http://www.swahilihub.com/image/view/-/4844660/medRes/2165574/-/5rxnjn/-/mbulaa.jpg

 

Mwigizaji wa kujitegemea ambaye licha ya umri wake, amefanikisha mengi tu

Caroline Mbula

Mwigizaji wa kike Caroline Mbula. Picha/JOHN KIMWERE 

Na JOHN KIMWERE 

Imepakiwa - Friday, November 9  2018 at  18:18

Kwa Muhtasari

Mwigizaji Caroline Mbula ni mmojawapo wa wasanii wachache wa kike ambao wameamua kujituma kuvumisha tasnia ya filamu na muvi hapa nchini Kenya.

 

NI kati ya wasanii wachache wa kike ambao wameamua kujituma kuvumisha tasnia ya filamu na muvi hapa nchini Kenya.

Ni taaluma aliyoiwazia tangia akiwa mdogo akisoma kwenye Shule ya Msingi ya Dandora, Nairobi.  

Hakika wahenga hawakupaka mafuta kwenye mgongo wa chupa walivyolonga 'Vitu vya biashara havigombani'.

Katika mpango mzima ni mwigizaji wa kujitegemea ambaye amefaulu kushiriki zaidi ya muvi 50 ambapo baadhi yazo zimefanikiwa kurushwa kupitia vituo tofauti nchini ikiwamo Citizen TV, KTN na Maisha Magic. 

Bila kuongeza chumvi wala ladha yoyote, Caroline Mbula, 28, amevalia kofia nyingi tu katika sekta ya uigizaji.

Alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji akishiriki filamu za mwongozo wa vitabu husika (setbooks) na tayari leo hii ameiva kinoma. 

Ni mwigizaji, msimamizi wa script pia mwongozaji wa muvi au mwelekezi (director). 

''Bila kujisifia hupata dili nyingi ambapo hufanya kazi baada ya kuandikiana mkataba na wahusika,'' anasema na kuongeza kuwa ndani ya miaka kumi pekee amehusika kutengeneza muvi kibao.  

Dada huyu amebahatika kufanya kazi na kampuni kibao kama Phil It TV, Citizen TV, Wide Ange Visions, Protel Studios Limited, Zamaradi Production, Spielworks Media Limited, Onfon Production, Kikwetu Production na Leela Production.  Hayo tisa. Kumi anamiliki brandi yake, Twenty Seven Production anakopania kufikisha tasnia ya muvi katika upeo wa juu miaka michache ijayo. 

''Kwenye sekta hii ninapania kutengeneza muvi za viwango vya juu maana katika malengo yangu ninatamani sana kufanya kazi na waigizaji wa hadhi ya juu kimataifa kama Dwayne Johnson na Dany Garcia,'' anasema.

Wawili hao (Wamarekani) wanamiliki kampuni ya Seven Buck Production. 

Kwenye uigizaji wake hawezi kuweka katika kaburi la sahau muvi ya kwanza kabisa aliyoshiriki mwaka 2010 ya 'Inspekta Mwala'. Anasema ndiyo iliyokuwa muvi ya kwanza kushiriki na kurushwa kwenye runinga hali iliyomtia motisha kuendelea kukinoa kipaji chake.

Baadhi ya muvi ambazo ameshiriki chini ya Spielwork Media ni: 'Pombe Haramu,' 'Urembo'  na 'Unprotected' zote huonyeshwa kupitia Maisha Magic. Zingine:'Bodaboda', 'Tax Driver'  na 'Katendoni'  kati ya zinginezo.

Ubunifu ni muhimu

Mwigizaji huyu anataka wenzie wanaoibukia kuwa wabunifu endapo wanapania kupenya katika sekta hii.

''Waigizaji wapya kwenye gemu wafahamu hakuna mteremko pia lazima wamakinike kama sivyo ni rahisi kuangukia meno ya maprodyuza ambao hupenda kuwashusha hadhi wasanii wa kike,'' anaeleza.

Kadhalika alisema ukuaji wa teknolojia unatoa njia mwafaka kuitumia kusambaza kazi za sanaa yao ili kutambulika na wengi kote.  

Naye pia anasema hupitia changamoto sawa na wenzie.

Anadokeza kuwa licha ya makubaliano kupitia maandishi, maprodyuza wengi huchelewesha malipo ya waigizaji na kuwapa wakati mgumu kimaisha.

Anawataka wamiliki wa vituo vya runinga humu nchini kuzingatia sheria iliyopendekeza kuonyeshwa kwa asimilia sitini ya kazi za burudani za wazalendo.