Wafanabiashara mtandaoni acheni ubabaishaji

Na  Emmanuel Mtengwa

Imepakiwa - Friday, May 10  2019 at  13:34

 

Mitandao ya kijamii imekuja na fursa nyingi katika
maisha ya binadamu. Ni muhimu kwa wajasiriamali
wanaochipukia kwa kuwa ni mojawapo ya nyenzo za
masoko.
Kutokana na mapinduzi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (Tehama), simu za kiganjani ni muhimu
katika kurahisisha shughuli hiyo.
Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamewafanya
wajasiriamali kubuni mbinu za kufanya biashara
mtandaoni.
Biashara kwa njia hiyo inaonekana kuwa chaguo la
wajasiriamali wengi hasa vijana.
Huenda njia hii inapendwa na wengi licha ya kwamba
inaendana na wakati, lakini inawezekana ikawa na unafuu
hasa katika kutangaza bidhaa kwa kuwa haihitaji
uwekezaji mkubwa.
Mathalani, katika biashara hiyo ya mitandaoni
kinachohitajika ni simu “smartphone” au kompyuta yenye
kuunganishwa na mtandao wa intaneti pamoja na akaunti
ya mitandao ya kijamii au kuwa na tovuti.

Ukiwa na vitu hivyo na bando kwenye simu ya
‘smartphone’ unaweza kuwafikia wateja wengi kwa
wakati moja ukizingatia kumekuwa na ongezeko la
watumiaji wengi wa intaneti kila kukicha.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya
Desemba 2017; imeonyesha kuwa idadi ya watumiaji wa
intaneti imefikia watu milioni 23.
Matumizi haya ya intaneti yamepanua wigo wa biashara,
siyo ndani ya nchi tu, bali kimataifa.
Mitandao kama Facebook, Twitter, WhatsApp, Youtube,
Instagram na Telegram hivi sasa imekuwa chaguo la
wengi ikiwasaidia kutangaza bidhaa na kuwafikia wateja
kwa urahisi.
Kupitia mitandao hiyo, vijana wengi wajasiriamali
wanaweka picha za bidhaa ikielekeza bei na mahali
inakopatikana.
Mathalan, kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp,
mjasiriamali anaweza kuposti bidhaa nyingi kwenye
‘status’ ikiambatana na maelezo ya ziada yakibainisha bei
ya bidhaa na mahali bidhaa inapopatikana.
Njia hizi za matangazo zinaonekana kuwapa ahueni
wajasiriamali kutokana na ukweli kwamba, kutangaza
bidhaa kupitia vyombo vya habari kama televisheni, redio
na magazeti ni gharama kubwa.

Naiona biashara ya mtandaoni ikiwa mkombozi kwa
wajasiriamali hasa kwa kipindi hiki ambacho vijana
wengi wanahitimu katika ngazi mbalimbali za vyuo na
kuhangaika mtaani bila ajira.
Pamoja na kwamba biashara hii inashamiri, nawiwa
kuwakumbusha wajasiriamali hawa kuwa kitu muhimu
katika biashara ni uhalisia katika matangazo yao ili
kuwaridhisha wateja. Hakuna sababu ya kumdanganya
mteja kwa kuweka picha za bidhaa ambazo mteja
akizihitaji unashindwa kumtimizia.
Nalisema hili kutokana na ukweli kwamba,
wafanyabiashara wengi wa mitandaoni wamekuwa na
tabia ya kutangaza bidhaa ambazo mteja akizihitaji
wanashindwa kumpatia kwa kuwa hawana bali
wameziweka kwa ajili ya kuwavutia wateja.
Huu ni udhaifu unaojitokeza kwa wengi waliokimbilia
soko la mtandaoni. Kwa namna nyingine, huu naweza
nikauita ulaghai.
Unaweka picha zinazoonyesha bidhaa nzuri lakini mteja
akihitaji unamzungusha mpaka anakata tamaa.
Nakumbuka miezi kadhaa, nilipitia “status” ya WhatsApp
ya mmoja wa marafiki zangu waliojikita kwenye soko la
mitandaoni, nikaona ameposti mashati mengi na
nikapenda moja, nikamuulizia bei na nikaliagiza baada ya
kuridhika na bei.

Ilipita wiki moja bila mafanikio na kila nikimuulizia
ananijibu kuwa anatafuta, baada ya wiki moja nilikata
tamaa na sikuendelea kumuulizia tena.
Yawezekana hao ni mfano ambao kiuhalisia umeakisi
uhalisia wa wafanyabiashara wengi wa mitandaoni na
huenda wananchi wengi wanakutana na huo ubabaishaji.
Simaanishi kuwa wote wanaofanya biashara mitandaoni
wana tabia zinazofanana. Wapo wanaotangaza vitu
ambavyo wana uwezo wa kuvimudu kumpatia mteja
atakapohitaji.
Ndiyo maana nimeandika makala haya, kuwaangazia
wale ambao wanachokitangaza ni tofauti na kile
walichonacho nikiamini kuwa, unapomtangazia mteja ni
mkataba kuwa utamtimizia pale atakapohitaji kununua.
Unaposhindwa kumuuzia kile ulichotangaza unamkatisha
tamaa.
Rai yangu kwa wajasiriamali ambao wameamua kutumia
fursa ya soko la mitandaoni, kuweni wakali kwa kuposti
vitu ambavyo mna uwezo wa kumpa mteja pale
anapohitaji. Hii itawajengea uaminifu kwa wateja ikiwa ni
njia mojawapo ya kukuza biashara.
Ninachoamini, ukimpa mteja kile anachohitaji, huwezi
kumpoteza na pengine anaweza kuwa daraja
kukuunganisha na wateja wengine.

Kikubwa ni kuwa mwaminifu kwa wateja kwa kutangaza
bidhaa ambazo una uhakika wa kuwapa wateja
wanapozitaka, kinyume na hapo naona ukiwapoteza
wateja na hali hii ikijitokeza ni dalili tosha kuwa biashara
yako inaenda kufa.
Uchambuzi huu umeandikwa na mwandishi wa gazeti hili
anayepatikana kwa simu namba; 0753-590823