http://www.swahilihub.com/image/view/-/4633296/medRes/2023639/-/y4p8ed/-/chiku.jpg

 

Elimu Dengue, Chikungunya ni wakati wake sasa

Mbu

Mwanamke akiwa na kijijarida cha maelezo kuhusu mbu aina ya Aedes aegypti Februari 17, 2016,mjini Cali, Colombia. Mbu huyu anahusishwa na usambazaji wa Zika, Dengue, na Chikungunya. Picha/AFP 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, June 27  2018 at  08:06

Kwa Muhtasari

Kinachoonekana ni kuwa ugonjwa wa Chikungunya upo zaidi katika nchi jirani ambako ndiko waliobainika kuwa nao pale Holili walikotoka.

 

JUMANNE katika toleo la gazeti la Mwananchi kulikuwa na habari iliyohusu magonjwa mawili; Dengue na Chikungunya ambayo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyazungumzia wakati akizungumza na mkurugenzi mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt Adiele Onyeze.

Waziri Ummy alisema magonjwa hayo yameingia nchini, lakini Serikali imejipanga kukabiliana nayo kwa kuwa na mikakati kadhaa ikiwamo kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji utakaokuwa na vituo maalumu na hasa Dar es Salaam na Tanga.

Kwa mujibu wa waziri huyo, watu wanne wa familia moja wamebainika kuugua Chikungunya wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na wengine 226 wameugua Dengue jijini Dar es Salaam.

Akasema Serikali inaendelea kuimarisha utambuzi wa magonjwa haya katika maabara ili kuyathibitisha, lakini changamoto kubwa ni vituo vyetu vya afya na hospitali na hasa za watu binafsi akiomba waipatiwe taarifa Serikali pindi watu wanapobainika kuugua maradhi hayo.

Chikungunya ni ugonjwa mpya masikioni mwa wengi hapa nchini hata kama umekuwapo au uliwahi kuwepo nchini, lakini Dengue iliwahi kuripotiwa jijini Dar es Salaam miaka michache iliyopita na ikadhibitiwa.

Kwa kiasi fulani, wakati mlipuko wa Dengue ulipotokea katika miaka ya 2010, 2013 na 2014, elimu ilitolewa na ndiyo maana ilisaidia kuudhibiti ugonjwa huo. Pongezi kubwa ziende kwa Serikali wakati huo maana ilipambana kuhakikisha kwamba unatokomezwa.

Kuhusu Chikungunya, inaelezwa kwamba walioripotiwa kuugua hivi karibuni walibainika katika kituo cha mpakani cha Holili wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, wakiwa ni watu wanne wa familia moja waliokuwa wakitokea Mombasa nchini Kenya.

Watu hao walibainika kuwa na dalili zinazofanana za homa ya Chikungunya na sampuli za damu iliyochukuliwa na kupelekwa maabara, majibu ya vipimo yalionyesha kuwa na maambukizi ya vimelea vya ugonjwa huo.

Kinachoonekana ni kuwa ugonjwa huu upo zaidi katika nchi jirani ambako ndiko waliobainika kuwa nao pale Holili walikotoka.

Utoaji wa elimu

Kutokana na hali hiyo tunaiomba Serikali kuelekeza nguvu kubwa katika utoaji wa elimu ili kukabiliana na Chikungunya ambayo mpaka sasa ni watu wachache wanaoijua na pia wanaoifahamu kinga au tiba yake.

Dalili za ugonjwa huo zinaelezwa kuwa sawa na zile za Dengue ambazo ni homa ya ghafla, kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu ambazo kwa jumla huanza kujitokeza siku ya tatu hadi 14 tangu mtu anapoambukizwa.

Inaelezwa kwamba wakati mwingine dalili za Dengue na Chikungunya hufanana na za malaria, lakini mara nyingine huambatana na kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na njia ya haja kubwa au ndogo.

Hizi ni dalili zinazopaswa kufahamika kwa jamii ili kuirahisishia kujua namna ya kuutambua ugonjwa huo. Si hivyo tu, lakini pia tunapenda kujua maambukizi yake yanakuwaje. Kama Dengue inaambukizwa na mbu aina ya aedes na Chikungunya ni mbu huyohuyo, tutawadhitije wadudu hao?

Hata hivyo, wakati tukiipa Serikali changamoto na kuiomba itoe elimu zaidi juu ya magonjwa hayo, ni vyema huku mitaani tujitahidi kuweka safi mazingira yetu kwa kuepuka kuishi na maji yaliyotuama, kwani mbu siku zote hufuata na kuishi palipo na madimbwi au maji yaliyotuma ama nyasi ndefu. Usafi ni uhakika wa kuwa na maisha yenye afya na salama, hivyo tujikite katika usafi wa mazingira.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647