Elimu inahitajika matumizi ya taasisi za fedha

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Friday, June 16   2017 at  11:18

Kwa Mukhtasari

Kifo cha mfanyabiashara wa Shinyanga Maduhu Masunga, 75, aliyefariki wakati akijaribu kuokoa mamilioni ya shilingi alizokuwa amehifadhi nyumbani kwake ni ishara mbaya kwamba bado tuko nyuma katika matumizi ya benki na taasisi za fedha.

 

KIFO cha mfanyabiashara wa Shinyanga Maduhu Masunga, 75, aliyefariki wakati akijaribu kuokoa mamilioni ya shilingi alizokuwa amehifadhi nyumbani kwake ni ishara mbaya kwamba bado tuko nyuma katika matumizi ya benki na taasisi za fedha.

Masunga alifariki dunia Jumatatu katika eneo la Kirumba Mwanza. Baada ya moto huo kuzimwa na Kikosi cha Zimamoto, zaidi ya shilingi 230 milioni ziliokolewa na kiasi kingine kisichofahamika kikiwa kimeteketea.

Mkanda wa video uliorekodiwa kwenye eneo la tukio ulionyesha askari wakimwaga noti zilizokuwa katika ndoo ya plastiki kwenye shuka. Baadhi ya noti zikiwa zimeungua na nyingine zikiwa salama.

Taarifa kutoka katika familia yake zimesema mzee huyo ambaye alijikita katika biashara ya sekta ya nyumba na hoteli hakuwa na tabia ya kuhifadhi fedha zake benki badala yake alikuwa akizihifadhi ndani ya nyumba.

Moto huo ambao haujafahamika chanzo chake, uliteketeza fedha hizo licha ya udhibiti wa chumba ambacho fedha hizo zilikuwa zimehifadhiwa.

Wake wanne wa mfanyabiashara huyo walikuwa hawaingii katika chumba hicho na pia kulikuwa na milango minne ya chuma.

Tukio la Masunga ni mfano tu wa wananchi wengi ambao  hawajawahi na wala hawana mpango wa kutumia benki kuhifadhi fedha zao na badala yake wanaona  mahali salama ni majumbani mwao.

Ziko taarifa kuwa  watu wengine hutunza fedha zao kwenye vibubu, mitungi, mashimo, nk. ilimradi tu wasiende benki.

Pamoja na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kueleza kuwa ni kinyume na sheria kuhifadhi kiasi kikubwa cha fedha nyumbani kwa sababu ni kukwamisha mzunguko wake, ni Watanzania wachache wenye elimu na wanaofahamu faida za kuhifadhi fedha benki.

Meneja wa Idara ya Uchumi ya BoT Kanda ya Ziwa James Machemba alisema kuwa kisheria fedha zote zinapaswa kuhifadhiwa kwenye taasisi za fedha ili zirejee kwenye mzunguko na hivyo kusisimua uchumi.

Ni bahati mbaya kwamba tukio hilo limetokea katika kipindi ambacho  huduma za kuhifadhi fedha zinazidi kupanuliwa nchini kukiwa na benki na taasisi za fedha zikizidi kupanuliwa kukiwa  na benki na taasisi  za fedha  zaidi ya 50 na huduma zake kusambaa mikoa yote kulingana na mahitaji.

Huduma za kifedha

Vilevile limetokea katika kipindi ambacho kuna mitandao ya simu inayotoa huduma za kifedha  kila kona ya nchi na hivyo kuweka, kuhamisha na kufanya malipo bila kwenda benki kusimama foleni.

Kinachotushangaza ni kuwa wakati mazingira ya upatikanaji wa huduma za kifedha yakizidi kuwa bora nchini, bado tunakutana na matukio kama haya ya kupoteza mamilioni ya fedha katika majanga ya moto, mafuriko na ujambazi.

Hii ni kutokana na watu wengi kutofikiwa na elimu ya utunzaji fedha ambayo tunaamini inasaidia usalama wa fedha  na mambo mengine.

Huu  ni wakati murua wa elimu hiyo kuanza kutolewa na Benki Kuu na vyombo vingine vya fedha ili kuhakikisha Watanzania wengi wanatambua  umuhimu wa kuhifadhi fedha katika benki.

Vilevile Serikali inatakiwa kuondoa vikwazo kwa wananchi kutunza fedha benki zikiwamo gharama  kubwa za tozo na kodi ambazo watu wengi huamini kuwa zinapunguza fedha zao na pia taasisi za fedha zilipe riba  inayotokana na fedha zinazowekwa kuzunguka kibiashara.

Ili kuondokana na tatizo hili moja kwa moja, ni wakati elimu ya matumizi ya benki na taasisi za fedha kuingizwa kwenye mitalaa ya elimu ili watoto wetu wakue wakijua umuhimu wa kuhifadhi fedha benki.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.