http://www.swahilihub.com/image/view/-/5034988/medRes/2287403/-/nipynm/-/vita+pic.jpg

 

Vita dhidi ya dawa za kulevya iwe endelevu

Baadhi ya aina ya dawa za kulevya 

Na Mwandishi wetu

Imepakiwa - Thursday, March 21  2019 at  08:31

 

Kati ya vitu muhimu tunavyotakiwa kupambana navyo kwa nguvu zote ni dawa za kulevya.

Dawa hizi huathiri nguvu kazi kwa kiasi kikubwa. Na kama vile wauzaji wana malengo ya kuua vijana wengi, wateja wao wakuu ni vijana hasa wadogo.

Hawa, endapo watakuzwa kwa misingi inayotakiwa, ndio watakaokuwa viongozi wa jamii na familia zao siku za usoni.

Kuna kila haja jamii kushirikiana kuvipiga vita vitendo vyovyote vinavyoonyesha dalili ya kuhamasisha biashara hii kwani athari zake ni kubwa. Hakuna faida zaidi ya watu wachache kujitengenezea kipato haramu kinachoacha majonzi kwa jamii.

Vita dhidi ya dawa za kulevya huwa na athari kwenye shughuli za ujasiriamali hasa taasisi ndogo za fedha ambazo ni nguzo muhimu ya huduma za fedha kwa wajasiriamali wa chini na kati.

Kama ilivyokuwa maeneo mengine, ujasiriamali na biashara ndogo zinazojumuisha taasisi ndogo za fedha zinaathirika kutokana na lolote linaloendelea kwenye jamii inayojihusisha nayo kila siku kutokana na bidhaa au huduma zake.

Kutokana na ukweli kuwa watumiaji na waathirika wengi wa dawa za kulevya ni vijana wa rika la uzalishaji wenye nguvu za mwili na akili, basi moja kwa moja dawa hizi zinaharibu rasilimali watu ambayo ingeweza kufanya kazi kama wasaidizi au wamiliki wa biashara hizo.

Vijana hawa, kama hawatakuwa wamiliki wa biashara basi wanaweza kufanya shughuli nyingine itakayochangia kuimarisha na kuongeza mnyororo wa thamani ukapata fedha na faida nyingine za kutoa huduma.

Vilevile, taasisi ndogo za fedha zinawahitaji vijana wasomi kwa ajili ya uendeshaji, uongozi na ubunifu utakaofanikisha huduma zenye tija kwa wananchi na kukua kwa ofisi husika.

Dawa hizi zinafanya idadi yao kupungua kwenye soko la ajira, hivyo kuwafanya kuwa adimu kusimamia taasisi hizi pendwa hivyo kupunguza na kupoteza nafasi ya kuwa na wataalamu wengi kwenye sekta hii muhimu ya fedha.

Dawa za kulevya zinaua soko la bidhaa na huduma za wajasiriamali na taasisi ndogo za fedha kutokana na ukweli kuwa uwezo wa kununua bidhaa kwa watu wengi utakuwa unapungua kutokana na uwapo wa waathirika ambao hawana nguvu ya kufanya kazi.

Licha ya hivyo, kukosa kipato cha uhakika kutokana na kushindwa kufanya kazi kunawanyima nafasi na uwezo wa kununua bidhaa na huduma za wajasiriamali na itakayokuwa inawalea waathirika hawa kuanzia ngazi ya familia uwezo wao wa kiuchumi utapungua kutokana na gharama za kufanya hivyo.

Kwa sababu gharama za kuwalea vijana hawa ni kubwa kiasi cha kuyumbisha shughuli za wajasiriamali, athari hizo hufika mpaka kwenye taasisi ndogo za fedha ambazo hupata ugumu wa kufanya biashara na kundi la watu wa namna hii kwa sababu kufanya hivyo ni kuhatarisha fedha zao.

Kupungua na kupotea kwa usalama kwenye mazingira ya kufanyia kazi kwa wajasiriamali na taasisi ndogo za fedha, kutokana na kukua kwa kundi la waathirika wa dawa za kulevya hasa wenye kipato cha chini mara nyingi huwafanya wahusika wajiingize kwenye uhalifu wakati mwingine wa kutumia silaha ili kutafuta fedha za kuwawezesha kununua tena dawa hizo.

Ikifikia kwenye hatua hii wajasiriamali wadogo pamoja na mali zao wanakuwa hatarini kuvamiwa na kuporwa au wakati mwingine kupoteza maisha kitu kinachodhohofisha ukuaji wa uchumi.

Suala hili pia huziathiri taasisi ndogo za fedha na kuziweka kwenye kwenye hatari ya kuvamiwa na kupoteza mtaji hivyo huleta hasara na kupoteza muelekeo wa watu wengi sana wanaonufaika na huduma zao. Pasipo kuwapo na amani na utulivu ni ngumu kutengeneza uchumi imara na wenye nguvu.

Kujihusisha na dawa za kulevya ni kosa kisheria hivyo ni vizuri taasisi na ofisi husika zikaendelea kupambana na tatizo hili bila kuchoka kwa ushirikiano na wadau wengine kwa kufuata utaratibu ili kuhakikisha vijana wanaacha kujihusisha nazo na kufikiria kufanya mambo tofauti yenye tija kwa jamii na taifa kwa jumla.

Tufumbue macho na kuingia kwenye ujasiriamali, kila mtu kwa nafasi yake, ili kuitengeneza Tanzania ya viwanda na uchumi wa kati.

Kufanikiwa kwenye ujasiriamali kuna hitaji mambo mengi ikiwamo uvumilivu na ubunifu. Haya yote yanaweza kufanywa na vijana wasiotumia dawa za kulevya.

Mwandishi ni mtaalamu wa taasisi ndogo za fedha. Anapatikana kwa namba 0657 157 122