Utafiti uvisaidie vyama kuinua wanawake

Imepakiwa - Thursday, April 11  2019 at  11:41

 

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) umependekeza kwa vyama vya siasa mbinu kadhaa zitakazosaidia kuwapata wagombea wanawake kwa nafasi za ubunge na udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020.

Matokeo ya utafiti huo yalitolewa juzi jijini Dar es Salaam mbele ya viongozi wa vyama vya siasa na kuwataka kuanza sasa kuutumia katika kupata wagombea wanawake kwa uchaguzi ujao.

Utafiti huo uliofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya wanawake, ulifanyika katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na Mjini Magharibi kwa visiwani Zanzibar.

Vigezo sahihi vinavyotajwa na utafiti huo ni kuchambua wanawake wenye nia, kutafuta mabinti waliopo vyuoni au waliomaliza na kuchambua waliogombea ndani ya chama katika uchaguzi uliopita wa 2015.

Tunachokiona ripoti ya utafiti huo imekuja kwa wakati mwafaka kwa kuwa mwishoni wa mwaka huu nchi itakuwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwakani ni Uchaguzi Mkuu.

Licha ya juhudi zinazofanywa za kuwezesha wanawake washiriki kwenye nafasi za uongozi hasa za kugombea ndani ya vyama vya siasa, fursa hiyo bado imekuwa duni.

Pia, semina, makongamano na warsha nyingi zimefanyika za kuwajengea uwezo wanawake wa kugombea kwenye nafasi za uongozi wa kisiasa.

Miongoni mwa sababu zinazotolewa ni kwamba wanawake wenyewe hawana ujasiri wa kugombea nafasi hizo, ukosefu wa fedha, lakini kubwa ni kutoaminiwa na vyama vya siasa kwamba wanaweza kukiletea chama ushindi.

Pia, taarifa zingine zinadai wanawake wenyewe hawapendani au hawaaminiani pale mwenzao anapoomba nafasi ya uongozi kupitia chama cha siasa.

Vigezo vilivyotolewa na UDSM ni msingi mzuri wa kuvifanya vyama viweze kuwachuja wagombea wanawake na kuwapata wale wanaoamini watawaletea ushindi.

Inaweza ikawa ni kweli kwamba kuna baadhi ya wanawake ambao husukumwa kwenye nafasi za kugombea na wapambe, lakini mioyoni mwao hawana nia hiyo.

Hivyo, kuna viashiria vya ukweli kwamba mgombea asiyekuwa na nia hawezi kukiletea chama ushindi na hata kama atashinda mchango wake wa maendeleo kwa chama au wanajamii hautakuwa madhubuti.

Vyuo vikuu vingi vilivyopo Tanzania kila mwaka vinatoa wahitimu wanawake ambao kama watatumika vizuri kwenye vyama vya siasa wanaweza kuvisaidia vyama hivyo kushinda katika uchaguzi.

Pia, kuna haja kwa vyama vya siasa kuwachambua wagombea wanawake waliojitokeza kupambana na wanaume katika uchaguzi uliopita.

Tunaamini wagombea wanawake walijitokeza kupambana na wanaume kwenye kura za maoni ndani ya vyama vya siasa walikuwa na nia ya dhati, na kama watapewa nafasi katika uchaguzi ujao wanaweza kufanya maajabu.

Lakini, ni vyema vyama vya siasa vikaanza kutumia vigezo hivyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tunaamini kwenye Serikali za Mitaa ndiko maendeleo ya wananchi yanakoanzia, huko ndiko waliko wananchi wa kipato cha chini na wanaotegemea uchuuzi kama vile machinga na mama lishe.

Hivyo, wakati vyama vikijiandaa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu ni vyema vikaanza mchakato wa kutumia vigezo vya utafiti huo kuwapata wagombea wanawake