http://www.swahilihub.com/image/view/-/4803332/medRes/2138837/-/d624xf/-/franc.jpg

 

Wamiliki wa matatu zisizofuata sheria za Ntsa na trafiki kukamatwa

Mkurugenzi mkuu wa Ntsa, Francis Meja  

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  16:43

Kwa Muhtasari

Wamiliki wa matatu wahakikishe yamefuata kanuni kabla ya kuingia barabarani, la sivyo mkono wa sheria utawaandama

 

Nairobi. Halmashauri ya kitaifa ya usalama na uchukuzi (Ntsa) imesema itawwadhibu wamiliki wa matatu zisizofaa kuwa barabarani ilhali zinaendelea kuhudumu.

Imesisitiza kwamba haitaruhusu matatu yoyote inayokiuka sheria za trafiki kubeba abiria. Ntsa ilitoa msimamo huu Alhamisi, siku moja baada ya taifa kupoteza watu 56 katika iliyotokea eneo la Fort Tenan, Kericho, barabara kuu ya Kisumu-Muhoroni.

Mwenyekiti wa bodi ya Ntsa Jackson Waweru aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kuwa wamiliki wa matatu wahakikishe kuwa magari yao yamefuata kanuni za Ntsa na trafiki kabla ya kuingia barabarani, la sivyo mkono wa sheria utawaandama.

"Tutakamata wamiliki wa matatu zisizofuata sheria za Ntsa na trafiki. Si ombi tena, lazima magari yao yawe katika hali tunayotaka," alisema Waweru. Baada ya ajali ya Kericho, ilibainika kwamba matatu iliyosababisha maafa haikuwa na leseni ya kuhudumu usiku na ilizidisha idadi ya abiria. Ajali hiyo ilitokea asubuhi ya kuamkia Jumatano.

Aidha, basi hilo lilitakiwa kubeba abiria 62 lakini Ntsa ilisema lilikuwa na abiria 71. Watu 16 waliripotiwa kupata majeraha mabaya. Mmiliki wake pamoja na dereva walifikishwa kortini jana kwa mashtaka ya mauaji. Inasemekana kwamba dereva juyo ana umri wa miaka 72.

Mkurugenzi mkuu wa Ntsa Francis Meja alisema sheria za kudhibiti miaka kwa wanaofaa kuwa madereva hazijatiliwa maanani, akiongeza kuwa ni suala linalofaa kujadiliwa kwa kina na washikadau husika. "Ajali nyingi zinazotokea nchini husababishwa na vijana walio kati ya miaka 15-30. Hili ni jambo tunalofaa kulitathmini kwa undani," alieleza Meja.

Mkutano huo ulihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa idara ya usalama ikiongozwa na Inspekta Mkuu wa Polisi (IG) Joseph Boinnet na Msemaji wa Polisi Charles Owino. Inspekta Boinnet, alisema maafisa wote wa trafiki waliokuwa zamu barabara ilikopita basi hilo wataadhibiwa. Alisema mbali na maafisa wa trafiki kuwa barabarani washirikishi wa kaunti na makamanda wa polisi wanafaa kuwajibikia usalama katika barabara.