http://www.swahilihub.com/image/view/-/4657122/medRes/2040490/-/4n8p8sz/-/vifaa.jpg

 

Vijana kwa wazee 119,000 kuvuliwa ‘mkono wa sweta’ Geita

Vifaa vilivyoandaliwa kwa ajili ya kuanza tohara kwa wanaume 

Na Rehema Matowo

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  09:58

Kwa Muhtasari

Tohara hupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60

 

 

Geita. Ili kuhakikisha unapunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60, mkoa wa Geita umelenga kuwafanyia tohara wanaume 119,000 ifikapo Oktoba.

Takwimu zinaonyesha maambukizi ya VVU mkoani Geita, ni asilimia tano na inaelezwa sababu kubwa ni muingiliano wa wananchi kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu.

Akizungumza jana, mratibu wa kuzuia Ukimwi mkoani hapa, Joseph Odero alisema zoezi la kuwafanyia tohara wanaume lilianza tangu Oktoba.

Odero alisema wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa hawakuwa na utamaduni wa kutahiriwa, hivyo kusababisha uwapo wa idadi kubwa la wanaume wasiotahiriwa.

Alisema lengo ni kupunguza maambukizi ya Ukimwi na kwamba, utafiti unaonyesha kuwa wanaume ambao hawajafanyiwa tohara wanaathirika zaidi ikilinganishwa na waliotahiriwa.

Mratibu huyo alisema kampeni hiyo inaanzia kwa watoto wa miaka 10 na watu wazima hata mzee ambaye ataridhia kufanyiwa.

Naye mshauri wa huduma za tohara kutoka shirika la Intrahealth, Peter Sewa alisema tayari wanaume 71,000 mkoani hapa wamefanyiwa tohara sawa na asilimia 60 ya lengo.

Sewa alisema utafiti unaonyesha tohara hupunguza maambukizi ya Ukimwi kwa asilimia 60 kwa wanaume na asilimia 30 kwa wanawake na kwamba, kampeni kubwa wameiweka eneo la mji mdogo wa Katoro ambako maambukizi ya Ukimwi ni asilimia saba.

“Tumelenga zaidi vijana kati ya miaka 20 na 29 kwa kuwa ndilo kundi linalofanya ngono zisizo salama, awali waliamini sisi ni Freemason lakini kutokana na elimu wanayopewa wamebadilika, mwitikio umekuwa mkubwa,” alisema.

Kampeni hiyo mwaka 2016, ilipanga kuwafanyia tohara wanaume 39,000 wa wilaya za Chato na Geita, lakini walivuka lengo na kufikia 41,000.

Katika malengo ya mradi huo kwa mwaka 2014/17, ulilenga kuwafikia wanaume 210,000 lakini ilishindikana kutokana na halmashauri tano kuondolewa kwenye mpango huo.