Changamoto ya gharama za tiba itafutiwe dawa

Sindano

Mtu akidungwa sindano. Picha/HISANI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, July 12  2017 at  12:10

Kwa Mukhtasari

Kwa mara nyingine, juzi madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walifanya jambo jingine la maendeleo.

 

KWA mara nyingine, juzi madaktari wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili walifanya jambo jingine la maendeleo.

Waliowasha kifaa cha kuwezesha kusikia walichowapandikiza watoto watano mwaka mmoja uliopita.

Uwekaji wa kifaa hicho kinachowawezesha watoto hao kusikia kinaitwa ‘cochlea impact’.

Edwin Liyondo, daktari bingwa wa magonjwa ya koo, pua na masikio (ENT) wa hospitali hiyo alisema gharama zote za kumwezesha mtoto kutibiwa na kupata vifaa vya usikivu ni TSh37 milioni na kwamba kama watoto hao wangepelekwa India kila mtoto angelazimika kulipiwa TSh70 milioni, hivyo kuifanya huduma hiyo hapa nchini kumepunguza gharama za matibabu kwa watoto wenye ulemavu wa kusikia.

Katika kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita, madaktari wa Muhimbili hasa wa Taasisi ya  Moyo ya Jakaya KIkwete (JKCT) na Taasisi ya Mifupa (MOI) , kazi ambayo ilikuwa ikifanyika nje ya nchi tena kwa gharama kubwa ambazo wamekuwa wakifanya matibabu ambayo awali  hayakufikiriwa kabisa kama yangefanyika hapa nchini.

Mojawapo ni kupandikiza vifaa maalumu vya kusaidia mapigo ya moyo kazi ambayo ilikuwa ikifanyika nje ya nchi tena kwa gharama kubwa ambazo wananchi wengi walikuwa hawawezi kuzimudu.

Ijapokuwa hata sasa gharama hizo tunaziona kuwa zipo juu pamoja na matibabu hayo kufanyika hapa nchini, ukweli ni kwamba yanapofanyika nje ya nchi ni ghali zaidi na wakati mwingine hata mara mbili zaidi.

Kwetu jambo la msingi ni kwamba sasa  matunda ya kuwekeza kwa wataalamu wetu yanaonekana kwa kuwa wanafanya mambo yaliyokuwa yakidhaniwa kuwa yanawezekana nje tu. Tunatamani wawaambuakize wataalamu wa fani nyingine.

Pamoja na msingi huo, kwa kuwa lengo la wataalamu hao na Serikali kwa jumla ni kuhakikisha  wananchi wanapata tiba ya kisasa na kwa wakati, ni wakati sasa wa kuzingatia ni jinsi gani changamoto hiyo ya kumudu gharama za matibabu inafanyiwa kazi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi za dunia ya tatu ambazo wananchi wake hawana kipato cha kumudu si  tu gharama kubwa za matibabu, bali wakati mwingine  wanapaswa kuangalia njia bora ya kuwafikia wote wenye mahitaji.

Mojawapo ya njia ya kukabiliana na changamoto hii ilitolewa na mmoja wa wazazi wa watoto ambao  walipata huduma hiyo ya matibabu ya masikio.

Mzazi huyo Agnes Mboya aliiomba Serikali kujumuisha matibabu hayo kwenye Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili wazazi wengi zaidi waweze kumudu.

Alisema mbali na kulipia gharama hizo, kila mwaka wanatakiwa kubadilisha betri ambayo ni zaidi ya  Sh450,000 kiasi ambacho ni kikubwa kwa mwananchi wa kawaida kuweza kukimudu.

Pia aliiomba Serikali kuanzisha shule maalumau kwa ajili ya wanafunzi waliopandikizwa vifaa hiyo ili viweze kuwa endelevu. Alisema katika shule za kawaida zenye watoto wengi, ni vigumu  kutunza vifaa kwa watoto wa aina hii.

Mzazi mwingine, Easter Barnabas alitilia mkazo suala hilo akisema gharama hizo zikiwekwa NHIF  zitawasaidia wazazi wengi zaidi kujitokeza  kuwatibu watoto wao akisema kuna watoto wengi mitaani ambao ni walemavu wa kusikia ambao kwa gharama hizo ni vigumu kutibiwa.