http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930862/medRes/2221332/-/oyg0x0/-/baa.jpg

 

Wamiliki washauri jinsi ya baa kukesha bila kero

Baa 

Na Mwandishi wetu, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  14:09

Kwa Muhtasari

Baa zilizopo maeneo ya makazi zitumie teknolojia ya kuzuia sauti

 

Dar es Salaam. Huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiandaa utaratibu ili baa zifanye kazi kwa saa 24, wamiliki wamesema kupunguza sauti ya muziki ni moja ya mambo yatakayopunguza kero kwa wananchi.

Makonda alitoa ahadi hiyo takribani wiki moja iliyopita wakati akizungumza na vyombo vya ulinzi na usalama, wakuu wa wilaya, makatibu tawala na maofisa wa TRA wa mkoa kuhusu mkakati wa ukusanyaji mapato bila kuwabugudhi wafanyabiashara, akisema anaandaa utaratibu ili wafanye biashara kwa saa 24.

Kwa sasa wamiliki wa baa wanapaswa kuuza vinywaji vyenye kilevi kuanzia saa 10:00 jioni na kufunga baa saa 5:00 usiku.

Watejwa wanaokutwa wakinywa nje ya muda huo, hukamatwa na polisi lakini ni wachache wanaochukuliwa hatua za kisheria.

Jana, Makonda aliieleza Mwananchi kuwa utaratibu wa baa kufanya kazi kwa saa 24, kwa zile ambazo zipo katika maeneo ya makazi, sasa zijipange kuweka vizuizi vya sauti.

Alisema baa ambazo hazitaweza kufanya hivyo watakubaliana na uongozi wa serikali zao za mitaa nini cha kufanya ili starehe zisiwe karaha kwa watu wengine.

Meneja wa baa ya Hongera iliyopo Sinza, Kajetan Tesha alisema kila mmiliki wa baa asipige muziki kuanzia saa 6:00 usiku na akikiuka hatua za kisheria zichukuliwe.

Suala la sauti ya muziki pia lilizungumzwa na meneja mkuu wa baa ya Uhuru Peak iliyopo Kinondoni, Deogratius Mtei aliyesema serikali ya mkoa inaweza kuzuia biashara kufanywa kwa ya saa 24 katika makazi.

“Lakini pia wafanyabiashara tunaweza kuweka sound proof (kizuio cha sauti kusambaa) kama katika baa yangu kwa sababu niko kwenye makazi,” alisema.

Meneja mkuu wa Rombo Green View iliyopo Shekilango, John Masawe alisema baa zilizopo maeneo ya makazi zitumie teknolojia ya kuzuia sauti isisambae au kuzima muziki kuanzia saa 6:00 usiku.

Ushauri kama huo ulitolewa na meneja wa baa ya Sugar Ray iliyopo Sokota wilayani Temeke.

“Leseni zote huwa zinawekewa masharti. Huwezi kuwa kinyume. Sasa, utaratibu watakaouweka unaweza kuangalia mazingira ya baa husika. Wanaweza kuzima kabisa wakati wa usiku au kupunguza sauti ya muziki,” alisema.

Hata hivyo, meneja wa Klabu ya Wazee, iliyopo wilayani Ilala, Richard Leticia alisema hana sababu ya kurejesha utaratibu wa biashara ya kufanywa kwa saa 24 kwa kuwa inasababisha kero kwa wakazi.

Wakazi wanaoishi karibu na maeneo yenye baa walitofautiana kuhusu suala hilo, baadhi wakishauri utaratibu mpya uondoe kero wakati wa usiku na wengine wakitahadharisha dhidi ya matukio ya uhalifu.

“Kama wanataka kurejesha saa 24 ni sawa, lakini serikali iweke utaratibu mzuri. Naamini watakuwa wamejipanga kwa utaratibu mzuri,” alisema Bibi Ridhiwani Mohammed.

Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alipendekeza utaratibu utakaoanzishwa uandaliwe sheria ndogo katika ngazi ya halmashauri ili kuhalalisha kisheria badala ya kutekelezwa kwa matamko.

Pia alisema suala hilo halkiathiri mapato ya halmashauri bali Mamlaka ya Mapato kwa kuwa wao huchukua mgao wao wakati wa kutoa leseni.