http://www.swahilihub.com/image/view/-/3413070/medRes/1458364/-/sr976u/-/wasichana.jpg

 

Familia ziwajibike kumlinda mtoto wa kike

Siku ya Msichana Duniani

Baadhi ya wasichana wa shule na watetezi wa haki za mtoto wa kike waadhimisha Siku ya Msichana Duniani eneo la Freedom Corner, Nairobi Oktoba 11, 2016. Picha/WANDERI KAMAU 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, October 12  2017 at  09:18

Kwa Mukhtasari

Jumatano Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo hapa nchini iliadhimishwa wilayani Tarime, Mkoa wa Mara.

 

JUMATANO Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ambayo hapa nchini iliadhimishwa wilayani Tarime, Mkoa wa Mara.

Siku hiyo ni mahsusi katika kuhamasisha utatuaji changamoto zinazowakabili watoto wa kike ikiwamo kilinda haki zao na kuwawezesha kufikia malengo yao.

Siku hiyo ilipitishwa rasmi na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Desemba 2011.

Hapa nchini Serikali na asasi mbalimbali hufanya matamasha kielimisha jamii namna ya kulinda haki za watoto wa kike hasa umuhimu wa kupata elimu.

Tunafahamu Tanzania yenye makabila zaidi ya 120 kila moja ina mila na desturi zake kuhusu malezi hasa kwa mtoto wa kike lakini tangu tupate uhuru bado mtoto huyo ameendelea kukabiliana na changamoto lukuki hasa vitendo vya ukatili.

Kuna baadhi ya maeneo ya Tanzania ambayo bado yanaamini mila za kukeketa, kitendo ambacho kimefanya wale wasiopenda vitendo hivyo kuishi kwa wasiwasi na wengine kufikia hatua ya kutoroka nyumbani.

Vitendo vya ukeketaji vimekuwa chanzo cha tatizo la afya ya uzazi kwa mama na mtoto.

Kwa mfano mikoa ya Manyara, Mara, Dodoma Arusha na Singida wasichana muda wowote wana wasiwasi wa kukeketwa kwa kuwa kitendo hicho kimekuwa sehemu ya utamaduni katika jamii nyingi za huko.

Siku hii pia inaadhimshwa wakati mtoto wa kike akiwa anakabiliwa na mimba na ndoa za utotoni.

Wasichana wengi wanashindwa kumaliza elmu ya msingi ama kwa kupata ujauzito usiotarajiwa au kuolewa katika umri mdogo kutokana na shinikizo la wazazi.Tunafahanu juhudi za Serikali ikiwamo kuweka sheria kali katika kumlinda mtoto wa kike lakini utafiti unaoyesha kuwa takriban nusu ya wasichana wenye umri wa miaka 15 – 19 mkoani Katavi ni wazazi na robo yao walipata mimba za utotoni.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba watoto waliopewa mimba katika umri mdogo hukatisha masomo na ndoto zao huzimika.

Watoto hawa wanakwenda mitaani kuongeza jamii ya kinamama wenye elimu ndogo na ambayo hupata wakati mgumu kujikwamua kiuchumi.

Tanaamini wa haki za watoto wa kike kwa sehemu kubwa unaanzia kwenye famiia.

Kama jukumu la kumlinda na kumwendeleza mtoto wa kike litaanzia kwenye familia pengine changamoto hizo zingepungua.

Hata hivyo kinachoonekana pale mtoto wa kike anapopata tatizo la kufanyiwa ukatili wa aina yoyote, baadhi ya familia zimekuwa zikishirikiana na watuhumiwa kuficha uhalifu huo kwa ahadi ya malipo.

Kesi nyingi zimeshindwa kufunguliwa katika vyombo vya sheria au kuendelea kusikiizwa mahakamani kwa kuwa upande mmoja umeshindwa kutoa ushirikiano.

Pamoja na kwamba elimu inaendelea kutolewa juu ya kumlinda mtoto wa kike lazima ifahamike kuwa asasi za kiraia, polisi na Serikali kwa jumla hawataweza kufahamu ukatili unaofanywa dhidi ya watoto wa kike kama famila au majirani wameshindwa kuripoti matukio haya.

Tunawasihi wazazi, walezi, wanajamii wote na Serikali kwa jumla kuwajibika katika kulinda haki za watoto wa kike kwa kuhakikisha anasoma vyema, analindwa dhidi ya mila kandamizi za ndoa za utotoni, ukeketaji na utatili mwingine kama vipigo na kazi lukuki.

Waovu wote wafichuliwe na Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wote wanaohusika ili kutengeneza Tanzania salama yenye fursa sawa za kimaendeleo kwa watoto wote.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au 0754780647