http://www.swahilihub.com/image/view/-/4335936/medRes/1904922/-/hh6xgf/-/naswada.jpg

 

'Handshake' itumiwe kusaka mbinu za kupunguza gharama ya mishahara

Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga Machi 9, 2018 katika Harambee House, Nairobi. Picha/JEFF ANGOTE 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  13:21

Kwa Muhtasari

Ni bayana kuwa taifa la Kenya kwa sasa linapitia mahangaiko makuu ya kiuchumi na ambapo linaonywa kuwa kando na masuala mengine ya dharura, linahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu gharama ya mishahara ambayo imefika Sh630 bilioni kwa mwaka hivyo basi kunyima wananchi ufadhili wa kimaendeleo.

 

NI wazi kuwa taifa la Kenya kwa sasa linapitia mahangaiko makuu ya kiuchumi na ambapo linaonywa kuwa kando na masuala mengine ya dharura, linahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu  gharama ya mishahara ambayo imefika Sh630 bilioni kwa mwaka hivyo basi kunyima wananchi ufadhili wa kimaendeleo.

Shida hiyo ilianza kuandama taifa hili miaka ya 90 ambapo serikali ya mzee Daniel Moi ilitumia ajira kama hongo ya kisiasa kwa jamii na makundi ili kujiimarishia ufuasi na uthabiti.

Serikali hiyo ilitumia ajira kama njia moja ya kujikinga dhidi ya mipigo ya upinzani ambapo kulikuwa na msukumo wa kuimarishwa kwa demokrasia na vyama vingi vya kisiasa viidhinishwe.

Kufikia mwaka wa 2002 ambapo serikali ya upinzani katika mrengo wa Narc ilitwaa mamlaka ya utawala, hali ya gharama ya mishahara ilikuwa imepanda kiasi cha kutatiza hazina za kimaendeleo.

Ni katika mustakabali huo ambapo serikali ya rais Mwai Kibaki ilitoa ilani ya kupunguza gharama hiyo kupitia kwa ujumbe spesheli (OP. AB.39/4A(20) iliyotiwa sahihi na aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Bw Francis Muthaura.

Bw Muthaura alipendekeza idara zote za serikali zijiandae kwa ustaafishaji ambao ulilenga kupunguza gharama ya mishahara hadi asilimia 7.2 ya pato la kitaifa.

Lengo lilikuwa kuwatimua wafanyakazi 21, 338 huku ikizindua uchunguzi dhidi ya wafanyakazi bandia na pia kupiga marufuku usajili wa wafanyakazi wapya serikalini.

Hata hivyo, wadau wa kisiasa walipinga hatua hiyo kama iliyokuwa na uwezo wa kusambaratisha serjikali na badala yake, serikali ikaongeza utozaji ushuru na kisha kuanza kuongeza wafanyakazi hao mishahara baada ya kuandamwa na migomo mikali.

Katika mtazamo huo ambapo serikali imepanuka maradufu kupitia katiba mpya, sio suala la kujadiliwa kuwa taifa hili linahitaji kupata mbinu ya kupunguza gharama hiyo ambayo inakadiriwa kuwa kufikia mwaka wa 2020, ikiwa hakutapatikana ufadhili mbadala wa kugharamia mishahara hiyo, basi asilimia 70 ya ushuru wa bajeti utakuwa wa kulipa mishahara hiyo.

Ni vyema Wakenya waambiwe bila kufichwa kuwa mada kuu katika siasa zinazoendeshwa za kura ya maamuzi imejificha katika kutupilia mbali baadhi ya afisi zilizoko katika Katiba mpya.

Nyadhifa hizo aidha ziko katika tume huru zilizoundwa na katiba hiyo, teuzi ambazo zimehalalishwa za kushughulikia usawa wa jinsia, kupunguza idadi ya Kaunti na pia uwezekano wa kufutilia mbali nyadhifa za wawakilishi wa wanawake bungeni na pia zile za useneta.

Kwa mujibu wa mbunge wa Ndaragwa, Jeremiah Kioni ambaye pia alikuwa mgombezi mwenza wa muungano wa Amani uliongozwa na Bw Musalia Mudavadi katika uchaguzi mkuu wa 2013, mijadala yote inayoendeshwa na wanasiasa kuhusu kura hiyo ya maamuzi inafaa kupuuziliwa mbali na badala yake Wakenya wakwamilie kupunguza gharama ya mishahara.

"Magavana wanaitisha pesa zaidi katika migao ya Kaunti huku wakikataa kuwajibika kuhusu jinsi wanavyotumia pesa zao," akasema.

Aidha, Bw Kioni anasema kuwa serikali ya Jubilee imechanganyikiwa kwa kuwa inajua kwa kweli inahitaji kura ya kupunguza gharama ya mishahara, lakini haijui ianzie wapi.

"Uliona Rais Kenyatta akiongoza maafisa wake wakuu serikalini katika harakati za kujipunguzia mishahara ili kuhepa bili kubwa inayowatatiza kuendesha serikali. Hiyo ni ishara tosha kuwa Rais anajua wazi umuhimu wa kura hiyo, lakini hajui aanzie wapi," akasema.

Ukweli wa mambo ni kwamba, wakati wa kampeni za kuidhinisha katiba mpya, wadau wote waliafikiana kuwa ilikuwa na vipengele tata na ambavyo vilihitaji kurekebishwa kabla ya kupitishwa.

Lakini kwa kuwa Wakenya walikuwa wamechoshwa na siasa za kudai katiba mpya kila mwaka wa uchaguzi, walionelea afadhali waipitishe jinsi ilivyokuwa lakini baadaye kuwe na mjadala wa kuirekebisha.

Shida ni kwamba, mirengo yote inayoendesha kampeni za kuokoa Kenya kutokana na mtego huo wamejawa na unafiki na wanatumia harakati hizo kujiimarisha kisiasa na pia kujipa kinga dhidi ya kuandamwa katika njama zao za ufisadi.

Katika mijadala inayoendeshwa kuhusu kura hiyo, utapeli wa kimawazo unaoendeshwa kwa njia ya propaganda za kila aina zinaishia kuzua hali ya mashindano ya kisiasa ambapo mwananchi wa kawaida amebakia kuhadaiwa.

Ajabu ni kwamba, kuna wanasiasa kutoka mirengo yote ya kisiasa ambao wameafikiana hadharani kuwa kunahitajika suluhisho la gharama hiyo, lakini hali hiyo inaishia kunyamazishwa na mchecheto wa hisia za malumbano.

Kiranja wa mrengo wa Nasa bungeni Bw John Mbadi tayari ametoa kauli yake kwamba serikali ambayo inatawala kwa sasa iko na miundo pana sana na ambayo imeletwa na katiba mpya.

"Katiba tuliyo nayo kwa sasa iliunda nyadhifa nyingi za kikatiba na ambazo zimepewa uhuru wa kujiwekea viwango vya mishahara. Ni wazi kuwa hatuwezi tukamudu gharama hiyo kwa muda mrefu na athari za kuikwamilia zinaweza hata kupindua serikali kupitia migomo ya mishahara," anasema.

Anasema kuwa lengo la mrengo wa Nasa la kuitisha mjadala wa kitaifa lilikuwa ni la kutafuta mwelekeo wa kutambua tishio loa mishahara lakini serikali ya Rais Uhuru Kenyatta ikakataa mwito huo.

"Sisi hatukuwa na njama fiche ila tu tulikuwa tunajaribu kutatua shida ya mishahara hiyo. Lakini Rais Kenyatta na serikali yake walitupuuzilia mbali wakitwambia kuwa tulikuwa tunataka tugaiwe serikali yake," akasema.

Umaarufu

Hata hivyo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na sheria Bw Geoffrey Kahuthu anasema kuwa wazo hilo la Nasa lilikuwa limeletwa kwa misingi ya siasa kali za kumhadaa Mkenya, huku wandani wake wakikijitafutia umaarufu.

"Mrengo wa Cord ulikuwa umevizia serikali kwa msingi kuwa, mada yao ya kutaka mishahara ipunguzwe ilikuwa ipokelewe na Wakenya kwa moyo mkujufu huku nayo serikali ikiwa katika mtego wa kuaibika kuwa haikuwa imewaza kuhusu suala hilo," akasema.

Kutokana na siasa zilizochipuka huku mrengo wa Rais Kenyatta ukikataa katakata kuitikia mwito wa Cord wa kuandaliwa kwa mjadala wa kitaifa, taifa liligeuzwa kuwa la malumbano ya wazi yakihusisha mirengo yote ya kisiasa.

Bw Kahuthu anasema kuwa kwa sasa, kelele zote ambazo zimejaa hapa nchini kuhusu kura ya maamuzi ni bure na imepoteza imani ya Wakenya kuwa kuna haja ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.

"Kwa kuwa lengo la kupunguza  gharama ya mishahara kupitia kura ya maamuzi lilihujumiwa na kusambaratishwa na siasa za malumbano ambapo Wakenya walikuwa wamejiandaa kutupilia mbali nyadhifa zisizo na maana, haja ya kura hiyo kuandaliwa imewaponyoka Wakenya," akasema.

Msimamo huo unaungwea mkono na ripoti ya Kenya Institute of Public Policy Research and Analysis (KIPPRA) ambayo inaonyesha kuwa kuna pengo kubwa ambapo pesa za umma hupotelea kwa marupurupu.

"Wengine hulipwa asilimia 100 ya mishahara yao kama marupurupu na huwafanya kuwa na mishahara zaidi ya miwili ndani ya ajira moja," ripoti hiyo yasema

Na njia ya kipekee ya kufanya hivyo, ni kuandaa kura ya maamuzi ya kufutilia mbali afisi ambazo kufikia sasa mijadala ya wakenya imetambua kama zisizo na manufaa yoyote katika utawala.