisigino kwani husababisha ugonjwa wa calcunus spur.

Wataalamu hao pia walizungumzia tatizo la udumavu wa watoto na kuwashauri wazazi kuwawapatia lishe bora kwani hiyo ndiyo sababu ya hali hiyo.

Walisema kuna tofauti kubwa kati ya mtoto kula na kushiba na kupata lishe bora na kwamba hayo ni mambo muhimu ya kuzingatia kwa afya na makuzi ya mtoto.

Katika lishe hawakuishia kutoa ushauri kwa watoto pekee, walisema ulaji usiofaa kwa watu wazima husababisha asilimia 80 ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Ushauri mwingine muhimu uliotolewa ni kuhusu meno. Baadhi ya wananchi wamezoea kung’oa meno wenyewe au kuomba msaada kwa wenzao hasa kwa yale ambayo hayaumi. Lakini wataalamu hao walitahadharisha kuhusu tabia hiyo wakisema ni hatari kwani inaweza kusababisha madhara makubwa.

Walisema jino lina uhusiano mkubwa na ubongo hivyo liking’olewa vibaya mzizi unaweza kukatika na kusababisha madhara makubwa.

Tunazipongeza taasisi zote zilizoshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kambi hiyo. Kwa hakika wamesaidia wananchi wengi kutambua afya zao na hivyo kujiweka katika nafasi nzuri ya ama kupata tiba sahihi au kujitunza ili waendelee kuwa na afya njema na kushiriki vyema katika shughuli za maendeleo ya Taifa lao.

Pia, tunawapongeza wananchi waliojitokeza kupima afya zao tukiamini kwamba watazingatia ushauri wa wataalamu wa afya ili kuhakikisha afya zao zinaimarika hivyo kuwapa fursa ya kufanya kazi zao kwa manufaa ya familia zao na Taifa kwa ujumla.

Msisitizo wetu upo kwenye ushauri ulitolewa ili kuepuka kupata maradhi hasa yale yasiyokuwa ya kuambukiza. Tumesikia ushauri hasa katika matumizi ya vifaa ambavyo kwa dunia ya sasa hayaepukiki; simu za mkononi, kompyuta na marumaru, tutakavyotumia vifaa hivyo kwa kuzingatia masharti yaliyotolewa, ndivyo tutakavyoendelea kufaidi matunda yake.

Haya ni mambo ambayo hayawezi kutungiwa sheria kuwalazimisha wananchi kuyafuata, ni suala la mtu binafsi kulichukua kama zingatia kwa ajili ya maisha yake na familia yake. Rai yetu ni kila mmoja kuzingatia hili kwa masilahi yake.