http://www.swahilihub.com/image/view/-/4884020/medRes/2190657/-/efphlcz/-/kasim.jpg

 

Ziara za kushtukiza zilivyosababisha Bandari kufumuliwa

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa Bandari ya Dar es Salaam alipofanya ziara ya kushtukiza mwaka jana. Picha na maktaba   

Na Elias Msuya, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  14:32

Kwa Muhtasari

Tatizo ni ucheleweshaji wa mizigo na utendaji mbovu

 

emsuya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ziara za Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Bandari ya Dar es Salaam zinatajwa kuwa chanzo cha Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuwatosa vigogo wake na kutangaza nafasi 68 za kazi.

Juzi, mkurugenzi mkuu wa TPA, Deusdedit Kakonko aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa kutangazwa kwa nafasi hizo za kazi ni mkakati wa Serikali kupitia upya sifa za watumishi wake, “Ili kuhakikisha inapata watumishi wenye sifa, hilo ni jambo la kawaida.”

Bandari ya Dar es Salaam ndiyo kubwa kuliko zote nchini ikipitisha zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayoingia na kutoka nchini.

Bandari hiyo pia inategemewa na nchi zisizo na bahari ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Habari za ndani zinasema kuwa ziara za mara kwa mara za wakuu hao wa nchi na kutotimizwa kwa baadhi ya maagizo yao kunaweza kuwa chanzo cha kufumuliwa kwa mamlaka ya bandari nchini.

Ziara za kushtukiza

Tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani Novemba 5, 2015, Bandari limekuwa eneo linaloonekana kuwa na utata mwingi huku kiongozi huyo pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa wakifanya ziara za kushtukiza za mara kwa mara huku wakitoa maagizo mazito.

Mapema Novemba 27, kabla hata Rais Magufuli hajatangaza Baraza la Mawaziri, Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza bandarini na kuamuru kukamatwa kwa maofisa kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na wengine kufukuzwa kazi.

Kama hiyo haitoshi, Februari 11, 2016 Waziri Mkuu Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza bandarini hapo na aliibukia kitengo cha mita za kupimia mafuta (flow meters) eneo la Kurasini.

Rais Magufuli alianza kutembelea Bandari ya Dar es Salaam Septemba 26, 2016 kwa kuzungumza na wafanyakazi wa bandari hiyo.

Pamoja na mambo mengine alitoa miezi miwili kwa TPA kununua mashine nne za kukagulia mizigo na pia akatembelea eneo la mita za kupima mafuta.

Machi 23, 2017, Rais Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza bandarini hapo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo ikiwemo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.

Novemba 26, 2017, Rais Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza bandarini na kubaini uwepo wa magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 yaliyokwama tangu Juni 29, 2015 yakiwamo magari ya jeshi la polisi 53 yaliyokuwa yamekwama tangu Juni 2016.

Rais Magufuli pia alibaini uwapo wa magari yaliyotekelezwa bandari hapo kwa zaidi ya miaka 10. Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli alitoa siku saba kwa TRA, TPA na jeshi la polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama bandarini hapo kwa muda mrefu. .

Wadau wataka mabadiliko

Je, kufanya mabadiliko ni suluhisho la matatizo hayo? Wadau wamekuwa na maoni tofauti.

Rais wa Chama cha Wasafirishaji (TAT), Omary Kiponza amesema utendaji hafifu ndio sababu ya mlundikano mkubwa wa mizigo bandarini hapo.

“Sisi kama wasafirishaji wa mizigo furaha yetu ni kuona mabadiliko yanafanyika ili kuharakisha usafirishaji wa mizigo,” alisema Kiponza.

“Tatizo kubwa pale bandarini ni mlundikano wa mizigo kiasi cha kusababisha meli kuchelewa kushusha mizigo na kuondoka. Ndiyo maana tuliwashauri wawahusishe wenye bandari za nchi kavu ili mizigo ikishashushwa ihamishiwe kwenye bandari hizo ili bandarini kuwe na nafasi,” alisema Kiponza.

Eliachim Kivae wa Kampuni ya Vamwe International Logistic Co. Ltd alisema licha ya kubadilishwa kwa watendaji, itachukua muda mrefu kumaliza tatizo la rushwa na urasimu katika bandari hiyo.

“Mabadiliko ya utendaji hapa bandarini yatachukua muda mrefu kubadilika hata kama watabadilisha hao watendaji. Rais alitusaidia kurudisha polisi bandarini wanaosaidiana na polisi wa bandari, lakini bado hawajamudu kukabiliana na rushwa na urasimu,” alisema Kivae.

“Tatizo ni ucheleweshaji wa mizigo na utendaji mbovu, halafu watendaji wengi siyo waadilifu, rushwa ipo kila kona. Hata wageni wanaokuja kutoka nje bado wanalalamikia huduma zetu, wanasikitishwa na vitendo vya rushwa. Mabadiliko yafanyike tu, lakini bado kuna kazi ngumu ya kubadilisha,” alisema.