Wafikisha miezi minane bila kulipwa mishahara

Na Sanjito Msafiri, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  14:08

Kwa Muhtasari

Tangu tujiunge na kampuni hii tulilipwa mishahara ya miezi mitatu tu

 


 

smsafiri@mwananchi.co.tz

Pwani. Kuchelewa kulipwa na wateja wake kumeiingiza kwenye lawama kampuni binafsi ya ulinzi ya PRC Associates Security Tanzania, baada ya wafanyakazi wake kuituhumu kuwa imekiuka agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola la kutaka kampuni hizo kuwalipa mishahara wafanyakazi wake kila mwezi.

Akiwa ziarani wilayani Bunda, Mara hivi karibuni, Waziri Lugola alitoa siku 30 kwa kampuni za ulinzi nchini kujirekebisha juu ya kasoro mbalimbali ikiwamo kutowalipa mishahara wafanyakazi wao.

Wafanyakazi wanadai hawajalipwa mishahara yao kwa miezi minane ilhali kampuni hiyo imeingia mkataba wa ulinzi na kiwanda cha zamani cha Tamco, eneo ambalo linatumiwa na wawekezaji mbalimbali.

Hata hivyo, akizungumzia kwa simu, kiongozi wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Pantaleo Butunga alikiri kutolipa mishahara wafanyakazi hao na kwamba sababu kubwa ni kutolipwa na wateja wao.

Pia, Butunga alisema suala hilo kwa sasa linashughulikiwa na ngazi za juu serikalini na litapata ufumbuzi karibuni.

Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walioomba kutotajwa kwa sababu za usalama, walilieleza gazeti hili juzi kuwa wanaishi kwa shida kutokana na kutolipwa mishahara yao kwa miezi minane.

“Tangu tujiunge na kampuni hii tulilipwa mishahara ya miezi mitatu tu nayo tulipewa baada ya kumfungia geti Mzungu mmoja ambaye ni mmoja wa wawekezaji ndani ya eneo hili (Tamco),” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.