Wananchi wa Mbeya mnataka nini?

Imepakiwa - Tuesday, March 26  2019 at  09:41

 

Machi 22, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), lilitangaza kwamba maadhimisho ya Sherehe za Wafanyakazi Duniani maarufu kwa jina la Mei Mosi zitafanyika jijini Mbeya.

Taarifa ya katibu mkuu wa Tucta, Dk Yahya Msigwa iliyosambazwa katika mitandao ilisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli na kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tanzania ya uchumi wa kati inawezekana, wakati wa mishahara na masilahi bora kwa wafanyakazi ni sasa.”

Akifafanua kwa njia ya simu, Msigwa alisema anaamini Mei Mosi mwaka huu pia itakuwa na ‘mafuriko’ ya watu wakiwamo viongozi mbalimbali wa Serikali kutokana na ukweli kwamba Rais Magufuli anawashirikisha viongozi wote katika maadhimisho makubwa kama haya.

“Mbali ya viongozi wa kitaifa, kwa kawaida wanakuwepo wakuu wa mikoa ya karibu na Mbeya, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali, wakuu wa mifuko ya hifadhi ya jamii na upo uwezekano uwanja ukapokea kati ya watu 40,000 hadi 60,000,” anaema Msigwa.

Anasema kuanzia Aprili 14 Jiji la Mbeya litapokea wafanyakazi karibu 2,000 watakaoshiriki michezo ya aina mbalimbali na washindi watakabidhiwa zawadi wakati wa kilele cha Mei Mosi.

Naye katibu tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja anasema uamuzi wa Tucta kufanyia Mei Mosi mkoani humo umepokewa kwa furaha na kwamba tayari wameshaunda kamati za maandalizi kufanikisha ya maadhimisho hayo.

 

Uchambuzi

Na Lauden Mwambona

Mtunguja anasema mkoa huo ulipata taarifa rasmi ya Tucta kufanya maadhimisho ya Mei Mosi ikiambatana na barua ya mgeni rasmi wa siku hiyo.

Kwa jumla hiyo ni fursa kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Mbeya hususan Jiji la Mbeya. Ni fursa ya pekee na ya aina yake ambayo wananchi wanatakiwa kujipanga vizuri ili walau biashara ya utalii, nyumba za kulala wageni, vyakula na vinywaji ifanyike kwa faida.

Kama ilivyoelezwa hapo juu ni kwamba wageni karibu 2,000 wanaanza kuwasili Aprili 14 ambao watakaa siku zisizopungua 16 wakipata vyakula, vinywaji na hata mavazi.

Hali kadhalika zipo taarifa kwamba kanisa moja litakuwa na wageni wengi mwishoni mwa Aprili watakaofika Mbeya kumsimika kiongozi wao mkuu.

Hivyo, kinachotakiwa sasa ni kwa wafanyabiashara wa Mbeya kujipanga kwa usafi na huduma bora kwa ajili ya wageni hao.

Wafanyabiashara wote wakiwamo wa maduka ya nguo, viatu, hoteli, usafirishaji abiria, wauzaji matunda, mchele, maharage, nyama na vinywaji vya aina mbalimbali ni lazima wajiandae kufanya biashara kwa ukarimu na ubora wa hali ya juu na si kuongeza bei kiholela.

Wageni kutoka mikoa yote nchini ikiwamo ya Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Kagera, Kigoma na Mwanza au Mara wapokewe kwa upendo na kuelezwa maeneo ya utalii kwamba yapo mengi kama vile Ziwa Ngozi, Mlima Rungwe na maporomoko ya Mto Suma yenye urefu wa mita 100 katika kijiji cha Malamba.

Wananchi wa Mbeya lazima wawe tayari kutangaza vivutio vilivyopo Chunya kwamba kuna machimbo ya dhahabu, Wilaya ya Mbarali ni ya kilimo cha mpunga, Kyela ni kilimo cha mpunga na kakao wakati Wilaya ya Rungwe ni chai, ndizi kwa wingi na wilayani Mbeya kuna kilimo cha viazi mviringo na pareto.

Bila shaka wageni kutoka Zanzibar watapenda kuyaona masoko ya Mbeya hususan la Mwanjelwa kwa lengo la kununua mchele. Hiyo ni fursa ya pekee.

Hali kadhalika ujio wa viongozi wakuu wa nchi wakiongozwa na Rais Magufuli ni ufunguo wa kupata majibu ya baadhi ya changamoto ambazo hazijatolewa majibu.

Baadhi ya changamto hizo ni pamoja na kujua lini ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Uyole hadi Mbalizi utaanza kama alivyoahidi wakati wa kampeni zake 2015.

Vilevile, je ni lini mpango wa kuleta maji jijini Mbeya kutoka Rungwe utatekelezwa na pia kujua mradi wa kujenga barabara ya lami kuanzia Tukuyu -Mwakaleli, Lwangwa, Mbambo hadi Tukuyu utakamilika.

Sina shaka, wakazi wa Mbeya hawatajaribu kutumia fursa ya ujio wa viongozi na wageni hao kufanya mambo ya kihuni badala yake watafikiria utajirisho zaidi. Jamani wakazi wa Mbeya Mungu awape nini?

Mwandishi ni mdau wa maendeleo mkoani Mbeya - 0767-338897