http://www.swahilihub.com/image/view/-/4608210/medRes/2006099/-/7701jxz/-/limau.jpg

 

Limau ni muhimu kwa urembo na kuboresha mwonekano

Limau

Limau (Wingi ni malimau). Picha/MAKTABA 

Na MARGARET MAINA

Imepakiwa - Tuesday, June 12  2018 at  12:47

Kwa Muhtasari

Limau ni tunda ambalo kwa kawaida huwa dogo lenye ladha ya uchachu.

 

LIMAU ni tunda ambalo limesheheni vitamini C na kwa kawaida huwa dogo lenye ladha ya uchachu.

Kiwango cha juisi ya limau moja kinaweza kutosha kwa mahitaji ya vitamini C katika mwili wako kwa siku nzima.

Kuwepo kiwango kikubwa cha vitamini B kunasaidia kuzuia matatizo ya moyo na mishipa ya damu, husaidia kutuliza kiwango cha sukari mwilini na pia husaidia utulivu kiakili. Malimau huwa na madini kama phosphorus, iron, na magnesium ambayo ni muhimu kwa mwili wa binadamu.

Malimau husaidia kujenga kinga ya miili.

Kando na kuimarisha vitamini na madini katika mwili, malimau pia yanatumiwa kwa urembo.

Zifuatazo ni mbinu chache ambazo unaweza ukatumia ili kuimarisha mwonekano wako:

Kusafisha ‘makeup’ usoni

Kamua kipande nusu cha limau, chukua kipande cha pamba au kitambaa safi cha pamba kisha tosa kwenye maji ya limau na kisha kitumie kusafisha uso wako.

Hapo utakuwa umesafisha na kuongeza vitamini C katika uso wako; chunga isiingie machoni.

Safisha kwa maji mengi endapo itaingia machoni.

Kutoa alama za kuungua kwa jua na madoa meusi

Chukua kiasi kidogo cha mlozi (ground almonds), ongeza ute wa yai na nusu kijiko cha chai ya limau na uchanganye.

Paka usoni mchanganyiko huo na uache kwa muda wa dakika 20 kabla ya kuosha.

Husaidia ngozi ambazo ni kavu (ambazo hazina mafuta na huparara)

Changanya vijiko vitatu vya chai ya limau, vijiko vitatu vya chai ya asali na kijiko kimoja cha kabichi (iliochemshwa na kusagwa).

Paka usoni na shingoni kisha subiri kwa dakika 10 halafu osha kwa kutumia maji baridi.

Kufanya hivi kunasaidia kulainisha ngozi yako ya jamala.

Husaidia ngozi zenye mafuta

Changanya nusu kijiko cha chai ya mkandaa, vijiko viwili vya limau na vijiko vitatu vya papai iliyosagwa. Paka kisha kwa ngozi subiri kwa muda wa dakika 20 kisha osha.

Hatua hii itasaidia kupunguza mafuta usoni na pia kupunguza chunusi.

Kusafisha meno na kuondoa harufu mbaya ya kinywa

Chukua limau iliyo kwenye glasi iliyojaa nusu na utie chumvi kidogo na baking soda kidogo sana. Tumia kusugulia meno.

Husaidia nywele kutokatika

Kamua limau zima na changanya vijiko kati ya 3-5 vya mafuta ya nazi.

Paka kichwani kisa acha kwa muda wa saa moja kisha osha. Fanya hivi angalau mara moja kwa wiki.

Huzuia mba (Mba ni ugonjwa wa ngozi unaosababisha kuwepo kwa mabaka mwilini)

Changanya juisi ya limau moja na yai moja. Paka kichwani, acha kwa muda wa saa moja kisha osha. Fanya hivi aghalabu kwa mwezi mmoja.

Kung'arisha nywele

Baada ya kuosha nywele, tia juisi ya malimau kwenye nywele bila kuosha tena.

Kulainisha midomo iliyokauka

Changanya mafuta (cream) kijiko kimoja, juisi ya malimau na asali. Sugulia taratibu kwenye midomo mpaka pale unapopata nafuu.

Hung'arisha ngozi

Changanya kiwango sawa kwa sawa cha nyanya iliosagwa, malimau na maziwa.

Paka kwa muda wa dakika 10-15 kisha osha. Fanya hivi mara kwa mara.

Huchunga ngozi dhidi ya mikunjo

Changanya kijiko kimoja cha asali, kijiko kimoja cha limau na vijiko viwili vya mafuta ya mlozi (almond) au mafuta ya zaituni (olive). Kisha paka kwenye ngozi; acha kwa muda wa dakika 20 kisha osha. Fanya hivi mara moja kwa siku.