http://www.swahilihub.com/image/view/-/2758636/medRes/1040993/-/hpl66o/-/nyonyesha.jpg

 

Haki ya mtoto ilindwe, utaratibu ufuatwe

Mwanamke amnyonyesha mtoto

Mwanamke amnyonyesha mtoto. Picha/MAKTABA 

Na MHARIRI - MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, April 12  2018 at  09:50

Kwa Muhtasari

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Dkt Faustune Ndugulile amekemea udhalilishaji wa watoto kwa watu wenye malalamiko ya kutelekezwa na wazazi wenzao yanayowasilishwa na watu kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Tanzania.

 

KATIKA toleo la Jumatano la gazeti la Mwananchi kulikuwa na habari iliyonukuu Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee Dkt Faustune Ndugulile akikemea udhalilishaji wa watoto kwa watu wenye malalamiko ya kutelekezwa na wazazi wenzao yanayowasilishwa na watu kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Pia Dkt Ndugulile alisema ni muhimu utaratibu wa kusikiliza malalamiko ya kijamii ambayo kiutaratibu husikilizwa faragha na kwa kufuata mifumo sahihi. Dkt Ndugulile hakuishia hapo. Pia alitoa rai kwa wananchi wote wenye malalamiko kufuata taasisi zinazohusika kwa ajili ya kutatua migogoro inayohusu wenza waliotofautiana. Tunakubaliana na alichotukumbusha Dkt Ndugulile kuhusu haki za mtoto; kwamba kila mmoja wetu anapaswa kuzilinda hivyo kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kuwaonyesha hadharani watoto waliofuatana na wazazi wao hakikubaliki sheria.

Hata kitendo cha baadhi ya vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii  kuchukua picha  za watoto hao na kuwaonyesha hadharani  si cha kimaadili  na hakikubaliki kisheria. 

Pia kitendo cha walalamikaji kuwatuhumu hadharani wanaowalalamikia ni ukiukwaji wa utaratibu  wa namna ya kutatua matatizo katika jamii.

Tunaamini dhamira ya Mkuu wa Mkoa ni njema na imelenga   kuwasaidia wanawake wenye matatizo katika jamii ambao ni wengi. Hata hivyo kwa mtazamo wa wengi dhamira hiyo njema imeonekana kugeuka kama nia ya kukomoana na kuaibishana  vinavyojionyesha kwa namna walalamikaji wanavyotoa tuhuma nzito hadharani kwa wenza wao lakini ni namna Mkuu wa Mkoa alivyotoka hadharani na idadi ya  wabunge na viongozi wa dini akidai anavyowatelekeza wanawake waliozaa nao jambo ambalo haikutakiwa kufanyika kwa kuwa bado ni tuhuma na zinaelekezwa kwa watu kutoka kwa taasisi na vyombo vyenye heshima.

Pia, Mkuu wa Mkoa ngeufanya mchakato huo  kwa njia ya faragha na kuwazuia alioenda kupeleka tuhuma dhidi ya wenzao kuzungumza nje ya eneo lililokusudiwa ili kuepuka watu kutochafuana.

  Umati wa watu wa walalamkaji uliojazana kwemye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa tangu  Jumatatu ni kielelezo kwamba tatizo ni kubwa na kuna haja ya taasisi husika kutathmini kama kweli una ufanisi.

Serikali kupitia Wizara ya Afya ina kitengo cha ustawi wa jamii ambacho kazi yake kubwa ni kushughulikia migogoro ya ndoa na haki za watoto lakini kwenye vituo vya polisi kuna dawati la jinsia.  

Hatuwezi kuwahukumu ustawi wa jamii wala dawati la jinsia la polisi lakini wanapaswa kujiangalia upya wapi kuna kasoro ili wazirekebishe  kwa lengo la kuboresha  utendaji wao.

Tunaamini tatizo hili lipo maeneo yote nchini, hivyo rai yetu kwa wakuu wa mikoa  mingine kutoa  elimu ya kutosha kwa wananchi wao kuhusu njia za kutatua matatizo ya mafunzo ya watoto, ndoa na mengine kwa kutumia vyombo vilivyowekwa kisheria ili kuepuka athari zanazoweza kusababishwa na kuwekwa hadharani kwa matatizo yao.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647