Wanahabari kuweni chachu ya maendeleo

Imepakiwa - Tuesday, May 14  2019 at  11:28

 

Mei 3, wanahabari wa Tanzania waliungana na wenzao duniani kote kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari.

Ijapokuwa siku huyo adhimu kwao imeshapita, bado nawiwa kuandika machache kuhusiana na wanahabari wa Tanzania hasa kutokana na majukumu muhimu waliyo nayo katika kuitengeneza nchi kimaendeleo.

Ninapowatazama wanahabari hawa najielekeza katika kisa kidogo chenye kufikirisha. Hebu msomaji fikiria unamuona tembo akimkanyaga chura anayeugulia maumivu, halafu wewe ukachagua kukaa kimya.

Naaamini chura huyo hatauelewa ukimya wako. Faraja ya chura ni kuona ukitoa kauli ya kumkemea tembo. Kuchagua kukaa kimya ni sawa na kuungana na tembo kumtesa chura.

Maisha ya ububu siyo ya kukumbatia, kushangilia au kupigia debe. Ni jambo ambalo binadamu anatakiwa apingane nalo kwa nguvu kubwa.

Kuchagua kukaa kimya pale unapoona uonevu, unyonywaji, ukandamizwaji, unyanyasaji au madhara yoyote dhidi ya mtu, nchi, jamii, Serikali, chama au taasisi na kuamua kukaa kimya basi wewe ni msaliti wa haki.

Ilivyo ni kuwa ububu kwenye ukiukwaji wa haki, ni laana ambayo hastahili binadamu. Wale wanaoona mambo yakienda ndivyo sivyo na wakachagua kukaa kimya ama kwa woga au masilahi, nao wanachangia kuiyumbisha nchi.

Ujasiri ni mbegu bora ya kupandwa katika nchi na ya kudumishwa, kwani Taifa letu litasonga mbele kama kila mmoja akisimama kwenye nafasi yake kushauri au kukemea pale penye ulazima

Niliwahi kuandika siku za nyuma kuwa vyombo vya habari vinabaki kama sauti ya kukemea na kusema pale wengine wanapoogopa kusema.

Pamoja na dhoruba ya vitisho wanavyokumbana navyo wanahabari duniani, bado wana uthubutu wa kupaza sauti ya onyo, kuuliza, kuhabarisha na kukemea pale jahazi linapoonekana kwenda mrama.

Vikundi au serikali yoyote ya kiimla duniani ina hulka ya kuburuza vyombo vya habari, kumnyang’anya mwandishi kalamu, kuteka na hata kuua waandishi na kufanya lolote kuhakikisha vyombo vya habari vinaandika yale tu wanayotaka kuyasikia. Kwa kufanya hivyo Taifa husika mara nyingi hukosa mwelekeo.

Vyombo vya habari vinayo dhima kubwa katika harakati za maendeleo ya Taifa lolote duniani.

Hawa ni msaada mkubwa katika mapambano ya jamii, kuhabarisha na kuisaidia jamii, ndio wanaomulika na kueleza uhalisia wa mambo kama yalivyo katika uwanja wa mafanikio au changamoto.

Kadhalika, vyombo vya habari vina wajibu wa kuwakumbusha viongozi kuhusu mambo mbalimbali. Siyo kueleza ubora wao tu, vilevile kufichua uovu, kueleza unafiki wao, undumilakuwili na mengineyo. Ni mojawapo ya dhima ya vyombo vya habari duniani kote.

Waandishi ni vioo vya jamii na viongozi kujitazama mazuri au udhaifu wao na kufanya uamuzi. Kupitia kuwaeleza huko, vyombo vya habari vinakuwa mwanga na nuru ya jamii.

Wanahabari kwa kutumia kalamu zao ndio wanaoweza kujenga Taifa lenye watu makini, jamii na viongozi waadilifu, wenye heshima, wawajibikaji, wanyoofu na wanaotenda na kuona haki ikitendeka.

Kwa maana hii lazima shina la uhuru kamili wa vyombo vya habari lipigiwe chapuo na kukemewa likienda ndivyo-sivyo kuliko kuwazongazonga waandishi wanapotekeleza majukumu yao ya kutafuta taarifa, kuhabarisha, kuandika, kuchambua na kuhoji.

Serikali yenye shabaha ya kulisukuma mbele gurudumu la Taifa ni lazima italinda uhuru wa vyombo vya habari.

Hawa siyo wa kutishiwa, kuburuzwa, kunyanyaswa au kutungiwa sheria kandamizi, bali inafaa walindwe, wawezeshwe na waandaliwe mazingira rafiki ya kazi.

Ni kwa mazingira haya naisihi Serikali kuboresha zaidi hali na mazingira ya wanahabari kufanya kazi zao kwa uhuru, huku wakiwajibika kufuata sheria.

Kwa zile sheria zinazolalamikiwa kuwaminya wanahabari, ni wakati sasa wa kuondokana nazo.

Hawa ni watu muhimu siyo kwa Serikali tu, lakini kwa jamii pana ya Kitanzania. Tuwape nafasi wafanye kazi ipasavyo matokeo yake yataonekana.

Hata hivyo, niwaombe pia wanahabari kufuata weledi na taaluma ya uandishi, na siyo kutoa habari kwa lengo la kuchochea, kupendelea au kutaka kutangaza na kuandika habari ili iuzwe kama bidhaa nyingine sokoni.

Noel Shao ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Anaptikana kwa baruapepe; calvin.noelshao@gmail.com au simu namba; 0769-735826