http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885242/medRes/2191300/-/11e3iqsz/-/saa.jpg

 

Weka malengo yakusaidie kazini

Saa inayotumika kupanga muda maalumu wa kufanya jambo fulani kulingana na malengo ya siku 

Na Christian Bwaya

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  10:18

Kwa Muhtasari

Pangilia vipaumbele kulingana na uzito wa majukumu

 

Mafanikio katika eneo lako la kazi, kwa kiasi kikubwa yanategemea matumizi ya muda ulionao kwa siku.

Kile unachokifanya kati ya saa 6:00 usiku na saa 5:59 usiku wa siku inayofuata, ndicho kinachoamua utekelezaji wa majukumu yako.

Sote bila kujali aina ya kazi tunazofanya wala mahali tunapoishi tumepewa mtaji wa saa 24 kwa siku. Tofauti, hata hivyo, ni namna tunavyoweza kutumia saa hizo kwa tija.

Makala haya yanakupa uzoefu wa watu ninaowajua wana shughuli nyingi lakini wameweza kujijengea tabia ya nidhamu ya muda. Kwa ujumla, wanatufundisha tabia tano muhimu.

Mhandisi Sylvanus Kamugisha, Mkurugenzi wa Kampuni ya Sylcon Builders Limited anasema mahali pa kuanzia ni malengo ya mwaka uliyonayo:

“Vipaumbele vinatokana na malengo ya mwaka niliyonayo. Mfano, mwaka huu nimeazimia kuwa mtu wa sala. Kupunguza uzito kilo 20, kusoma vitabu 40 na mambo kama hayo.”

“Kwa hiyo kwenye ratiba yangu ya siku pamoja na mambo mengine inaanza na dakika 15 za sala, baadae naenda kufanya mazoezi dakika 30 mpaka 45, baada ya hapo nasoma kurasa 10 mpaka 15 za kitabu kilicho kwenye ratiba yangu na ratiba nyingine inaendelea.”

Aidha, namna unavyotafsiri malengo yako katika siku inayofuata ni muhimu kama anavyoeleza Prosper Mwakitalima, Mkurugenzi wa Ubunifu wa Brand Exponential:

“Nina utaratibu wa kupangilia siku yangu, siku moja kabla. Kisha ninaandaa mambo ya kutekeleza kesho kabla sijalala. Hii inanipa muda wa kuiona kesho kabla sijalala.”

Erick Mbogoro, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma naye anakubaliana naye kwa kusema:

“Huwa naandaa abstract schedule (ratiba) yangu kabla ya kuanza siku. Kwa hiyo nafanya kazi kulingana na muda niliojipangia.”

Dk Mwemezi Rwiza, mhadhiri katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) jijini Arusha hupangilia vipaumbele kwa kuangalia uzito wa majukumu.