http://www.swahilihub.com/image/view/-/3460250/medRes/1493938/-/uf9h6k/-/ganze.jpg

 

Njaa: Bajeti ya mabilioni bado kuwaauni Wakenya kikamilifu

Njaa Ganze

Wakazi wa Ganze, kaunti ya Kilifi wasubiri chakula cha msaada. Baa la njaa linawatatiza mwaka huu 2016. Picha/CHARLES LWANGA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Monday, January 9  2017 at  08:45

Kwa Mukhtasari

Kenya ni taifa la kutangaza migao ya bajeti ya mabilioni ya pesa kila mwaka kufadhili miradi ya kilimo cha unyunyiziaji lakini ukame unaandamana na janga la njaa na kiu.

 

KENYA ni taifa la kutangaza migao ya bajeti ya mabilioni ya pesa kila mwaka kufadhili miradi ya kilimo cha unyunyiziaji lakini ukame unaandamana na janga la njaa na kiu.

Tangu serikali itangaze 2004 kuwa imo mbioni kuafikia malengo ya ruwaza ya 2030 ya kupambana na ukame kupitia uchimbaji wa mabwawa na kufadhili miradi ya kilimo cha unyunyiziaji, hadi sasa imetangaza kutengwa kwa Sh110 bilioni katika ripoti zake za bajeti kila mwaka wa kifedha.

Migao hiyo ni kati ya Sh130 bilioni ambazo imetangaza kuwa inahitaji kwa awamu tano za hadi mwaka wa 2025 ili kufanikisha lengo lake la kuweka hekari 700,000 chini ya kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji.

Akiongea hivi majuzi katika mradi wa unyunyiziaji wa kijamii katika Kaunti ya Murang'a wa Thathawa ambapo alitoa ufadhili wa serikali wa Sh10 milioni, mkurugenzi wa huduma za Unyunyiziaji mashamba hapa nchini Bw Robinson Gaita alisema kuwa pesa hizo zikitumika vizuri taifa hili litapata utoshelevu wa chakula na liwe na cha ziada kuuzwa katika masoko mbalimbali.

Njaa

Sasa maeneo mengi yanalia kuhusu uwezekano mkubwa wa hatari ya njaa kufuatia ukosefu wa mvua ya kutosha ambapo maeneo mengi hayatapata mavuno msimu huu.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa wanawake wa Kiambu bungeni Bi Nyokabi Gathecha, kaunti ya Kiambu kwa sasa iko katika hatari ya kukumbwa na janga la njaa na "tunaomba serikali itupe chakula cha msaada.”

Anasema kuwa maeneo ya Ndeiya na Juja tayari yameanza kukumbwa na janga la njaa “na hatutaki kusikia kuwa misaada ya chakula inapelekwa katika eneo la Kaskazini Mashariki pekee kwa kuwa hata sisi tumeathirika.”

Athari ni kuwa, msimu huu kutashuhudiwa upungufu mkali wa mavuno ya nafaka na kwa kawaida, bei ya unga itapanda hivi karibuni kwa kiwango kikubwa.

Kaunti za eneo la kati na Rift Valley ambazo hufaa taifa hili na mavuno ya mahindi tayari zimetangaza mimea kukauka mashambani kupitia ukosefu wa maji, hili likiwa ni janga la mwaka mpya 2017 ambalo linawaandama Wakenya.

Gavana wa Kirinyaga Bw Joseph Ndathi tayari ametoa onyo kuwa eneo hilo limekumbwa na uhaba mkubwa wa mchele kwa kuwa “mradi wetu wa ukuzaji mpunga ulikumbwa na ukosefu wa maji ya kilimo kiasi kwamba mavuno yamesambaratika kwa kiwango cha asilimia 70.”

Katika eneo hilo, serikali imetangaza bajeti ya Sh16 bilioni za kujenga bwawa la maji la kuzidisha kilimo cha mpunga lakini hadi sasa, bwawa hilo bado halijajengwa.

Kiangazi

Waziri wa Ugatuzi Bw Mwangi Kiunjuri ambaye amekuwa katika mstari wa mbele katika kutangaza bajeti hizo za kujenga mabwawa hapa nchini tayari amekiri kuwa “kuna hatari ya janga la njaa kwa kuwa mvua imetufeli kabisa.”

Anasema kuwa mvua inayotegemewa kugurumisha mavuno tosha ni ya kati ya mililita 1,000 na 1,500 lakini tumepata mililita chini ya 500 msimu huu.

Katika hali hiyo, lishe kwa binadamu na kwa mifugo imeadimika na darubini ya kesho ya Wakenya kilishe inaonyesha tu giza.

Swali ni je: Mabilioni ya pesa kuzidisha maji yametangazwa kila mwaka, lakini mabwawa yenyewe hayaonekani na yakionekana, hakuna manufaa kwa unyunyiziaji: Pesa hizo huwa na manufaa gani ikiwa Wakenya hawaonekani kupata afueni ya maji?