http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801172/medRes/2137448/-/msh99l/-/ummy.jpg

 

Waziri wa Afya afichua siri ya madaktari

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu  

Na Bakari Kiango

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  12:42

Kwa Muhtasari

Baadhi wanaficha taarifa za ukatili wa kijinsia kwa watoto kukwepa kutoa ushahidi mahakamani


 

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kuna madaktari wanaoficha taarifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto na kuonya hatasita kuwafutia usajili wao.

Mwalimu alitoa kauli hiyo juzi wakati akifungua mjadala wa kitaifa wa siku tatu kuhusu changamoto za mimba, ndoa za utotoni na ukeketaji ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA).

UNFPA imeshirikiana na wizara hiyo na wadau mbalimbali kikiwamo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani leo.

“Kuna tatizo moja nimelipata, kuna mtoto amekutwa amebakwa na aliyembaka akakiri lakini alipofanyiwa vipimo daktari akasema hakuna ubakaji wala ulawiti.”

“Nilipojaribu kufuatilia nimebaini madaktari hawa hawapendi kutoa ushahidi pindi wanapohitajika, yaani ile nenda na rudi ya mara kwa mara,” alisema.

Mwalimu aliwataka madaktari wote kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa mujibu wa viapo na kuonya hatasita kuwachukuliwa hatua watakaobanika.

“Takwimu za vitendo hivyo haziridhishi na ukweli ni mchungu lazima usemwe ili kukabiliana navyo,” alisema.

Mbali na hilo, Mwalimu ameziagiza hospitali zote za mikoa nchini kuweka dawati la jinsia kwa ajili ya kuwasaidia waathirika mbalimbali wa matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto na kupewa huduma bure bila kutozwa fedha.

Mwalikishi Mkazi wa UNFPA nchini, Jacqueline Mahon alisema mjadala huo utatoa nafasi kwa Serikali na wadau mbalimbali kujitafakari namna ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

Akizungumza katika mjadala huo, Chifu wa kabila la Wagogo, Lazaro Masuma ameiomba Serikali kukomesha vitendo vya baadhi ya wazazi kupokea mahari za watoto wao wakiwa bado wanafunzi.

“Mipango hii inafanyika kwenye vilabu vya pombe na mahari zinazotolewa ni mifugo hasa ngo’mbe. Mtoto anasoma lakini tayari ameshawekewa oda, ikitokea amemaliza na kufaulu mzazi anamwambia haina haja ya kuendelea na shule kwa sababu nimeshapokea mahari yako,” alisema.