http://www.swahilihub.com/image/view/-/4838674/medRes/2161870/-/hwevhy/-/inakili.jpg

 

Changamoto hizi zishughulikiwe pia

John Magufuli

Rais John Magufuli wa Tanzania. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, November 6  2018 at  06:57

Kwa Muhtasari

Miongoni mwa changamoto ambazo tungependa zishughulikiwe Tanzania ni kuhusu ukosefu wa nafasi au uhuru wa kujieleza katika jamii, kuminywa kwa demokrasia, matumizi mabaya ya sheria ya kuweka ndani watu kwa saa 48 inayotumiwa na wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na kudhibiti matukio ya watu kushambuliwa baadhi hadharani, kutekwa na wengine kuuawa na watu wasiojulikana.

 

RAIS John Magufuli ametimiza miaka mitatu tangu alipochaguliwa Oktoba 25, 2015, kisha kuapishwa kukalia kiti cha urais Novemba 5, 2015, akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Jakaya Kikwete.

Magufuli anapotazama msururu wa ahadi alizowapa wananchi wakati wa kampeni, anaona hatua aliyopiga na safari iliyo mbele yake. Ukweli katika kipindi cha miaka mitatu amefanya mambo kadhaa yanayoonekana.

Miongoni mwa mambo hayo, ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake ni ujenzi wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ambayo kwa kiasi kikubwa, na usimamizi bora wa raslimali za nchi kwa kupambana na mafisadi, wazembe kazini na wezi.

Kwa upande wa miundombinu, tumeshuhudia ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), barabara ya juu kama ilivyofanyika eneo la Tazara jijini Dar es Salaam, viwanja vya ndege pamoja na ufufuaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuipatia ndege zilizonunuliwa na Serikali. Miradi hiyo yote imegharimu mabilioni ya shilingi kutokana na fedha za walipakodi – wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara.

Kadhalika tumeshuhudia uboreshaji katika huduma ya elimu na afya. Mpango wa elimu bila malipo kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne, kuondolewa kwa michango ya ziada isiyo na tija, na ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, vyote kwa pamoja vimeongeza hamasa ya utoaji elimu kwa vijana.

Wananchi katika vijiwe na mitandao ya kijamii wanazungumzia usambazaji wa huduma ya maji na umeme mijini na vijijini pamoja na mawasiliano.

Tuna matumaini makubwa kwamba miaka michache ijayo, tutakuwa tunaishi katika taifa la asali na maziwa la watu wenye furaha, upendo na amani ikiwa kasi hii ya maendeleo itaelekezwa katika kukabili changamoto zilizojitokeza.

Miongoni mwa changamoto ambazo tungependa zishughulikiwe ni kuhusu ukosefu wa nafasi au uhuru wa kujieleza katika jamii, kuminywa kwa demokrasia, matumizi mabaya ya sheria ya kuweka ndani watu kwa saa 48 inayotumiwa na wakuu wa mikoa na wilaya, pamoja na kudhibiti matukio ya watu kushambuliwa baadhi hadharani, kutekwa na wengine kuuawa na watu wasiojulikana.

Katika kipindi hiki tumeshuhudia baadhi ya vyombo vya habari vikifungiwa, wananchi kunyimwa fursa ya kuwaona mubashara wabunge wao wakijenga hoja za maendeleo bungeni, pamoja na mikutano ya hadhara ya wanasiasa kuzuiwa.

Ni katika kipindi hiki kumekuwa na usalama mdogo baada ya baadhi ya watu kufungwa kwenye viroba na kutupwa baharini, viongozi wa serikali ngazi ya vijiji Tanga, Mwanza na Pwani wilaya za Mkuranga, Ikwiriri na Rufiji wakiuawa hadi Jeshi la Polisi lilipoweka kambi na kudhibiti.

Pamoja na polisi kuweka ulinzi mkali, jamii imeshuhudia mwanasiasa mmoja akilengwa kwa mtutu wa bastola, mwanasiasa mwingine akimiminiwa risasi, na watu kadhaa wakitekwa kama ilivyotokea hivi karibuni kwa mfanyabiashara mashuhuri Mohammed Dewji.

Tunaamini polisi wana uwezo wa kufanya uchunguzi na kuwafikisha wahalifu mahakamani ili Tanzania iendelee kujulikana kuwa kisiwa cha amani hasa katika kipindi hiki ambacho juhudi kubwa ni kuhamasisha wananchi washiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda. Jambo zuri ni kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kwa kutekeleza ahadi zake, bila shaka, hata bila kuishauri itashughulikia changamoto hizo ili zisiwe kikwazo katika shughuli za uzalishaji na uchumi.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647