http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885154/medRes/2191247/-/b395e7z/-/zabiza.jpg

 

Zabibu: Banda mahaba kama yote

Zabibu

Abdi Banda akiwa na mke wake, Zabibu. Picha/HISANI 

Na CHARITY JAMES

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  09:59

Kwa Muhtasari

Zabibu ametokea familia ya wanamuziki.

 

ZABIBU Kiba ni mke halali wa Abdi Banda, beki tegemeo wa timu ya Taifa, Taifa Stars na klabu ya Baroka FC ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Zabibu ambaye alifunga ndoa ya aina yake na Banda Agosti 1, mwaka huu, mbali na kusimulia mahaba mazito anayopewa na mumewe, Banda, pia amefichua siri nzito za mume wake ambazo hata yeye mwenyewe hajawahi kuzijua.

Anasema, mumewe huyo pia ana wivu kwa mbali, jambo ambalo linaongezea mahaba katika ndoa yake.

Mwanaspoti lilifunga safari mpaka Tanga, mtaa wa Foes anapokaa mama mzazi wa mwanasoka huyo na bahati nzuri likamkuta Zabibu ambaye alienda kumtembelea mama mkwe wake ndipo likaamua kufanya naye mahojiano ya kina.

 

Mahaba mazito

Uwanjani, Banda hashikiki, wapinzani wanamjua anavyowadhibiti na hiyo ndio maana ameweza kuitumikia pia timu ya Taifa na kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini. Hata hivyo, sio uwanjani tu, Banda ni fundi hadi kwa mke wake. Anajua kupenda na hilo, linamfanya ajihisiyuko paradiso.

Zabibu anafichua jinsi Banda anavyompa mahaba mazito wanapokuwa pamoja na anafurahia jinsi anavyomjali na kumpa mahitaji yote kama mke.

“Banda ni mtu wa utani sana, nikiwa naye muda mwingi anautumia katika matani na kunisaidia kufanya usafi, kupika na amekuwa akiniona mrembo niliyestahili kuwa nae.”

 

Vipi kuhusu wivu?

Mapenzi hayaendi bila wivu, hata Banda ana wivu na hilo Zabibu anasema ni moja ya mambo yanayoimarisha ndoa yao.

“Mume wangu ana wivu sana na mimi, yote hii ni kwa sababu tunapendana muda mwingi. Akiwa kambini simu zake hazikatiki muda wote, anapenda tuwasiliane ili ajue nipo salama kiasi gani. Kwa mfano, sasa nipo huku nyumbani kwao, simu sio nyingi sana kwa sababu anajua nipo na mama mkwe wangu. Hapo anakuwa hana wasiwasi. Lakini nikiwa kwa mama yangu mzazi, simu zinakuwa nyingi zaidi kwa sababu anajua kule ndiko nilikozaliwa na nafahamiana na watu wengi,” alisema Zabibu.

 

Anamwamini sana mumewe

Pamoja na wivu, lakini Banda hupenda kulinda ndoa yake, hata hivyo, Zabibu yeye hana tatizo na mumewe kutokana na changamoto anazopitia.

Kikubwa anachojua, mumewe kazi yake ni moja ya kazi zinazompa mtu umaarufu na umaarufu hauendi bila ya changamoto za kusumbuliwa.

Anasema kuhusu kushika simu ya mumewe, huwa anashika sana kwa ajili ya mawasiliano, lakini sio kuikagua kwa sababu anaogopa kuumia kwa atakachokutana nacho.

“Mimi simu yangu huwa namwachia akague atakavyo, lakini ya kwake, naogopa kufanya hivyo kwa sababu ni mtu ambaye anawasiliana na watu wa kila aina kutokana na kazi yake.”

“Namwamini mume wangu, najua hawezi kunisaliti japo anakutana na changamoto nyingi za kusumbuliwa na wanawake kutokana na umaarufu wake, anatumiwa sana meseji na kupigiwa simu,” alisema.

 

Sio Muongeaji

Katika kitu ambacho watu hawakifahamu na wanamchukulia tofauti ni kumwona Banda mkorofi. Hata hivyo, mkewe ameweka wazi Banda ni mpole asiyependa kuongea, huku muda mwingi akiutumia kuangalia TV.

“Banda ni mtaratibu na mtu asiyependa maneno maneno, yeye kwake ni vitendo tu, akiongea sana basi utani na kufanya mambo mengine, lakini mimi naona anachukuliwa tofauti na watu na utani ukizidi huwa ananiwekea ‘headphones’ sikioni.”

“Wamekuwa wakimvisha ngozi si ya kwake kwa kumwona ni mkorofi, lakini tangu nimeingia katika uhusiano naye, nimejifunza mengi kutoka kwake na nimemwona ni mtu wa tofauti sana na anavyochukuliwa na watu.”

 

Anapenda kula, jikoni yuko vizuri

Kutokana na kazi anayoifanya Banda ya soka, mara nyingi anapenda awe fiti na hii inamfanya apende kula kila wakati. Mazoezi anayoyafanya akiwa na kikosi cha Baroka na nafasi anayocheza uwanjani, ni wazi msosi ni muhimu na Zabibu anasema,

“Mume wangu anapenda kula muda wote, anapenda kutafuna na ndio maana anahakikisha friji linajaa matunda, vinywaji, Chocolate na vitu vidogo vidogo ambavyo sio vya kupika ambavyo ni vya kula moja kwa moja.”

“Kikubwa ninachoshukuru si mvivu wa kuingia jikoni kupika, akiona mkewe niko bize na mambo mengine ananisaidia majukumu ya jikoni.”

Anasema Banda pamoja na kupenda kula lakini sio mlaji sana, anapenda kudokoa kidogo na kuacha, hawezi kukaa mezani na akamaliza chakula kwa wakati, huwa anachukua kidogo anakula na kuacha.

 

Hapendi kufua

Barabarani au sehemu yoyote, huwezi kumwona Banda mchafu, anapenda usafi lakini kama kuna siri ambayo huijui, Zabibu anaiweka wazi.

“Pamoja na kupenda kunisaidia majukumu ya nyumbani, mume wangu ukitaka kumfukuza nyumbani, umwambie ni muda wa kufua, anakukimbia bila kufahamu amekwenda wapi.

“Katika vitu ambavyo Banda hapendi kuvifanya basi ni kufua, huwa anachukia sana hicho kitendo lakini huwezi ukamkuta amevaa nguo chafu hata siku moja. Hata kipindi akiwa mwenyewe anaona bora apeleke nguo kwa dobi zikafuliwe kuliko afue yeye.”

“Nimeshalijua hilo, hivyo halinipi tabu. Muda mwingine akishajua kabisa leo ni siku ya kufua, utamwona anahangaika na jiko ili tu anifurahishe na nikimaliza kufua, nitakutana na chakula, hapo ndipo ninapompendea mume wangu,” anasema Zabibu.

 

Kizizi cha banda

Mwanamke ni faraja ndani ya ndoa. Mwanamume anapokuwa katika majukumu ya kila siku, mwanamke hutakiwa kumpa hamasa na sapoti kubwa ili mumewe aweze kufanikiwa. Hilo ndio jukumu la Zabibu pale mumewe anapokuwa na majukumu uwanjani, kabla na baada ya mechi anahakikisha anamwandaa kisaikolojia.

“Klabla na baada ya mechi ni lazima tuwasiliane. Nisipopiga mimi, basi atapiga yeye, kikubwa tunachozungumza ni kuomba dua ili aweze kuanza salama na kumaliza salama,” anasema.

“Mume wangu anaipenda sana kazi yake na mimi naipenda pia kwa sababu inaendesha maisha yetu, hivyo tumekuwa tukimshirikisha mungu katika hilo ili aweze kumsimamia muda wote awapo kazini,” anasema.

 

Upinzani Man United, Liverpool

Licha ya Zabibu kutokea katika familia yenye wasanii wa muziki, Ali Kiba na mdogo wake Abdu Kiba, hata hivyo kwenye suala la michezo hasa soka pia wapo.

Nani asiyejua Ali Kiba amesajiliwa na Coastal Union ya jijini Tanga licha ya kutokucheza mechi hata moja za Ligi Kuu hadi sasa?

Zabibu naye ni shabiki mkubwa wa soka na anaipenda Manchester United ya Ligi Kuu Uingereza, huku Banda mbali na kucheza soka, pia ni shabiki wa kulialia wa Liverpool ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sasa bana, kama unavyojua timu hizi za England ni wapinzani wa jadi, kwa Zabibu na Banda napo kuna upinzani hasa pale timu moja inapofungwa na utani huchukua nafasi yake.

Anacheka, “Kwa upande wa mpira wa nje kila mmoja ana timu yake na hapa ndio utani unapozidi kwani kila mmoja ana timu yake tofauti na Baroka ambako ndiko kunapotuingizia pesa.

Licha ya kumuoa mdogo wa King Kiba, ambaye ni hasimu mkubwa wa Diamond Platnumz unafahamu Banda ni shabiki wa msanii gani hapa Bongo na anafanya nini anapokuwa nyumbani? Fuatilia kesho Jumamosi ambapo, Zabibu atafichua mazito zaidi na ishu nzima ya mama mkwe wake.