http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928794/medRes/1768782/-/x4094ez/-/erio.jpg

 

Wanachama 900 NSSF wawasilisha madai feki

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio 

Na Kelvin Matandiko, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  10:55

Kwa Muhtasari

Madai hayo yana thamani ya  Sh6.9 bilioni, yalinaswa kupitia ukaguzi maalum

 

kmatandiko@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Changamoto mpya ya uaminifu imejitokeza katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), baada ya kubaini kuwa wanachama wake zaidi ya 900 wamewasilisha madai feki ya kujitoa.

Madai hayo ambayo thamani yake inafikia Sh6.9 bilioni, yalinaswa kupitia ukaguzi maalumu uliofanyika kwa wanachama zaidi ya 4,000 waliowasilisha maombi ya fao la kukosa ajira kati ya Julai hadi Novemba mwaka jana.

Shirika hilo limeeleza kuwa tayari limeshawalipa wanachama 18,100 wenye sifa za kustaafu na kundi lingine la wanachama 11,411 kati ya 16,100 wa fao la kukosa ajira. NSSF ilianza kushughulikia madai ya wanachama waliokuwa na malimbikizo ya kuanzia 2016 hadi Desemba mwaka jana.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio alisema jana kwamba wanachama waliofanya udanganyifu walishirikiana na maofisa rasilimali watu katika kampuni na mashirika mbalimbali na baada ya kufuatilia kazini kwa walengwa, waligundua kuwa bado wanafanya kazi na wengine wamebadilisha maeneo ya ajira.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, ambaye alitembelea Ofisi za NSSF za mikoa ya Ilala, Kinondoni na Temeke, Erio alisema katika uhakiki huo ndipo walipowabaini wanachama 900 wasiokuwa waaminifu waliokuwa na madai zaidi. Alisema licha ya kuwa na fomu zao walipokwenda kwenye ofisi zao waliwakuta... “Kwetu haya ni madai feki kwa sababu hujaacha kazi.

“Utakuta mwingine anadai hadi Sh72 milioni, hili ni kosa kisheria na mtu anaweza kulipa faini ya Sh10 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja. Kwa hiyo ukaguzi hadi sasa wa kundi hilo la wanachama 4,000 bado unaendelea.”

Katika ziara hiyo, Waziri Mhagama alisema kuanzia Jumatatu kutakuwa na askari kanzu watakaokuwa katika ofisi hizo ili kuwanasa wote wenye madai feki.

Hata hivyo, wanachama waliokuwa wakimsikiliza katika ofisi hizo kwa nyakati tofauti, waliwasilisha kero mbalimbali ikiwamo ya usumbufu katika ufuatiliaji wa madai yao pamoja na malipo madogo ya asilimia 33 kwa waliokuwa na ajira za muda.

Akijibu madao yao, Waziri Mhagama aliagiza hadi kufikia mwezi ujao, wanachama wote wanaodai wawe wameshalipwa stahiki zao na maofisa wa NSSF wawe wanawapangia tarehe za uhakika za kufuatilia madai yao badala ya nenda rudi.

Aliaugiza pia uongozi wa shirika hilo kukamilisha malipo ya wanachama wa fao la kuacha kazi ifikapo Februari.

“Fomu zote zitaachwa hapa (katika ofisi husika), nimeagiza liwepo bango la namba za simu za ofisi ili ikifika tarehe aliyopangiwa apige simu ofisini (NSSF) ili kuondoa usumbufu huo,” alisema waziri Mhagama.