http://www.swahilihub.com/image/view/-/3501496/medRes/1523548/-/9h7alsz/-/rapoka.jpg

 

Hongera Matiang’i lakini tunahuzunika kwa 'E’ 33,000

KCSE 2016

Rais Uhuru Kenyatta (kulia) apokezwa ripoti kuhusu matokeo ya KCSE 2016 kutoka kwa Waziri Dkt Fred Matiang'i Desemba 29, 2016. Picha/PSCU 

Na MHARIRI - TAIFA LEO

Imepakiwa - Friday, December 30  2016 at  17:04

Kwa Mukhtasari

Matokeo ya Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) yaliyotolewa Alhamisi na Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i yaliashiria uwezo halisi wa kimasomo wa wanafunzi nchini.

 

MATOKEO ya Mtihani wa Kitaifa Kidato cha Nne (KCSE) yaliyotolewa Alhamisi na Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i yaliashiria uwezo halisi wa kimasomo wa wanafunzi nchini.

Japo ilikuwa jambo la kushtusha kwa zaidi ya watahiniwa 33,399 kupata alama ya 'E’, huu ni ukweli mchungu ambao washikadau wote wa sekta ya elimu wanapaswa kuumeza.

Uhalisia wa matokeo hayo ni kutokana na juhudi za Dkt Matiang’i na kundi lake ambao wanapaswa kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha wanaolala kazini wameadhibiwa.

Huu ndio mwanzo wa kuondoa wataalamu feki katika taasisi mbalimbali na sharti uungwe mkono na washikadau wote.

Prof Matiang’i alianza kazi katika Wizara ya Elimu wakati washikadau katika sekta hiyo walikuwa wanalaumiana kwa uchafu na mizozo iliyotawala wizara hiyo.

Tunakubaliana na kauli ya mwenyekiti wa Baraza la Mitihani nchini(Knec) Prof George Magoha kuwa changamoto kubwa itakuwa kudumisha juhudi zilizoanzishwa na Wizara ya Elimu.

Juhudi hizo za kulainisha sekta ya elimu kwa kuvunjilia mbali bodi ya Knec sasa zinapaswa kuenezwa katika vyuo vikuu na taasisi za kiufundi.

Baadhi ya vyuo vikuu, hasa vile vya kibinafsi vimegeuka na kuwa vituo vya biashara kwa yeyote anayetaka kununua cheti.

Sharti Dkt Matiang’i ahakikishe elimu ya juu imerejesha hadhi pia kwa kuanzisha mchakato wa kuwapiga msasa wahadhiri wote pamoja na kutathmini upya kozi zinazofundishwa vyuoni.

Upinzani mkubwa

Japo Dkt Matiang’i alikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya maafisa wa vyama vya walimu, alitumia mdahalo kushauriana na wadau wote, hatua ambayo imezaa matunda.

Ni wazi kuwa kwa kiasi kikubwa Dkt Matiang’i amefaulu kuzima matapeli waliokuwa wanafaidika kutoka na wizi wa mitihani.

Kwa ushirikiano na taasisi mbalimbali za serikali, Dkt Matiang’i ameafikia matokeo ambayo zaidi ya mawaziri kumi wa elimu walishindwa kuafikia.

Hongera Dkt Matiang’i lakini fahamu kuwa kutaendelea kuwepo na upinzani mkali hasa kutoka kwa baadhi ya vyuo vya kibinafsi ambavyo vimechangia sana kushusha hadhi ya elimu nchini.