http://www.swahilihub.com/image/view/-/4959886/medRes/2238751/-/15tfwdyz/-/mwaibola.jpg

 

Uchambuzi: Daladala zirudishwe Kimara kushindana na mabasi yaendayo kasi

David Mwaibula

Aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Mamlaka ya Leseni za Usafiri Dar es Salaam, David Mwaibula. Picha/MAKTABA 

Na BADRU KIMWAGA

Imepakiwa - Thursday, January 31  2019 at  12:47

Kwa Muhtasari

Wakati awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (Udart) ulipokuwa unazinduliwa, Januari mwaka 2017 wakazi wa Dar es Salaam walikuwa na matumaini makubwa na mradi huo.

 

WAKATI awamu ya kwanza ya mradi wa mabasi yaendayo haraka (Udart) ulipokuwa unazinduliwa, Januari mwaka 2017 wakazi wa Dar es Salaam walikuwa na matumaini makubwa na mradi huo.

Hii ni kwa sababu wengi waliamini na kutegemea ungewapunguzia kero wanazokumbana nazo kwenye daladala. Hakuna ubishi daladala ni kero kwa abiria wengi wa jijini Dar es Salaam, hasa tangu aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Mamlaka ya Leseni za Usafiri Dar es Salaam, David Mwaibula aondoke.

Mwaibula alikuwa kiongozi wa vitendo, alisimamia alichokisema ndio maana mpaka leo wakazi wa Dar wanakumbuka jinsi alivyorahisisha usafiri kwa kuanzisha ruti ndefu na mpya.

Hata hivyo, baada ya usafiri huo wa umma kuwekwa chini ya Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mambo yalianza kwenda ovyo kwani madereva wa daladala walifanya watakavyo.

Hakukuwa na wa kuwagusa kwa vile wasimamizi wa mamlaka hiyo wamezoea kufanyia kazi ofisini tofauti na Mwaibula aliyekuwa akizifuatilia daladala barabarani na kuwanyoosha waliojifanya kichwa ngumu.

Kwa wanaokumbuka enzi hizo, watumishi wa daladala walikuwa wakimuogopa Mwaibula kuliko trafiki tofauti na ilivyo sasa ambapo trafiki ndio tishio kwa watu wa daladala.

Hivyo, wakati mabasi ya mwendokasi yalipozinduliwa wengi waliamini kero, adha na manyanyaso waliyokuwa wakiyapata yamefika ukingoni.

Wengi waliuona usafiri huo ni mkombozi dhidi ya madhira ya daladala lakini sasa wanalia kila uchao, bora daladala zirudishwe kuliko hali wanayokumbana nayo kwenye vituo vya mabasi hayo.

Kwa sasa usafiri wa mwendokasi umeondoa kero ya kukaa kwenye foleni lakini tabu nyingine ni zaidi ya walizokuwa wakikumbana nazo katika daladala. Hii ni hasa kwa abiria wa Kimara-Kivukoni, Kimara-Gerezani hata Kimara-Mbezi, zaidi asubuhi na jioni.

Hii ni kwa sababu ili upate usafiri huo, kwanza lazima uwe umekula na kushiba kukuwezesha kukabiliana na kivumbi cha kuupanda.

Abiria wanajazana vituoni hata kuhatarisha afya zao huku wenye mahitaji maalum kama wazee, watoto, wajawazito, walemavu na wagonjwa ikiwa ni mateso zaidi kwao.

Hakuna utaratibu mzuri wa kupanda magari hayo isipokuwa kwa kutumia nguvu na ubavu. Kinachoumiza na ninachoikumbusha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, watoa huduma hiyo wanadengua kama wale wa daladala tu.

Kama waziri anadhani usafiri huo upo poa, ajaribu siku moja kuvua suti na kujitosa asubuhi kutoka Kimara kwenda mjini kisha jioni arudi kutoka Gerezani au Kivukoni kuelekea Kimara aujue muziki wa mabasi hayo ulivyo.

Kuna wakati abiria husubiri lakini mabasi yameegeshwa na madereva wakipiga stori na wakata tiketi wakiendelea kuuza bila kujali lolote.

Umati unaokuwa kwenye vituo hivyo hasa kuanzia safari kama Kimara Mwisho sio tu ni kero kwa watumiaji wa usafiri huo bali inahatarisha afya zao. Abiria wanakuwa kwenye tishio la kuambukizana kifua kikuu na magonjwa mengine ya njia ya hewa au ngozi.

Kuna kero katika upandaji hata ukiwa ndani raha yote inaisha kwa mbanano uliopo huku kila kituo basi likisimama kuruhusu abiria kuingia au kushuka ukiacha mabasi ya express.

Kila nionapo abiria walivyojazana vituoni na ndani ya mabasi ya mwendo wa haraka kwa mbanano wa kiwango cha aina yake, huwa nazikumbuka takwimu za maambukizi ya kifua kikuu zitolewazo kila Machi 25.

Taarifa za mwaka 2018 zinakadiria watu 160,000 wanaambukizwa kifua kikuu kila mwaka. Mwaka 2016 kwa mfano, inaonyesha watu 65,908 walibainika kuwa na ugonjwa huo huku 94,000 sawa na asilimia 59 hawakugundulika.

Watu hao kwa kutogundulika walikosa matibabu hivyo kuyaweka hatarini maisha yao na ya watu wengine ya kuambukizwa kwa njia ya hewa, ndipo hapo hofu inapokuja kutokana na mbanano na mshonano wa abiria vituoni na ndani ya mabasi ya mwendokasi.

Kwenye maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani mwaka jana, kaulimbiu ilikuwa inasema ‘’viongozi tuwe mstari wa mbele kuongoza mapambano ya kutokomeza TB.

Hivyo, viongozi wayaangalie mabasi ya mwendokasi kuwaokoa watumiaji wake, kinga ni bora kuliko tiba.

Rai yangu kwa Serikali, kama vipi, waruhusu daladala kutoa nafuu na kuwanusuru abiria wanaosumbuka. Tupo kwenye soko huria, tuwaondoe wasiojali wateja wao.

Badru Kimwaga ni mwandishi wa Mwananchi jijini Dar es Salaam; anapatikana kwa simu namba +255713-229787