http://www.swahilihub.com/image/view/-/4803300/medRes/2138805/-/12342yj/-/dct.jpg

 

Wanaume acheni woga, njooni mpime tezi dume

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa hospitali ya moyo ya Heameda iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam, Dk Hery Mwandolela  

Na Herieth Makwetta

Imepakiwa - Friday, October 12  2018 at  16:23

Kwa Muhtasari

Njia wanazotumia kugundua tezi dume ni za kisasa na si ya vidole ambayo inaogopwa na wanaume wengi

 

Dar es Salaam. Wanaume wametakiwa kwa mara nyingine kutoogopa kupima ugonjwa wa tezi dume kwani vipimo vya kisasa vinazidi kugunduliwa ikiwamo kipimo cha damu na Utra Sound.

Akizungumza jana wakati akitambulisha kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) itakayofanyika Oktoba 18 hadi 19 katika hospitali mpya ya moyo ya Heameda iliyopo Bunju jijini Dar es Salaam, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa hospitali hiyo, Dk Hery Mwandolela alisema njia wanazotumia kugundua tezi dume ni za kisasa na si ya vidole ambayo inaogopwa na wanaume wengi.

“Nawasihi wasiogope teknolojia imekuwa, sasa tuna kipimo cha damu (PSA) na Ultra Sound ambavyo tunavitumia kufanya uchunguzi,” alisema.

Alisema wataalamu huchukua kifaa hicho na kukiweka tumboni mwa mhusika na chenyewe huweza kuonyesha iwapo tezi dume imeathirika au la!

“Wanaume wasiogope, kipimo hiki ni salama kabisa na hakuna upimaji wa kuwaaibisha, tutachunguza pia saratani ya matiti kwa wanawake,” alisema.

Dk. Mwandolela alisema huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni kupima uzito, urefu, sukari, wingi wa damu, shinikizo la damu, tezi dume, macho, saratani ya kizazi na matiti bila malipo.

Alisema wameshafanya kambi tatu kama hizo, ambapo wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), asilimia 11.2 walikutwa na magonjwa ya moyo hasa shinikizo la juu la damu, asilimia tisa kisukari na asilimia tisa saratani ya tezi dume.