http://www.swahilihub.com/image/view/-/4269396/medRes/1862282/-/ub088x/-/somadini.jpg

 

Falsafa na maana ya elimu katika Uislamu

Dini

Mwislamu raia wa Yemen akisoma Kurani. Picha/MAKTABA 

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Friday, December 28  2018 at  10:36

Kwa Muhtasari

Elimu ni msingi wa maisha bora.

 

ELIMU ni utambulisho muhimu wa dini ya Uislamu tangu mwanzo wake. Kutokana na nafasi ya Qur’an kwa Waislamu kama ufunuo na neno la Mwenyezi Mungu, Waislamu wamelazimika kuisaka elimu kama wajibu wao mkuu kidini kabla ya matendo ya ibada.

Hii ni kwa sababu katika Uislamu elimu hutangulia matendo na matendo bila elimu hayakubaliwi na Mwenyezi Mungu. Kwa kulitambua hili, ndiyo maana tangu mwanzo wa Uislamu, Waislamu walisifika kwa sifa ya elimu.

Msukumo mkubwa wa Waislamu kutafuta elimu ulitokana na mahitaji ya elimu katika utekelezaji wa mafundisho mbalimbali ya Uislamu. Kwa mfano, ili kufanya ibada ya swala inambidi Musilamu kujua uelekeo wa Qibla (Makka) hivyo elimu ya Jiografia ikawa jambo muhimu kwa Waislamu.

Hivyo hivyo ili kugawa mirathi na kujua kiasi cha zaka za aina mbalimbali, ilibidi kujua elimu ya Hisabati.

Kwa namna hii, ndiyo maana hivi leo miongoni magwiji na wavumbuzi wa fani mbalimbali za elimu kama vile Jiografia, Hisabati, tiba, anga za juu, kemia, mwanga, uvumbuzi wa saa na kadhalika walikuwa Waislamu.

Hapa utawakuta kina Al-Zahrawi (ajulikanae nchi za Magharibu kama Abulcasis) aliyevumbua zana mbalimbali za kufanyia upasuaji, Ibn Finas aliyemtangulia Mtaliano Leonardo da Vinci kwa karne sita kama mtu wa kwanza kujaribu kuruka angani.

Wako pia kina Al-Kindi bingwa wa fani za madawa (Ufamasia), Kemia, anga za juu, Hisabati na Jiografia wakiitwa mabingwa wa fani nyingi kama alivyokuwa Ibn Al-haytham mvumbuzi wa kamera, Al-Jazari mvumbuzi wa saa na Al-Khwarizmi gwiji la Hisabati. Hata jina la aina fulani ya Hisabati ijulikanayo kama Logarith au Aligorithm ni kutokana na Al-Khwarizmi.

Nafahamu si wasomaji wengi wanaojua kwamba chuo kikuu cha kwanza duniani kinachotambuliwa na wasomi wa kweli ni kile kiitwacho Al-Qarween huko Fez nchini Morocco ambacho kiliasisiwa na mwanamke Muislamu aitwaye Fatima Al-Fihriyya mnamo mwaka 859 AD kama mali ya Wakfu.

Chuo hiki kinafuatiwa na Chuo Kikuu cha Bologna nchini Italia mwaka 1088 AD ambacho ndicho chuo kikuu cha kwanza barani Ulaya. Kwa maneno mengine, Waislamu ndio waliokuwa wa kwanza kuanzisha vyuo vikuu na hata hospitali kama tuzijuavyo leo.

Ni kwa nini hali hii?

Hali hii ya Waislamu wajuao Uislamu kuipa elimu nafasi ya kwanza katika maisha yao ni kutokana na kujua kwamba elimu ndilo jambo la kwanza alilopewa Adam (Qur’an 2:31) na pia ndiyo amri ya kwanza kuteremshwa katika aya za kwanza za Qur’an (96:1-5).

Lakini pia ni kutokana na ukweli kwamba lengo la elimu katika Uislamu ni kumwezesha mwanadamu kuliendea na kulifikia lengo la kuumbwa kwake, ambalo kama tulivyooona ni kumwabudu Mwenyezi Mungu kama Khalifa wake katika ardhi.

Pamoja na Mtume Muhammad (rehma na amani ziwe juu yake) kusema: “kutafuta elimu ni wajibu kwa kila Muislamu” (Imepokewa na Muslim), kukosa elimu ya dini na dunia na kuwa nyuma kimaendeleo ya kidunia, vimekuwa kama alama ya Uislamu ingawa hali inaanza kubadilika hivi sasa.

Falsafa ya elimu katika Uislamu inaeleza kuwa lengo la elimu ni kumpa mwanadamu nyenzo ya kumfanya amtambue Muumba wake, ajue jinsi ya kumwabudu, aweze kutumia neema zilizowekwa na Muumba katika ulimwengu na aweze kuhusiana na wanadamu wenzake kwa wema, hekima na amani.

Matokeo yake, elimu huwafanya Waislamu kukua kimaarifa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na hata kisiasa, kwa kutumia uwezo wa akili kuelewa na kuhoji mambo yanayomzunguka. Kwa kulitambua hili, Muislamu atahakikisha anasoma na kuijua dini yake angalau kwa kiwango cha utekelezaji binafsi wa ibada na mafundisho mbalimbali. Lakini pia katika masomo ya kusomwa na Muislamu yatakuweko yale ya sayansi ya asili, sayansi ya jamii na lugha mbalimbali, huku Kiarabu kikipewa kipaumbele.

Changamoto kubwa na muhimu kwa Waislamu zama hizi ni kuwa na mfumo wa elimu ambao utazalisha wasomi wenye kuijua vema Qur’an na fani mbalimbali za Uislamu lakini bila kuweka kando maarifa ya kidunia.

Hakuna njia ya mkato ya kuikabili changamoto hii isipokuwa ni kuitafuta elimu kama ibada kubwa kabisa itakayofanya ibada nyingine ziweze kufanyika ipasavyo na ili kumwezesha Muislamu kuendana na ulimwengu wa leo.

Pamoja na kujifaharisha kwa mchango mkubwa wa Waislamu walioutoa katika maendeleo ya ulimwengu kisayansi na kiteknolojia, Waislamu hawawezi kuendana na ulimwengu wa leo kwa kutazama mafanikio ya babu zao.

Juhudi

Siku zote hawezi kuendelea yule anayeishi kwa kujivunia historia yake huku hafanyi juhudi kuiinua hali yake ya sasa.

Elimu ni nini katika Uislamu?

Maarifa ayapatayo mwanadamu ama hupewa na Mwenyezi Mungu (wahyi au ufunuo) au huyapata kwa kujifunza mwenyewe au kufundishwa na wengine. Mchakato wa mwanadamu kujipatia maarifa ndiyo huitwa elimu.

Elimu katika Uislamu ni mchakato wa kujifunza, kufundisha na kupokea maarifa mbalimbali. Kwa kuwa elimu ni mchakato wa maarifa, falsafa ya elimu katika Uislamu itategemea mtazamo mzima kuhusu maarifa katika Uislamu.