Gharama za gesi, umeme zitalinda misitu

January Makamba

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira na Muungano) Januari Makamba nchini Tanzania, . Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, August 3  2017 at  09:36

Kwa Mukhtasari

Serikali imeamua kuzipiga marufuku baadhi ya taasisi zake zinazokusanya idadi kubwa ya watu hasa kambi za jeshi, magereza, shule hosptali na vyuo kutumia nishati ya mkaa na kuni.

 

SERIKALI imeamua kuzipiga marufuku baadhi ya taasisi zake zinazokusanya idadi kubwa ya watu hasa kambi za jeshi, magereza, shule hosptali na vyuo kutumia nishati ya mkaa na kuni.

Zuio hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Mazingira na Muungano), January Makamba kwamba wamefikia uamuzi huo baada ya kugundua Serikali ni moja wa watumiaji wakbwa wa kuni na mkaa.

Alisema hatua hiyo ni mpango wa Serikali kutaka kuondokana kabisa na matumizi ya mkaa na kuni hasa baada ya Ripoti ya Pili ya Hali ya Mazingira Nchini iliyochapishwa mwaka 2014 kubainisha kwamba hali ya mazingira si nzuri kutokana na uvunaji holela wa misitu.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam pekee unatumia tani 500,000 za mkaa kila mwaka na mahitaji hayo yanaweza kuongezeka kadri jiji linavyoweza kupanuka.

Pia taarifa ya Taifa ya ufuatiliaji wa Tathmini ya Rasilimali za Misitu kubainisha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu nchini ni kubwa sana ambapo kiasi cha hekta 372,000 au ekari takriban milioni moja za misitu zinaangamizwa kila mwaka.

Juhudi za Serikali zinapaswa kuungwa mkono kwa sababu uharibifu wa mazingira una madhara makubwa kwa maisha ya wanadamu lakini suala hilo litawezekana iwapo nishati mbadala iliyokusudiwa itapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu.
Matumizi ya nishati madala yanayotajwa kila mara yatawezekana iwapo nguvu ya Serikali itawezekana kama vikundi vya wanawake wanaouzunguka mgodi wa makaa ya mawe ya Ngaka iliyopo Kata ya Ruanda wilayani Mbinga, kutengeneza vitofali vya kupikia vya makaa ya mawe.

Hivyo kama Serikali imeamua kwa dhati kuokoa misitu, haina budi kuwekeza katika uzalishaji mkubwa wa makaa ya mawe ili wananchi wa kawaida waweze kuyapata kwa urahisi.

Tunaomba Serikali iweke nguvu kwenye matumizi ya nyumbani ya makaa ya mawe kwa kukaribisha wawekezaji wa ndani katika sekta hiyo ili Watanzania wa kipato cha chini wawe na uwezo wa kuyatumia.

Pia matumizi ya pumba kama nishati mbadala ya kupikia majumbani yanaweza kuenezwa katika maeneo mengi ya nchi na hili litawezekkana iwapo teknolojia ya majiko ya kutumia pumba itafikishwa katika maeneo yote ya vijijini.

Tunaamini nishati ya gesi inayozungumzwa sana na Serikali itaweza kuwafikia wananchi kama inayochimbwa nchini itazalishwa kwa kiwango kikubwa na kusambazwa kote nchini.

Kwa kuongeza uzalishaji wa gesi yetu kutapunguza hata bei ya gesi inayoingizwa hapa nchini na wafanyabiashara ambayo bei yake haimwezeshi mwananch wa kipato cha kawaida kutamani kuitumia.

Pamoja na juhudi za kuongeza matumizi ya umeme lakini yanaishia katika kuwasha taa, redio na runinga. Suala la kutumia umeme kupikia limekuwa la nadra sana kutokana na gharama kubwa.

Hata hivyo tunaamini gharama nafuu za nishhati mbadala na upatikanaji wake wa uhakika utapunguza utegemezi wa nishati ya kuni na mkaa hali itakayosaidia kutunza na kulinda misitu.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.