Ni balozi wa kukabiliana na ulanguzi wa binadamu

Sophie Otiende

Bi Sophie Otiende, balozi wa harakati za kukabiliana na ulanguzi wa binadamu, yaani utumwa mamboleo, hapa nchini. Vile vile, anahudumu kama mshauri wa miradi katika shirika lisilo la serikali la kukabiliana na ulanguzi wa binadamu, Haart. Sophie amewahi kuathirika na utumwa mamboleo. Picha/HISANI 

Na CAROLYNE AGOSA

Imepakiwa - Thursday, November 19  2015 at  16:20

Kwa Mukhtasari

Bi Sophie Otiende ni balozi wa harakati za kukabiliana na ulanguzi wa binadamu nchini Kenya na mshauri wa mradi wa shirika la kukabiliana na ulanguzi wa binadamu - Haart.

 

VISA vya Wakenya kutoroshwa Mashariki ya Kati kutumiwa kama wajakazi wa nyumbani vimekuwa jambo la kawaida. Siku baada ya nyingine twapokea habari za Wakenya hawa wakiwa katika hali ya kutamausha baada ya kutendewa ukatili na wenyeji wao.

Tatizo ni kuwa Wakenya hawa hawawezi kurejea nyumbani pasipo kwa hiari ya waajiri hao ambao hutwaa pasipoti na hati zao zingine muhimu za usafiri.

Hii ni aina moja tu ya visa vya ulanguzi wa binadamu, yaani utumwa mamboleo.

Mateka hawa hufanyishwa kazi ngumu katika mazingira duni. Wanalipwa ujira mdogo ama kunyimwa kabisa pato lao. Mara kwa mara wanateswa na kudhulumiwa kimapenzi.

Watu wengi wamenaswa katika minyonyoro hiyo kupitia umaskini, kutojua, vitisho, kulazimishwa, kutekwa nyara, ulaghai ama hila.

Soko hilo limeenea hata Amerika ya Kusini, Ulaya na mataifa mengine ya Afrika ambako mateka hawa hufanywa watumwa wa ngono.

Cha kusikitisha ni kwamba yanatendeka hata humu nchini ila kwa njia fiche. Ajira ya watoto, wajakazi wa nyumbani wa kulazimishwa na ukahaba wa kulazimishwa ni baadhi tu ya mifano.

Uhalifu huo umenawiri mjini Nairobi, Mombasa Kwale, Suba, Turkana na eneo la Magharibi.

Watoto na wanawake ndio waathiriwa wakuu hasa wanaotoka familia maskini, mayatima, wakimbizi ama hawana makazi.

Watoto hawa wanatumiwa kama wajakazi wa nyumbani, kufanya kazi ngumu za shambani, kuchuuza bidhaa barabarani, kuingiza bidhaa haramu nchini maeneo ya mpakani. Pia hutumiwa kama kafara na makahaba.

Miezi michache iliyopita Kenya ilizindua Mpango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Ulanguzi wa Binadamu 2013-2017.

Bi Sophie Otiende ndiye balozi wa harakati hizi humu nchini na mshauri wa mradi wa shirika la kukabiliana na ulanguzi wa binadamu - Haart.

Bi Otiende aliwahi kuwa mwathiriwa wa uovu huu.

 

Tueleze kifupi shughuli za Haart hasa ni zipi?

Ni shirika lisilo la serikali la kukabiliana na ulanguzi wa binadamu. Mimi ni mshauri wa miradi. Liliundwa 2010 kuhamasisha umma kuhusu utumwa huu kupitia makundi ya kijamii mashinani.

Huwasaidia waathiriwa, hushiriki katika uundaji sera na pia kushirikiana na wadau wengine kukomesha visa hivyo. Pia huwashtaki wakosaji.

 

Je, ulijua wewe ni muathiriwa?

La hasha! Ni rafiki yangu mmoja alinigutusha. Waathiriwa wengi hawajui ni mateka, na hiyo ndiyo changamoto kuu katika kukomesha tatizo hili.

Aidha, visa hivi hutumbukizwa katika kopo la dhuluma za kijinsia, dhuluma za kimapenzi, ama suala la utunzi wa watoto.

Kumbe ni visa ambavyo vimekuwepo tangu zamani ila kwa njia isiyo ya wazi kupambanua. Ni kawaida kusikia wasichana wachanga wamehadaiwa na jamaa zao eti wanapelekwa mjini kuendeleza masomo, kumbe wataishia kuwa wajakazi wa nyumbani. Ama visa vya wanadada kutoka jamii maskini kuahidiwa kazi na wahisani lakini wanapelekwa mafichoni na kugeuzwa watumwa wa ngono.

Ukizingatia haya utagundua kuna maelfu ya waathiriwa wanaoumia gizani. Ni ufichuzi ulionipa msukumo hata zaidi wa kujiunga na harakati hizi.

 

Tueleze kwa ufupi kisa chako

Nilizaliwa katika familia iliyoweza kujikimu. Baba alikuwa na kazi nzuri na alijiweza kifedha. Kwa bahati mbaya alipoteza kazi na masaibu yakaanza. Tulilazimika kuishi katika mtaa wa mabanda.

Licha ya hilo baba alikataa kabisa kutuhamishia shule za gharama ya chini. Nilipofika darasa la saba ilibidi auze kila kitu cha thamani nyumbani ili kupata karo.

Akampa mjombangu pesa alizokuwa nazo ili anipeleke shuleni lakini hakufanya hivyo. Nadhani alitumia pesa hizo akitarajia kupata zingine.

Mjomba akanigeuza mjakazi nyumbani kwake Kisumu huku wanawe wakiendelea na masomo. Katika kipindi hicho cha karibu mwaka mmoja nilisumbuka sana na hata kudhulumiwa kimapenzi.

 

Nani aliyekuokoa?

 Siku moja mwezi Novemba nilipata fursa ya kwenda mjini. Bahati iliyoje kukutana ghafla na rafiki ya mamangu. Aliponitazama tu alijua mambo hayakuwa shwari.

Alimpasha habari mama na keshoye mama alifika kunichukua. Nikarudi nyumbani na kurejea shuleni.

 

Je, ulipata ushauri wowote kukabiliana na madhara ya kipindi hicho?

La! Tulikuwa tunapitia wakati mgumu kama familia na hivyo mzigo ungekuwa mzito zaidi.

Pili, nilikuwa mtoto kidomodomo na sikudhani yeyote angeniamini. Fedheha na woga zilinifanya kunyamaza. 

Ni hadi nilipofika chuo kikuu ndipo nilianza kutafuta usaidizi wa wataalamu. Imenichukua miaka mingi kukabiliana na wingu hilo jeusi.

Mwenyewe hata sikujua ninachokumbana nacho. Ni hadi sasa nilipojiunga na Haart ndipo nilifahamu kumbe nilikuwa mmoja wa waathiriwa wa utumwa mamboleo.

 

Moja ya mbinu mnazotumia kueneza ujumbe wenu ni sanaa? Eleza.

Jina la mradi ni Arts to End Slavery ambapo tunatumia sanaa kama njia ya kueleza vyema zaidi ulanguzi wa binadamu kwani sio rahisi kupambanua.

Ni mradi mchanga ulioanza mnamo 2014.  Katika hafla ya uzinduzi tulikuwa na maonyesho ya picha, michoro na vinyago vya wasanii mbalimbali wa humu nchini na kigeni. Tunalenga pia kutumia densi na tamthilia. Vile vile, mashirika ya kutetea haki za binadamu na kijamii kama vile Pawa254 lake mwanaharakati Boniface Mwangi (maarufu kwa michoro katika barabara za mji wa Nairobi kuashiria ulafi wa wanasiasa).

 

Mojawapo ya jukumu kuu la kampeni hizi ni kuwalinda waathiriwa. Fafanua.

Kwanza tunawahoji kubaini hali yao halisi. Lazima mtu awe amesajiliwa kwa kitu fulani, amesafirishwa kutoka eneo moja hadi lingine, na ametumiwa vibaya. Vigezo hivi havizingatiwi kwa watoto kwa sababu mtoto hafanyi lolote kwa hiari yake. 

Kisha tunawapa waathiriwa ushauri nasaha na usaidizi wanaohitaji.

Pia tunatoa mafunzo kuhusu uhamiaji salama, haki zao na jinsi ya kupata usaidizi wakijipata pabaya.

Vile vile tunatoa mafunzo ya kiuchumi ili kuwawezesha waathiriwa kujitafutia kibaba.