http://www.swahilihub.com/image/view/-/3337766/medRes/1197154/-/sc217hz/-/DNAlcohol1207i.jpg

 

William Kabogo: Fundi wa stima na mwanasiasa

William Kabogo

Aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo ahutubia wafuasi awali. Picha/PAUL WAWERU  

Na MWANGI MUIRURI na KABRASHA LA HISTORIA

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  14:02

Kwa Muhtasari

William Gitau Kabogo ni mwanasiasa tajika katika eneo la Mlima Kenya na uwezo wake kamili hujidhihirisha katika ukwasi mkuu, ufasaha wa maneno na ujasiri wa kufanya maamuzi.

 

WILLIAM Gitau Kabogo ni mwanasiasa tajika katika eneo la Mlima Kenya na uwezo wake kamili hujidhihirisha katika ukwasi mkuu, ufasaha wa maneno na ujasiri wa kufanya maamuzi.

Hata hivyo, sifa hizo zote hazikumwezesha kujinasua kutoka kwa mtego wa Ferdinand Waititu ambaye alimtimua kwa kura kutoka ugavana wa Kiambu katika uchaguzi wa Agosti 8, 2017.

Mbinu iliyotumiwa na wapinzani wake ilikuwa sawa na ngome ya mchezo wa raga ambapo upinzani hujumuika kama siafu kwa mshambulizi.

Huku akikambwa kisawasawa kupitia muungano wa karibu wanasiasa wote waliokuwa wakiwania nyadhifa zingine Kiambu, mrengo mwingine wa propaganda ulizinduliwa na ukafanikiwa kumwangazia Kabogo kama mtundu wa kimaongezi na aliyekuwa na dharau tosha kwa masikini na aliyekuwa na maringo kutokana na ukwasi wake.

Kwa hayo yote, Kabogo anasemwa kuwa alifanya makosa makuu ya kufikiria kuwa wapiga kura wangeazingatia utendakazi wake wa awamu ya kwanza na ambao husifiwa kuwa ulileta manufaa halisi.

Wakati wa kiama ulipofika, Kabogo nje, Waititu ndani, ingawa leo hii kuna manung’uniko Kiambu kutoka kwa baadhi ya wapiga kura ambao waziwazi wanasema “afadhali Kabogo”.

Ni mwanasiasa ambaye akiamua kusema yaliyo moyoni mwake hasiti kuyatoa, lakini akijipata taabani anakimbia kurekebisha hali.

Amenukuliwa akisema kuwa wale wanawake ambao hawajaoelwa hawafai kuchaguliwa kuongoza umma, akisema kuwa hajali kushtakiwa kwa kuwa ako na mihela ya kununua uhuru wake, akanaswa akitisha raila Odinga na wafuasi wake na ambapo alishtakiwa kwa uchochezi lakini akaachiliwa huru.

Aliwahi kulaumiwa kwamba alitoa kauli ya akina mama wengine ni maskini kiasi cha kukosa pesa za kununua chupi. Ni madai ambayo alikanusha.

Kigogo

Alizaliwa Aprili 4, 1961, na hutazamiwa kuwa mmoja wa kiungo thabiti cha siasa za jamii za Mlima Kenya ingawa huwa na mazoea ya kujikwaa kiholela katika hali ambazo angeibuka mshindi kwa urahisi.

Kwa mfano, wengi hutilia shaka uaminifu wake kwa siasa za unyumba kwa kuwa amekuwa akitangaza hadharani kuwa “sio lazima William Ruto arithi urais 2022”  bali ikiwa itafanyika hivyo ni lazima kuwe na majadiliano ya ni vipi atatuza Mlima Kenya ukimuunga mkono.
 Hivi majuzi ameonekana akikutana na kinara wa ODM, Raila Odinga wakishauriana mawili matatu ya kisiasa, mpangilio ambao kwa kawaida uliibua hisia za shaka kichinichini ikizingatiwa kuwa eneo hilo humhusisha Odinga na upinzani wao wa moja kwa moja kisiasa.
 Mwaka wa 2007 alimenyana kisawasawa na aliyekuwa waziri wa usalama wa ndani, John Njoroge Michuki aliyekuwa amemworodhesha Kabogo kama mmoja wa wafadhili wa makundi haramu.
 Pia, amejipata katika orodha mbaya ya Marekani kuhusu hili na lile mitaani ambapo vijana wa kuhangaishwa na maisha hujipa utulivu wa kujiharibu, lakini akajitetea kwa dhati.
 Akiwa mbunge wa Juja kabla ya kuwa gavana, alikuwa mmoja wa wanasiasa bungeni ambao walifahamika kuwa na maswali hatari kwa mawaziri akitaka kujua ukweli ulio uchi.
 Katika jukwaa la kisiasa akisuta umasikini wa wapinzani wake, alikuwa akisema kuwa mamake mzazi akimtarajia nyumbani kumtembelea, alikuwa akiangalia angani wala sio kwa lango barabarani kwa kuwa ni mumiliki wa helikopta.
 Sio mara moja alinaswa akisema kuwa “yote mazuri hutoka mbinguni, mazuri kama mvua na pia Baraka za Mungu na ambapo mimi hujitokeza kutoka juu kwa ndege hivyo basi kuwa kielelezo cha baraka pia.”
 Mwaka wa 2013 alisema kuwa angemenyana na rais Uhuru Kenyatta katika kuwania usemaji wa kijamii Mlima Kenya akisema kuwa “hata mimi naweza kuwa kigogo wa kisiasa.”

Fundi wa stima

Alisomea shule ya msingi ya St George na kisha akajiunga na ile ya Thika Technical High School na akahitimu kama fundi wa stima.

Aliishia kujiunga na chuo kikuu cha Panjab nchini India kusaka taaluma ya kibiashara na mwaka wa 1982 akahitimu.

Amefanya kazi kama mhasibu katika afisi ya mkaguzi wa fedha za umma  na pia katika mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali.

Alihamia jijini Mombasa miaka ya 1980s na ndipo alianza kujulikana kwa ukwasi kiasi kwamba ameorodheshwa kama mmiliki wa kwanza kabisa nchini Kenya kumiliki gari aina ya Hummer.

Amejiorodhesha kama aliyepata ukwasi wake kupitia biashara katika sekta kadhaa, wengine wakisema yao, naye akisema akisema yake kuhusu biashara hizo.
Mwaka wa 2002, akajiunga na siasa na akashinda ubunge Juja, 2007 akashindwa na George Thuo lakini kabogo akakimbia mahakamani kupinga, ushindi huo ukabatilishwa na mwingine mdogo ukaamrishwa utekelezwe na Kabogo akatwaa ushindi tena.

Mwaka wa 2013 akachaguliwa kuwa gavana na sasa ndiye huyo nje ya siasa, akiwa ni mume kwa Philomena Kabogo na ambapo wako na watoto wawili wa ambao ni Andrew Kabogo na Alvin Kabogo.