Atumia kalamu ya wino kuchora

Kevin Wesah

Kevin Wesah, mchoraji anayetumia kalamu ya wino. Picha/KENNEDY KIMANTHI 

Na KENNEDY KIMANTHI

Imepakiwa - Sunday, March 19  2017 at  15:17

Kwa Mukhtasari

Kalamu ya wino si kifaa cha kawaida kwa wachoraji wengi hapa nchini Kenya lakini kwa Kevin Wesah ina umuhimu mwingi kwa kazi yake.

 

KALAMU ya wino si kifaa cha kawaida kwa wachoraji wengi hapa nchini Kenya lakini kwa Kevin Wesah ina umuhimu mwingi kwa kazi yake.

Wesha, 28, hupendelea sana kuchora picha zake kwa kalamu za wino; hasa za rangi za samawati na nyeusi.

Ustadi na ukakamavu wake katika uchoraji umemshindia mashabiki chungu nzima wanaoamini na kuthamini kazi yake.

Wesah amekuwa akichora tangu utotoni.

“Nilikuwa na kipaji cha uchoraji na ushairi. Vipaji hivi nilivigundua nilipokuwa mdogo sana,” aliambia Swahilihub.

Alipoenda katika Shule ya Upili ya Mtakatifu Petero Mumias katika kaunti ya Kakamega mwaka wa 2003, alisomea sanaa kama mojawapo ya somo lililompendeza sana.

Shuleni humo, alijifunza uchoraji wa picha akizangatia usawa wa rangi inayohitajika na karatasi zipi zinafaa kutumiwa katika uchoraji.

Mwaka wa 2006, alipata alama ya B kwenye somo la sanaa katika mtihani wa kidato cha nne wa Kiswahili KCSE.

Hata hivyo, safari yake ya kuendelea na sanaa haikuwa rahisi.

Alijiunga na chuo kikuu cha Kenyatta mwaka wa 2008 ambako alitarajiwa kusomea somo la kemia.

Kwa miaka mitatu, alifanya juu chini kusoma lakini akashindwa.

“Sikupenda somo hilo hata kidogo na sikuenda darasani kusoma kwani sikuwa na hamu ya kemia. Mara nyingi nilijipata katika ukumbi wa sanaa wa KU. Ndani ya ukumbi huo kuna picha nyingi sana za kupendeza ambazo zilinipa msukumo wa kuchora zaidi,” asema Wesah.

Mwaka 2012, aliamua kuacha masomo yake ya kemia ili kuanza uchoraji. Hakumhusisha yeyote katika uamuzi huu.

“Mamangu alikasirika na hatua niliyochukua kwani alisema nilimpotezea pesa na raslimali zake nyingi katika miaka tatu niliyokuwa KU,” Wesah alisema.

Katika mwaka wa 2013, alijiingiza kikamilifu katika biashara ya sanaa na kuanza kutafuta umaarufu kwenye mitandao ya Facebook akijiita Wesah_n_Biro.

Mkakati huo ulifanya kazi na akaanza kupata wateja wengi.

Picha ya kwanza ya ukubwa wa A3 aliyochora alilipwa Sh800.

“Niliichora kwa karatasi spesheli ambayo iko na uzito mwingi na ni laini zaidi kushinda karatasi ya kawaida,” Wesah alielezea Swahilihub.

Mashindano

Juhudi zake zilimsaidia aliposhinda mashindano ya uchoraji yaliyoandaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom katika mwaka wa 2014.

“Shindano hilo lilikuwa la kupigia debe mojawapo ya bidhaa zao kwa njia ya sanaa. Nilishinda Sh50,000. Ilikuwa hatua muhimu sana katika uchoraji wangu,” Wesah ambaye anawaiga wachoraji shupavu kama Nuru Bahati na Elias Mungora anasema.

Akitumia pesa hizo, alihama nyumbani kwa mamake katika mtaa wa Kayole na kuhamia katika nyumba kubwa mtaani humo humo ambako angefanya kazi yake katika nafasi kubwa.

Pia alinunua vifaa kama meza ya kuchoirea, karatasi za kuchorea na fremu za picha.

Anahisi vipi kufanyia kazi nyumbani?

“Hakuna tofauti na yule anayeenda ofisini kila asubuhi. La muhimu ni kuhakikisha unatilia maanani kazi yako na uifanye inavyohitajika,” Wesah alisema.

Ukubwa

Picha anazozichora zina ukbwa tofauti.

Picha ya A3 huuza kwa Sh4,000, A2 kwa Sh10,000 na ile ya A1 kwa Sh20,000.

Kutokana na biashara hii, anaunda kati ya Sh50,000 na Sh60,000 kila mwezi.

Kiasi hiki kinaweza kuongezeka wakati wa likizo kama vile siku ya Wapendanao, Pasaka, Siku ya Kuzaliwa na Krismasi

Kulingana na Wesah wateja wake wengi ni wapendanao.

Kutokana na pesa hizi, analipa bili zake, anahifadhi zingine na pia anamlipa mwajiriwa wake anayeweka picha kwenye fremu na glasi.

Picha ya A3 huchorwa kwa siku nne ilhali ile ya A2 hukamilika na siku 10.

Picha ya A1 ambayo ndiyo kubwa zaidi huchukua muda wa wiki mbili kukamilika.

“Picha nzuri inafikisha ujumbe kwa urahisi. Uga wa sanaa uko na mpigo mpana sana,” anaeleza.