Vyama vitalazimisha kuteua wenye ulemavu

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba 

Imepakiwa - Thursday, March 14  2019 at  09:47

 

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ameishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka mkazo kwa vyama vya siasa nchini kuwa na wagombea wenye ulemavu kwenye nafasi za uongozi wa kuchaguliwa.

Kibamba anajenga hoja kwamba jambo hilo likiwa kigezo cha kupitisha orodha ya wagombea wa chama husika, itahamasisha kulikumbuka kundi la watu wenye ulemavu.

Hoja ya kuvitaka vyama vya siasa kuwateua wagombea kutoka kundi hilo haijaanza sasa, hata kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopita kuna baadhi ya watu wenye ulemavu walilalamika kuwekwa kando na vyama vya siasa.

Tunachokiona hata yale makubaliano kwamba vyama vyote vya siasa vitakavyopata fursa ya kuteua wabunge wa viti maalumu, vitoe pia nafasi kwa walemavu ili wapate uwakilishi bungeni, hayatekelezwi ipasavyo.

Kigezo kikubwa ambacho kimekuwa kikiangaliwa na vyama vya siasa katika kuteua wagombea ni uwezo wake wa kukiletea chama ushindi.

Wanasiasa wenye ulemavu ambao walijitokeza kuomba nafasi za kuteuliwa na vyama kugombea uongozi wa kuchaguliwa, wengi hawakupitishwa na vyama hivyo.

Kuna mwanasiasa mwenye ulemavu wa macho aliwahi kulalamikia changamoto wanazozipata wenye ulemavu ikiwamo kutoaminiwa na vyama kama kweli wanaweza kuviletea ushindi.

Mwanasiasa huyo alikuwa akieleza kusikitishwa kwake na namna jina lake lilivyokatwa na vikao vya mwanzo vya chama chake.

Hoja ya Kibamba imekuja wakati mwafaka, kwamba mbali na kuiomba NEC kuweka kigezo cha umuhimu wa kundi la watu wenye ulemavu, kuna haja ya Serikali kupeleka muswada bungeni kutunga sheria itakayovilazimisha vyama kuthamini kundi hilo wanapoteua wagombea. Kuviacha vyama vya siasa viamue vyenyewe idadi na namna vinavyoona inafaa katika kuteua wagombea kutoka kwenye kundi la walemavu haitakuwa sahihi.

Tunadhani umefika wakati kwa vyombo vya kutunga sheria kuona umuhimu wa kuweka sharti la ulazima wa kuwapo watu wenye ulemavu katika majina yatakayopelekwa NEC na vyama vya siasa kwa ajili ya uteuzi.

Watu wenye ulemavu ni raia wa Tanzania wenye haki zote na wengi ni wasomi wakiwamo maprofesa, madaktari na wengine wana viwango vya kawaida vya elimu vinavyowawezesha kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Hivyo, tunaamini kwamba kundi la watu wenye ulemavu halipaswi kuachwa nyuma, ni watu wenye mchango mkubwa kwa ujenzi wa Taifa kama watapewa nafasi.

Hata hivyo, ndani ya Bunge ambacho ni chombo cha kutunga sheria, hakuna wabunge wa kutosha ambao wanatoka kundi la watu wenye ulemavu.

Hivyo, ni muhimu kutambua haki ya watu wenye ulemavu katika kugombea nafasi za uongozi kisheria badala ya kuwapa nafasi hizo kama hisani au fadhila.

Tunaamini kwamba, kwa kuwapa fursa watu wenye ulemavu kwenda kushiriki siasa za majukwaani kwa kushindana kwa hoja, kutawaongezea kujiamini na vilevile kuwatia moyo walemavu wengine wasijione wanyonge na watambue umuhimu wao katika kushiriki shughuli za ujenzi wa Taifa.

Rai yetu kwa Serikali ni kuwa, ni vyema ipeleke muswada bungeni kwa ajili ya kutunga sheria ya kuvitaka vyama vya siasa kutambua umuhimu na mchango wa kundi la watu wenye ulemavu katika kujenga Taifa.