Bangi: Hisia mseto

Bangi

Misokoto ya bangi iliyokuwa imenaswa awali. Picha/MAKTABA 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Saturday, April 8  2017 at  00:53

Kwa Mukhtasari

Swala la kuhalalisha matumizi ya bangi limepokelewa kwa hisia tofauti na kuzua mjadala mkali miongoni mwa Wakenya.

 

SWALA la kuhalalisha matumizi ya bangi limepokelewa kwa hisia tofauti na kuzua mjadala mkali miongoni mwa Wakenya.

Hii ni baada ya mtafiti mmoja hapa nchini, Gwada Ogot, kujitokeza Alhamisi na kuwasilisha pendekezo la kuhalalisha matumizi ya marijuana katika bunge la seneti.

Aidha Bw Ogot ambaye pia ni mwandishi anashikilia almradi mataifa kama Ujerumani, Israel na Ufilipino yalihalalisha matumizi ya marijuana basi ni wakati murwa Kenya kama taifa lenye demokrasia kuhalalisha bangi nchini akieleza ina manufaa tele kwa kutibu takriban magonjwa 677 kando na manufaa ya kuwa kitega uchumi.

"Mataifa kama vile Ujerumani, Israel na Ufilipino yalihalalisha bangi mwezi mmoja uliopita. Kwa nini Kenya isihalalishe pia, ikikumbukwa kwamba mmea huu una manufaa mengi kama vile kutibu magonjwa takriban 677 na kuingizia taifa fedha?" akadokeza Bw Ogot akihojiwa na vyombo vya habari Alhamisi.

Pendekezo la Bw Ogot kutoka Kaunti ya Siaya lilijiri wakati ambapo Seneta wa Nyamira  Kenneth Okong’o Mong’are amekuwa akionekana kuunga mkono kuhalalishwa kwa marijuana nchini. Seneta Mong'are akipeana mfano wake kuwa mtumizi wa bangi, alihoji amepiga hatua kubwa kimaisha kiasi cha kuwa seneta. "Haimaanishi mmea huo ukihalalishwa utaathiri maisha ya watu. Inategemea kiwango cha mtumizi. Mimi kama mfano mzuri nimeitumia. Nilikuwa nchi ya India ambapo mmea huu umehalalishwa, marijuana ni ya dhamana kuu iwapo watu wataitumia kwa shime. Mtu anaweza akaamua kutoitumia na huo ni uamuzi wake" akanukuliwa Seneta Mong'are.

Je, umeshawahi jisaili iwapo marijuana itahalalishwa na kutambulika kutokuwa miongoni mwa dawa za kulevya nchini?

Swala hili limesababisha Swahilihub kuhakikisha inatangamana kupokea maoni mbalimbali ya wananchi ili kuskia ufahamu wa kuhalalisha marijuana.

Wananchi wengi walionekana kukashifu vikali uhalalishaji wa mmea huu.

"Hapa Kenya ikihalalishwa, basi huo ndio mwisho wa taifa! Kama vile ilivyo tu kwa wachache wanaoitumia kisiri, madhara yake ni mengi sana kuliko matarajio, sembuse iwe halali? Huyu jamaa anafaa aambiwe Wakenya sio Wajamaica kamwe!" akasema Cheche Kanavule wakati wa mahojiano.

"Wakati mwingine watu huingiwa na ibilisi. Hawawezi wakaona jinsi jamii ilivyo potoka siku hizi. Si ubakaji, wizi, uhalifu na mauaji, bangi ikilihalalishwa visa kama hivi vitakuwa wimbo wa kila siku," akasema Beky Bekita akipinga swala la kuhalalisha bangi.

Wengine walidai kuwa watumizi watakosa maadili na kuwa watovu wa nidhamu.

"Napinga pendekezo hilo, kwa sababu watumiaji watakosa madili kwa kisingizio kuwa utumiaji wa bangi ni halali, hivyo napinga kabisa," akadokeza Kijana wa Teso kwenye mtandao wa Facebook.

Dawa za kulevya

Aidha kuna walioshikilia kuwa bangi ni miongoni mwa dawa za kulevya na kuhalalisha dawa za kulevya ni kukiuka sheria za taifa.

"Bangi ni dawa hatari ya kulevya, wote wanaoitumia na kuisambaza wanaswe," akasema Abraham Kirwa.

Eric Getwabu alisema, "Upuzi huo, watu wengi wanaotumia bangi hawana amani katika jamii, siungi mkono."

Hata hivyo kuna waliounga mkono pendekezo la kuhalalisha bangi wakisema matumizi yake yanategemea mtumizi mwenyewe.

"Namuunga mkono Bw Ogot kwa dhati, hapa Thika bangi huvutwa hadharani na hamna hata anayewashughulikia. Mbona mataifa mengine ni halali na hayana vituko kama Kenya?" akanukuu Arap Muge kwenye Facebook.

"Bangi si mbaya watumiaji ndio wabaya" akaongeza Batoh Fotty Wap kwenye Facebook.

"Binadamu yeyote hana uwezo wa kukataa mimea yoyote ambayo ilitengezwa na Mwenyezi Mungu," akadokeza Rono Kang'ogo Bernard.