http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924878/medRes/2217637/-/hn2n0f/-/okesa.jpg

 

Lily Okeyo: Anawafaa wasichana kuhakikisha wanapata elimu

Lily Okeyo

Lily Okeyo, mwanzilishi wa Work Her Dream Organisation (WHDO), shirika lenye makao yake mjini Eldoret na ambalo linasaidia watoto na hasa wasichana kutoka familia maskini kuendelea na masomo. Picha/HISANI 

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  10:56

Kwa Muhtasari

Bi Lily Okeyo, 33, anafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa wasichana wanasalia shuleni.

 

ANAFANYA kila awezalo kuhakikisha kuwa wasichana wanasalia shuleni. Ni shughuli ambayo Bi Lily Okeyo, 33, amekuwa akifanya kwa kusaidia wasichana kupata ufadhili wa kimasomo, kuwanasihi, vilevile kuhakikisha kwamba hawakosi kwenda shuleni wakati wa hedhi kutokana na ukosefu wa visodo.

Ni kazi ambayo amekuwa akiiendeleza kupitia Work Her Dream Organisation (WHDO), shirika aliloanzisha mwaka wa 2016, na ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake katika kaunti tano.

“Makao halisi ya shirika hili ni mjini Eldoret huku shughuli zake hasa zikiendeshwa katika kaunti za Uasin Gishu, Nandi, West Pokot, Baringo na Turkana,” anaeleza Lily Okeyo.

Nia yake nia kuwapa wasichana nguvu za kujisimamia babadaye maishani kupitia elimu. Haya wanafanya kwa kuwalipia karo na kuwapa vifaa vya masomo kama vile begi na vitabu.

Kadhalika, wamehusika pakubwa kwa kuwaelimisha wanafunzi kuhusu usafi wakati wa hedhi, vilevile kuwapa visodo.

Kufikia sasa wameendesha shughuli zao katika vitongoji duni kadha katika Kaunti ya Uasin Gishu ambapo kwa sasa wasichana 129 wananufaika moja kwa moja kutokana na mradi huu huku wakiwa wamesambaza zaidi ya visodo 10,000.

Mpango huu kadhalika unahusisha mradi wa kutoa chakula kwa wanafunzi, suala linalohakikisha kwamba hawazuiwi kwenda shuleni kwa sababu ya njaa.

“Wazazi wa watoto hawa ni maskini sana kiasi cha kwamba hawawezi mudu kuwalisha wanao. Kutokana na suala hili tulitambua kuwa hata tunapotoa vifa vya masomo na kuwalipia wanafunzi karo, masomo hayawezi endelea wakiwa na njaa, na hivyo tukaanzisha mpango wa kuhakikisha kuwa wanafunzi hawa wanafunzi,” aeleza.

Isitoshe, wamekuwa wakihusika na elimu kuhusu masuala ya afya ya uzazi na jinsi ya kukabiliana na mihadarati, vilevile virusi vya HIV ambapo wamekuwa wakiendesha mafunzo haya kwa kuandaa warsha katika shule mbali mbali.

Haya hayaishii tu hapo kwani pia wamekuwa wakisaidia familia za wasichana wanaopokea usaidizi na hasa akina mama, kujiimarisha kiuchumi.

Haya yamefanikishwa kwa kuwasaidia kuanzisha miradi ya kujichumia riziki kama vile vyama vya kukopeshana pesa na miradi ya kilimo miongoni mwa mingine.

Na shughuli hizi zimeanza kuzaa matunda kwani jitihada. Mradi huu umeimarisha masomo miongoni mwa wanafunzi kwani umeongeza idadi ya watoto wanaohudhuria shule.

“Shughuli hizi zimehakikisha kwamba wasichana wanasalia shuleni hata siku zao za hedhi, suala ambalo halikushuhudiwa awali, na ambalo lilichangia kudorora kwa masomo miongoni mwa wasichana,” aeleza.

Ukahaba

Na suala la kugawia wasichana visodo na kusaidia familia zao kujitegemea kiuchumi limesaidia kupunguza visa vya ukahaba, viwango vya virusi vya HIV na matumizi ya mihadarati.

“Awali wasichana wengi walisukumwa katika ukahaba na maovu mengine ili kupata pesa za kukidhi haya mahitaji yao, lakini sasa hawana sababu ya kufanya hivyo,” anaeleza.

Mojawapo ya sababu zilizomchochea Bi Okeyo kuanzisha mradi huu ni kwamba aligundua kuwa wasichana wengi katika maeneo haya hasa kutoka familia maskini, walikuwa wakinyimwa fursa ya kuendelea na masomo ili kutoa nafasi kwa wenzao wa kiume kuendelea kusoma.

“Fikra hii ilinichoma sana ambapo nilitaka kuleta mabadiliko,” anaeleza.

Pia, akiwa chuoni alipata ufadhili wa kuendelea na masomo ambapo alikamilisha mwaka wa 2015.

“Kwa sasa naona itakuwa vyema kutoa usaidizi ambao mimi pia nilipokea; hasa kwa kusaidia watoto kutoka familia maskini waweze kuendelea na masomo yao,” anaeleza.

Anaamini kwamba kwa kufanya hivi, wasichana hawa pia wataendeleza mwito huu katika siku zijazo na kusaidia wenzao kusaidika kielimu.