Wanawake wanaweza, wasisubiri kwezeshwa

Baadhi ya wanawake wakiadhimisha sherehe ya siku ya wanawake Duniani 

Imepakiwa - Friday, March 8  2019 at  08:39

 

 Leo ni siku ya Wanawake duniani. Ni siku ambayo wanawake nchini wanaungana na wenzao duniani kuadhimisha siku hii iliyoanza kuadhimishwa rasmi mwaka 1975.

Historia ya siku hii ilianza karne ya 20 nchini Marekani, kabla ya wazo hilo kupokwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hivyo kuadhimishwa na nchi wanachama wa umoja huo.

Siku ya Wanawake Duniani ni fursa muhimu inayowakutanisha wanawake na wadau wengine kutafakari na kuweka mikakati ya masuala yanaowahusu kama sehemu muhimu ya jamii.

Ni siku ambayo moja ya malengo yake ni kuhanikiza kuwepo kwa fursa sawa kwa watu wa makundi yote katika jamii. Pia siku hii inalenga kuhamasisha kuongeza ushiriki wa wanawake kama washirika sawa na watu wengine katika shughuli za maendeleo ya jamii na mataifa kwa jumla.

Ndiyo maana kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”.

Ni kaulimbiu yenye ujumbe mzito kuwa maendeleo hayana mipaka ya kijinsia na kwamba ushiriki wa wote ndio chanzo cha nchi mojamoja na hata dunia kwa jumla kufikia maendeleo endelevu.

Leo kama Taifa, Tanzania inajivunia kwa kiwango fulani kutekeleza ujumbe uliomo katika kaulimbiu hii. Mathalan, ushiriki wa wanawake katika baadhi ya nyanja muhimu kama vile siasa na uchumi unaonyesha ahueni tofauti na hali ilivyokuwa miaka iliyopita.

Japo hatujafanikiwa sana, angalau tumefika hapo kwa sababu kilio cha kuwawezesha wanawake kimekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Wanawake wenyewe hawajawa nyuma kupaza sauti ya kutaka kupewa nafasi. Wamekuwa wakitumia majukwaa mengi kuonyesha hisia zao, kama maadhimisho ya siku hii ambayo huwakutanisha kinamama wa kada mbalimbali nchini.

Hata hivyo, tunapopaza sauti kama Taifa na hata kwa ngazi ya kimataifa kuhusu usawa wa kijinsia, wanawake hawapaswi kubweteka wakisubiri huruma ya mipango na mikakati kutoka serikalini au kwa wadau wa maendeleo.

Tunadhani ni wakati mwafaka sasa wanawake wakaondokana na mawazo ya kusubiri kuwezeshwa kama suluhu pekee ya masaibu wanayokumbana nayo.

Tunachokijua na kukiamini ni kuwa wanawake wanaweza. Wakijiamini na kuonyesha uwezo walionao, ni rahisi kwao kufika mbali hata pasipokuwa na msukumo wowote mkubwa kutoka nje. Hili linadhihirishwa na mafanikio ya baadhi yao waliothubutu kuonyesha jitihada katika baadhi ya nyanja kama siasa.

Tunapowatakia wanawake heri na fanaka katika maadhimisho ya siku hii, ni muhimu tukasisitiza kuwa hiyo ni fursa adhimu kwa wanawake na jamii kwa jumla kujadiliana namna bora ya kukabiliana na changamoto na vikwazo mbalimbali wanavyokabiliana navyo katika kufikia ustawi wao na maendeleo ya Taifa kwa jumla.

Kwa umaalumu wa kipekee kama nchi, maadhimisho haya pamoja na mengineyo yatumike kama kilinge cha kutathmini hatua tulizofikia katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake katika nyanja zote za kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kisiasa.