http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801474/medRes/2135719/-/s6t3m8/-/amaru.jpg

 

Vigogo wamiminika kumzika Kamaru

Aliyekuwa mwanamuziki wa nyimbo za Agikuyu, Joseph Kamaru  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  16:00

Kwa Muhtasari

Marehemu ameacha pengp ambalo halitazibika


 

Murang'a. Mwanamuziki wa nyimbo za Agikuyu, hasa benga Joseph Kamaru amezikwa Alhamisi nyumbani kwake Kigumo, Murang'a.

Kamaru alifariki Jumatano wiki iliyopita, katika Hospitali ya MP Shah jijini Nairobi wakati akiendelea kupata matibabu. Ibada ya mazishi ilifanyika katika shule ya msingi ya Muthithi, Kigumo alikosomea marehemu.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wa Rais William Ruto na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ambaye pia ni kinara wa upinzani ni baadhi ya viongozi wakuu nchini waliohudhuria hafla hiyo ya buriani kwa mwendazake.

Kenyatta akitoa rambirambi zake alimmiminia Kamaru sifa, hasa kutokana na nyimbo zake zilizojawa na jumbe za maadili. "Mzee ameacha pengo. Hata hivyo, tunajivunia makuu aliyotufanyia hasa kukashifu maovu," alisema Rais.

Mwendazake atakumbukwa kwa nyimbo kama 'Ndari ya Mwalimu' unaokemea uhusiano haramu na wa kimapenzi kati ya mwalimu na mwanafunzi, 'Tiga Kuhenia Igoti' wenye maana ya; koma kuhadaa korti, 'Charia Ungi (tafuta mwingine).

Kamaru alitumia talanta yake kuangazia uzinzi na ukahaba, ambapo alivikemea vikali kwa kutumbuiza kupitia nyimbo zake. Naibu wa Rais William Ruto kwenye hotu zake, alisema marehemu ameacha nembo na kuweka Murang'a katika ramani ya kaunti maarufu kwa tasnia ya muziki. "Kamaru alifanya kazi kwa bidii, na hii ni kutokana na idadi ya nyimbo alizotunga. Hiyo ndiyo sababu Murang'a inajulikana katika safu ya muziki," alieleza.

Kamaru katika kipaji chake cha uimbaji hakusita kukosoa serikali hasa ya Mwanzilishi wa taifa Jomo Kenyatta, baba yake Kenyatta na ya Rais wa pili Daniel Arap Moi zilipoenda mrama. Wakati mmoja aliandamana na Rais Moi, ambaye kwa sasa ni mstaafu kuelekea Japan. Uhusiano wake na serikali ya Rais (mstaafu) Mwai Kibaki ulikuwa wa karibu sana, kiasi cha kualikwa amuombee alipopata ajali 2002 wakati akifanya kampeni za kuwania urais.

Mwanamuziki huyu pia alitetea demokrasia na kuwepo utawala wa vyama vingi miaka ya themanini na tisini, jambo lililomghadhibisha Moi. Kiongozi wa ODM Raila Odinga akisimulia urafiki wake wa karibu na Kamaru, alisema msanii huyu ni mmoja wa mashujaa ambao Kenya inajivunia kuwa nao. "Jina la Joseph Kamaru litasalia katika kumbukumbu zetu. Visa vya mauaji ya wasichana tunavyoshuhudia sasa alivikashifu," alisema Raila.

Kamaru pia alitumia kipaji chake kukuza talanta za waimbaji chipukizi. Hadi kifo chake, alikuwa ametunga zaidi ya nyimbo 3,000. Aliaga akiwa na umri wa miaka 79.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi ni gavana Mwangi Wa Iria wa Murang'a, Ferdinand Waititu (Kiambu), Lee Kinyanjui (Nakuru), aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.