http://www.swahilihub.com/image/view/-/4842144/medRes/2164063/-/14b0idqz/-/nywamaji.jpg

 

Faida za kunywa maji unapoamka

Maji

Mtu akinywa maji. Picha/MAKTABA 

Na MARGARET MAINA

Imepakiwa - Thursday, November 8  2018 at  10:19

Kwa Muhtasari

Iwapo mwili wako haupati maji ya kutosha, hali hii inaweza kusababisha madhara mbalimbali kama vile magonjwa ya shinikizo la damu, saratani pamoja na magonjwa ya figo.

 

MIILI yetu inaundwa na asilimia kati ya 70 na 75 ya maji.

Ni muhimu kunywa maji ya kutosha ili kuufanya mwili kufanya kazi vyema.

Iwapo mwili wako haupati maji ya kutosha, hali hii inaweza kusababisha madhara mbalimbali kama vile magonjwa ya shinikizo la damu, saratani pamoja na magonjwa ya figo.

Huondoa sumu mwilini

Unywaji wa maji mengi husaidia kuondoa sumu mwilini kwani huwezesha viungo kama vile figo kufanya kazi yake vyema. Unapokunywa maji kabla ya kula chochote asubuhi utauwezesha mwili wako pia kujenga misuli na kuzalisha seli mpya.

Husaidia kupunguza uzito

Unapoamka na kuanza kutumia vinywaji kama vile soda na juisi, vinakuweka katika hatari kwa sababu vitachangia sana kuongeza uzito wako wa mwili. Hivyo basi, ni vyema kunywa maji zaidi kuliko vinywaji vingine.

Huondoa kiungulia

Kunywa maji kutakusaidia kupunguza asidi inayopatikana tumboni ambayo husababisha tatizo la kiungulia. unywaji wa maji utarahisisha mchakato wa umeng’enywaji wa chakula.

Huboresha na kuimarisha ngozi

Utafiti unaonyesha kuwa kunywa maji kunarahisisha mzunguko mzuri wa damu katika ngozi. Hivyo basi, hili husababisha kuondoa sumu mbalimbali katika ngozi na kuiacha ngozi yako katika hali nzuri kiafya.

Huhamasisha ukuaji wa nywele bora zenye afya

Upungufu wa maji mwilini una madhara makubwa sana kwa afya yako. Utafiti unaonyesha kutokunywa maji yakutosha kutakufanya kuwa na ukuaji duni wa nywele; pia kutafanya nywele zako kuwa dhaifu.

Huzuia mawe kwenye figo (Kidney stones)

Unywaji wa maji hupunguza asidi inayosababisha mawe kwenye figo. Unywaji wa maji ya kutosha kutakuepusha kwa kiasi kikubwa na matatizo ya figo.  Ili kurahisisha utendaji kazi wa figo zako pamoja na afya yake, zingatia kunywa maji ya kutosha hasa asubuhi.

Huongeza na kuimarisha kinga ya mwili

Kujijenga kwa kinga mwili hutegemea sana maji katika mwili wako. Hivyo, ni vyema kuhakikisha unaongeza kinga ya mwili wako kwa kunywa maji ya kutosha hasa kabla ya kula kitu chochote.