http://www.swahilihub.com/image/view/-/4706548/medRes/2059714/-/sc25nkz/-/ummy.jpg

 

Watakaoongoza kidato cha pili kupewa tuzo ya ‘Ummy Mwalimu’

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu  

Na Burhani Yakub

Imepakiwa - Friday, August 10  2018 at  12:26

Kwa Muhtasari

Lengo ni kuamsha ari ya masomo kwa wanafunzi

 

Tanga: Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameanzisha tuzo ya ‘Ummy Mwalimu’ itakayotolewa kwa mwanafunzi atakayeongoza katika mitihani ya kuwapima uwezo wanafunzi wa kidato cha pili kwenye shule zilizopo Kata za Jiji la Tanga.

Ummy alitangaza tuzo hiyo jana alipokuwa akikabidhi madawati 40 yenye thamani ya Sh5.5 milioni kwa Shule ya Sekondari Chumbageni jijini hapa yaliyotolewa na asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha kuwajengea uwezo wasichana Mkoa wa Tanga (Tawode) kwa ufadhili wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Alisema tuzo hizo zitatolewa kwa mwanafunzi atakayeongoza masomo yote katika mashindano hayo ya mitihani na itahusisha wasichana peke yao.

Alisema tuzo nyingine itatolewa kwa mwalimu wa mwanafunzi atayaeongoza mitihani hiyo.

Ummy alisema lengo la mashindano hayo ni kuamsha ari ya masomo kwa wanafunzi wa Tanga.

Aliwataka wanafunzi kuwa na ndoto za kufanya mambo makubwa katika maisha yao badala ya kukata tamaa huku akitolea mfano wa historia yake katika masomo kwamba kama asingefanya jitihada asingefikia nafasi ya Waziri.

Mkurugenzi wa Tawode, Fatma Mganga alisema asasi hiyo imepata madawati hayo baada ya kuomba msaada NSSF.

Mkuu wa shule hiyo, Kavumo Mziray alisema wanakabiliwa na uhaba wa viti 163 na meza 60.