Wakati ni sasa wa kuitazama elimu yetu

Na Isaack Msawasi

Imepakiwa - Tuesday, April 16  2019 at  12:14

 

Mtunzi maarufu wa vitabu wa Brazil, Paulo Coelho anasema: “Kwa kuishi, tunajifunza; lakini kile tunachojifunza zaidi ni kujua kuuliza maswali vizuri na ya maana”. Shule isiyochochea udadisi, maswali, ubunifu na utu ni gereza linaloua vipaji. Elimu lazima itupe utamaduni wa kukubali ujasiri na si kupandikiza hofu na uongo.

Kadri tusomavyo lazima elimu iturudishe kwenye hali halisi ya mambo na kuleta mabadiliko sio kurandaranda katika nadharia huria.

Niwape kisa binafsi. Nilitoroka na kwenda kujiandikisha darasa la kwanza kijijini kwetu mwaka 1995. Nikarudishwa kwa kisingizio kuwa bado mimi mdogo, na niliambiwa maneno haya: “mwanangu maisha sio kukimbia, ni mchakamchaka”.

Nilikuwa napenda kucheza mpira na kuchora madudu. Kwangu michezo ilikuwa sehemu ya madarasa, sikujiona mjinga sina kitu kichwani. Kuna masomo niliyapenda, lakini kuna mengine hayakunipenda.

Mazingira ya shule yalikuwa magumu na kila mara nilifukuzwa kwa kukosa ada na michango mbalimbali. Maisha ya walimu, viboko na adhabu vilifanya kuchukia shule. Lakini zaidi, nilichukia utamaduni wa kukariri milima, majina ya maraisi, mabara na historia za ng’ambo. Sikufundishwa nidhamu ya kazi, fedha, muda, kujiajiri, vitu ambavyo ni muhimu katika maisha ya sasa.

Tulijifunza machache yanayohusu Tanzania na historia yake. Na mpaka leo sijui kwa nini walimu walikuwa wanatangaza mwanafunzi wa kwanza na yule wa mwisho kwenye mitihani.

Kutokana na hilo nilikua nikiamini kuwa maisha ni mashindano kuliko ushirikiano, ni bahati kuliko kazi. Wanafunzi wa kwanza walionekana ni wa kipekee, walitengwa na sisi. Huu ulikuwa ubaguzi. Ulikuwa mwenendo unaopingana na dini na kupindisha falsafa ya Azimio la Arusha lililohimiza jamii moja ya udugu, kujitegemea, uhuru na haki.

Shule ilinipa kichefuchefu na baadaye nilienda shuleni kwa amri si kwa kupenda. Kule katika dini hasa kanisani, tuliambiwa siri ni kukariri bila akili ya ziada. Tulikuwa tunajumlishwa kama kundi la kondoo, wote sawa sawa hata namna ya kufikiria. Aliyefikiria tofauti tulimcheka na kumuita njiti na msaliti wa darasa. Na hili linaendelea katika sekta zetu huko bungeni, shuleni, vyuoni na kwenye mashirika mbalimbali.

Kumbe taasisi za elimu bila kuwa makini, ni mashine ya kuua vipaji vya watoto, kwani watoto wanageuzwa watu wazima kabla ya wakati wao. Kibaya zaidi hata wazazi wanachangia kwa kutaka watoto wao watoke shule wakiwa wamefaulu mitihani na kuwa wafanyakazi wazuri.

Badala ya kutaka raia na watu wema tunakazia kuzalisha wafanyakazi na wateja wa masoko. Mwanafalsa Nietzche alipinga sana ukondoo. Alifuata mkondo tofauti. Alikuwa mbuzi mtukutu.

Shuleni pia sikufurahia kazi ngumu mashambani, kuosha vyombo, kuteka maji nyumbani kwa walimu, kuwaletea kuni na kusafisha nyumba za walimu. Shule na elimu havikuoana, hivyo havikunivutia, vilivutana. Lakini kwa majaliwa nilifaulu.

Leo hii nikitazama na kuchungulia mazingira mengi ya wadogo zangu hayajabadilika. Mazingira bado si ya kufaulisha wala kufurahisha. Hii, inanipa hamasa ya kupigania elimu bora zaidi.

Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema: “Wengine hufikiri kuwa kujielimisha ni kujua kusoma na kuandika. Hilo ni kosa lakini si kubwa kama la pili kwamba viongozi wetu, hufikiri kuwa wanajua kila kitu na hawana haja ya kujifunza jambo lolote hasa kutoka kwa wananchi wao. Bado kuna umbali mrefu kati ya wasomi wetu na hali halisi ya wananchi wengi.

Kama tunataka kujenga nchi yenye uchumi wa kati katika karne hii ya teknolojia na ushindani unaoletwa na utandawazi, lazima tuwekeze mno katika elimu, hasa elimu ya msingi, vyuo (ufundi na vikuu) pamoja na tafiti mbalimbali.

Sawa tuwape watoto wetu, simu na iphone wachezee ‘games’ lakini vitabu ni muhimu zaidi…Mzazi uwasomee habari, wasikilize wanaposoma, tengeni muda wa kusimuliana hadithi na watoto au wanafunzi wako.

Usipokuwa tayari kusikiliza stori ndogo ndogo za mwanao leo akiwa mdogo, akikua utatamani akwambie mambo yake muhimu lakini hatokuwa tayari.Unayoyaona madogo leo kwa mtoto ni mazito. Sikiliza.

Tuache ukasuku na kumwezesha mwanafunzi kufikiri tofauti na nje ya boksi. Elimu lazima ilete uhuru na kujitegemea. Ilete ubunifu kama ule wa kujiajiri.

Isaack Msawasi ni mdau wa elimu