http://www.swahilihub.com/image/view/-/2252568/medRes/711711/-/8s0b14/-/592361-01-02.jpg

 

Vladimir Putin: Ametawala Urusi kwa miaka 18

Vladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin. Picha/AFP 

Na SAMMY WAWERU, MASHIRIKA na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  11:50

Kwa Muhtasari

Mei 28, 2018, Vladimir Putin aliapishwa rasmi kwa muhula wa nne kuwa Rais wa Urusi baada ya kushinda uchaguzi mwezi Machi.

 

MNAMO Mei 28, 2018, Vladimir Putin aliapishwa rasmi kwa muhula wa nne kuwa Rais wa Urusi baada ya kushinda uchaguzi mwezi Machi.

Baada ya kula kiapo, Rais huyo ambaye amekuwa mamlakani kwa muda wa miaka 18 kama rais na waziri mkuu alisema ataangazia kuboresha maisha ya watu wa kawaida na kwamba kwa miaka 6 ijayo uchumi wa Urusi utaimarika pakubwa.

“Tunahitaji Urusi yenye nguvu,” akasema Putin kwenye hotuba yake Kremlin, Moscow. Hata hivyo, wapinzani wake wanamkosoa wakifananisha muda wake wa uongozi kama utawala wa mfalme uliojawa na udikteta.

Urejeo wake mamlakani kwa awamu ya nne, ulisababisha maandamano katika mji mkuu wa Urusi, Moscow na miji mingine nchini humo.

Rais Putin alichaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo 2000. Mwaka wa 2004, aliwania muhula mwingine kabla ya kujiuzulu 2008 ili kuhudumu kama waziri mkuu chini ya mrithi wake Rais Dmitry Medvedev.

Katiba ya Urusi hairuhusu kiongozi kutawala kama rais kwa zaidi ya mihula miwili mtawalia, hivyo basi kumshurutisha Putin 2008 kuwa Waziri Mkuu.

Hata hivyo, mwaka wa 2012 Putin alirudi mamlakani kama rais, muhula wa miaka sita. Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 64, atakamilisha muhula wake wa nne mnamo 2024.

Bw Putin alikuwa afisa wa ujasusi, aliyegeuka kuwa rais. Alizaliwa Oktoba 7, 1952. Alisomea uanasheria na kujiunga na kikosi cha Polisi wa KGB akiwa jasusi Ujerumani Mashariki iliyokuwa na Ukomyunisti 1997. Baada ya kuhudumu kama msaidizi mkuu wa meya wa St Petersburg, aliingia ikulu chini ya Boris Yeltsin na kuteuliwa kuwa mkuu wa kitengo cha polisi cha FSB mnamo 1999.

Aidha, alichaguliwa kuwa waziri mkuu na kuwa kaimu rais baada ya Rais Yeltsin kujiuzulu. Mwaka wa 2000 alichaguliwa Rais na kuhudumu mihula miwili ya miaka minne. Hata hivyo, 2008 katiba haikumruhusu kuhudumu muhula wa tatu mtawalia. Alishangaza watu kwa kurudi wadhifa wa waziri mkuu, huku mshirika wake Dmitry Medvedev akiwa Rais.

Mnamo 2012 alichaguliwa tena kuwa rais kwa muhula wa miaka sita. Kipindi cha muhula kiliongezwa kutoka miaka minne hadi sita, baada ya kufanya mabadiliko ya uongozi wa urais aliporejea mamlakani.

Mei 2018, alihifadhi urais kwa awamu ya nne. Licha ya wapinzani wake kumkosoa raia wa kawaida nchini humo yaani Warusi, walikaribisha kwa utulivu urejeo wake. Walitaja uongozi wa kwanza wa Rais Putin wenye manufaa baada ya kudhibiti mfumko wa bei ya bidhaa Urusi.

Hali kadhalika, walimmininia sifa kwa kufufua idara husika za serikali zizolififia awali. Bw Putin aliongeza umahiri wake uongozini kwa kuvipa uhuru vyama vya kisiasa ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari. Pia, alipunguza ushuru uliotozwa kwa mali ghafi ya mafuta.

Mgogoro

Hata hivyo, uamuzi wake wa kuihamisha rasi ya Annex Crimea kutoka Ukraine mwaka wa 2014 ulizua mgogoro mkubwa na kuleta vita baridi, iliyosababisha vikwazo vinavyoendelea kutoka Magharibi hadi sasa.

Ni chini ya utawala wa Rais Putin, ambapo Urusi inadaiwa kuingililia kati uchanguzi wa urais wa Marekani mnamo 2016 na kusaidia Bw Donald Trump kuibuka mshindi. Rais Trump alitoana kijasho na Bi Hillary Clinton.

Madai ya Urusi kuboronga uchaguzi huo kwa manufaa ya Trump yalizua utata katika mahusiano ya kimataifa. Hata hivyo, Urusi ilipinga vikali kuhusishwa na uchaguzi wa Marekani.