Vicoba waache kuweka mamilioni nyumbani

Imepakiwa - Thursday, September 13  2018 at  10:03

Kwa Muhtasari

Kumetokea wizi wa zaidi ya TSh48 milioni zilizokuwa zikihifadhiwa kwenye masanduku nyumbani kwa mweka hazina.

 

VIKUNDI vya Migombani Vicoba vinavyojumuisha vikundi vitatu vilivyopo Segerea, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam viko kwenye majonzi baada ya kutokea wizi wa zaidi ya TSh48 milioni zilizokuwa zikihifadhiwa kwenye masanduku nyumbani kwa mweka hazina wao.

Kuibwa kwa fedha hizo ni pigo kwa wanachama, kwani umuhimu wa Vicoba au Village Community Bank unafahamika kwamba ni mfumo wa kuweka na kukopa kwa wanachama waliojiunga kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi.

Mfumo huu umeonyesha mafanikio kwa wanachama kwa kukopeshana na kusaidiana katika matatizo mbalimbali na pia kuanzisha miradi ya kiuchumi. Kupitia vicoba jamii imepata maendeleo na Taifa nalo limenufaika.

Vicoba pia hutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara kwa wanachama kupewa fursa au kipaumbele cha kuendelezwa kiuchumi ili kuleta ongezeko na faida kwenye biashara wanazojihusisha nazo.

Hivyo, umuhimu wa vicoba kwa wananchi na Taifa kwa ujumla ni mkubwa, lakini mbali na mafunzo wanayoyapata wanachama ikiwamo utunzaji wa kumbukumbu, tatizo lipo kwenye kuhifadhi fedha kwa njia salama ikiwamo kufungua akaunti benki.

Pamoja na tahadhari zingine wanazochukua wanavikundi ikiwamo kuwa na bima ya kulinda mikopo yote inayoombwa na wanachama, bado udhibiti na utunzaji wa makusanyo ya fedha unafanyika kwa kuaminiana zaidi kuliko kufuata taratibu na kanuni za fedha.

Vikundi vingi vya vicoba vinadhibiti makusanyo ya fedha kwa kutangazwa mbele ya wajumbe wote na wahesabu fedha wanazikabidhi kwa mweka hazina ambaye atazihakiki na kuziweka ndani ya sanduku lenye makufuli matatu, huku fungo zake zikishikwa na watu tofauti.

Njia ya kutunza fedha nyingi tena mamilioni kwenye sanduku au vibubu siyo salama, ukiwasikiliza wataalamu wa mifumo ya kifedha. Masanduku kwa mujibu wa wanavicoba yanatakiwa kuhifadhi kiasi cha fedha kisichozidi TSh200,000 kutokana na hali ya usalama wa sasa. Ukichukulia mfano wa tukio la Migombani ni dhahiri kulikuwa na kasoro katika utunzaji wa makusanyo ya wanachama, ama ni uzembe kwa wanakikundi wenyewe kwa kuamua kuweka uaminifu kwa mtu mmoja kupita kiasi.

Ushauri wetu kwa vikundi vya vicoba ni huu, kwanza waache tabia ya kumwamini mtu mmoja kiasi cha kumwachia atunze fedha nyingi ndani ya nyumba yake, lakini pili wanaopewa majukumu ya kutunza fedha nyingi za kikundi wanapaswa kuacha tabia hiyo kwa kuwa ni hatari hata kwa maisha yao.

Pia, tunashauri vikundi hivi vijenge utamaduni wa kuwatumia polisi siku wanapokutana kwa ajili ya kukopa na kupokea marejesho ya wanachama.

Rai yetu kwa taasisi zinazosimamia vikundi vya mifumo ya kifedha ni kuweka kanuni ya kuwalazimisha wanavikundi kuwa na akaunti benki, kwa kuwa kuibwa kwa fedha kunawarudisha nyuma kiuchumi wanakikundi wengi.

Hata hivyo, hata utunzaji wa siri za kikundi iwe ni moja ya sharti kwa kuwa haitakuwa na maana kuwa na kikundi cha kujikwamua kiuchumi ambacho hakina taratibu za kujiweka katika mazingira salama ya wao wenyewe na fedha zao.

Wanakikundi wanatakiwa wajue kuweka fedha nyingi ndani hakuna maana zaidi ya kuhatarisha usalama wa fedha zao na kubwa zaidi ni kujirudisha wenyewe katika hali ya umaskini.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647