Bodaboda iwe na utambulisho kudhibiti uhalifu

Charles Njagua maarufu kama Jaguar

Mkurugenzi wa Bodi ya Nacada, Charles Njagua maarufu kama Jaguar amvalisha mhudumu wa Bodaboda vazi maalum linalorahisisha watumizi wengine kumwona kuweza kuzuia ajali. Picha/EVANS HABIL 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, April 11  2017 at  10:28

Kwa Mukhtasari

Kila Serikali inapofanikiwa kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji katika jamii huibuka nyingine na maswali mengi.

 

KILA Serikali inapofanikiwa kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji katika jamii huibuka nyingine na maswali mengi.

Changamoto kubwa katika miaka ya nyuma ilikuwa ni ukosefu wa vyombo vya usafiri kutoka eneo moja kwenda eneo jingine. Serikali iliitatua kwa kuruhusu uingiaji wa magari na mabasi makubwa kwa madogo na katika miaka ya hivi karibuni  iiruhusu usafiri wa pikipiki maarufu kama bodabida na bajaji, pia iliruhusu usafirishaji wa pikipiki za miguu mitatu maarufu kama ‘toyo’ ama 'tuktuk'.

Utatuzi huo ulirahisisha usafiri wa watu na usafirishaji mizigo kutoka eneo moja hadi eneo jingine hata katika maeneo ambayo zamani yalikuwa hayafikiki kwa magari leo yanafikika kwa pikipki, bajaji na toyo kwa urahisi na kwa wakati wote.

Wingi wa bodaboda uliibua changamoto ya weledi wa madereva lakini askari wa usalama barabarani walianzisha na wanaendelea kusimamia mafunzo kwa madereva na uvaaji wa kofia ngumu ili kupunguza ajali na vifo kwa madereza na abiria.

Wakati changamoto hiyo bado inasumbua, imebainika kuwa bodaboda  kutokana na uharaka wa kufika eneo fulani  zinatumika katika uhalifu. Kwa mfano waliorusha bomu wakati wa uzinduzi wa jengo la kanisa la Parokia ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Olasiri, Arusha  Mei 5, 2013 walitumia bodaboda.

Wiki iliyopita Polisi walifanikiwa kuwaua  wanaume watatu wahalifu  wakati wanataka kuvuka Daraja la Benjamin Mkapa wakitokea Ikwiriri. Jamaa hao walikuwa wamepakizana  katika bodaboda  na walivaa kama wanawake na kuficha nyuso zao kwa hijabu.

Kuna ripoti nyingi za watu  kuporwa mali zao mikoba na simu- majumbani na njiani wa watu wakiwa kwenye pikipiki.

Uchunguzi wa hivi karibuni  umeoyesha kuwa pamoja na juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kufanikiwa kudhibiti matukio ya ujangili, bodaboda ambao ni usafiri unaopendwa na wengi kutokana na ufanisi na unafuu, umeibuka kuwa ni tatizo katika vita dhidi ya vitendo hivyo.

Bodaboda hivi sasa ni adui mpya wa wanyamapori na maliasii nyinginezo kutokana na majangili kuzitumia zaidi kusafirisha nyara kutoka hifadhi na  mapori ya akiba. Bodaboda zimekuwa zikitumiwa na majangili kuingia kwenye  hifadhi na kufanya  uhalifu na kutoweka kirahisi bila kukamatwa na mamlaka husika.

Kasi ya uhalifu kwa kutumia bodaboda  inafanya vita dhidi ya ujangili ilazimike kutumia mbinu mpya baada ya kuwa na mafanikio makubwa kwa kuunguza matukio hayo kwa takriban mara nne kutoka matukio 8,631 mwaka 2014 hadi 2,179   Desemba 2016.

Namba za utambulisho

Ijapokuwa lengo kubwa la kuruhusu bodaboda  ni kurahisisha usafiri na kuongeza ajira kwa vijana, Serikali na jamii kwa jumla lazima washughulikie changamoto hii ya uhalifu na sisi tunapendekeza pikipiki zote zipewe namba za utambulisho zinazoonekana kwa urahisi na zisizofutika.

Tunajua kuwa vyombo vyote vya moto vimesajiliwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Lakini kwa upekee, magari yanayosafirisha abiria mjini – mabasi na teksi yana namba za utambulisho ubavuni ambayo abiria anaweza kuitumia kuishaki ikiwa atakuwa ameonewa.

Tunashauri mamlaka husika ziangalie uwezekano  wa kuandika namba kubwa zisizofutika  katika bodaboda hizi ili ikionekana mahali popote inafanya uhalifu, iwe rahisi kufuatiliwa.

Tunapendekeza  namba zisizofutika kwa sababu wahalifu hufuta kwa urahisi namba za usajili au hutengeneza vibao vya kughushi kwa lengo la kuwapotosha wanaofuatilia.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.