http://www.swahilihub.com/image/view/-/4207142/medRes/1822882/-/omusu5z/-/maruto.jpg

 

Hatua ya Kenya ni mwanzo mzuri wa ushirikiano

Uhuru na Ruto

Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wa Rais William Ruto waonesha vyeti vyao wakiwa na Mama wa Taifa Margaret Kenyatta na Rachel Ruto baada ya kiongozi wa nchi na naibu wake kuapishwa Novemba 28, 2017 uwanjani Kasarani. Picha/JEFF ANGOTE 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  08:42

Kwa Mukhtasari

Rais Uhuru Kenyatta alifungua milango kwa raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akisema sasa wanaweza kuingia Kenya, kufanya biashara, kumiliki mali na kufanya shughuli nyingine za maendeleo kwa kutumia vitambulisho bila kubaguliwa.

 

JUZI Rais Uhuru Kenyatta alifungua milango kwa raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) akisema sasa wanaweza kuingia Kenya, kufanya biashara, kumiliki mali na kufanya shughuli nyingine za maendeleo kwa kutumia vitambulisho bila kubaguliwa.

Rais Kenyatta alisema hayo katika hotuba aliyoitoa baada ya kuapishwa kwenye Uwanja wa Karasani jijini Nairobi.

Hatua hiyo imeonyesha dhamira ya Serikali kuwahudumia raia wa nchi za EAC kama wanavyohudumiwa raia wa Kenya kwa mujibu wa sheria.

Alisisitiza umuhimu wa uhusiano mwema wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kufanya kazi na viongozi wenzake wa Jumuiya hiyo kwa kuweka nguvu mpya na matumaini kwa umoja huo ikiwa ni pamoja na kuleta amani na ustawi wa jamii ambao wananchi wa nchi zote wanaulilia.

Tunaamini hatua iliyochukuliwa na Rais Kenyatta ya kuruhusu wananchi wa nchi wa Afrika Mashariki kuingia Kenya kwa vitambulisho ni kubwa kwa kuwa nchi nyingi hasa za Afrika zikiwamo za jumuiya za kikanda zimekuwa zikiondoa vikwazo vya kusafiri na uwekezaji.

Kwa mfano Ushelisheli imeruhusu nchi za Afrika kuingia bila visa na utaratibu huo umewezesha kuongeza mapato ya Taifa.

Mwaka 2013, Rwanda nayo ilipunguza vikwazo vya viza kwa nchi za Afrika na hasa kwa raia wa nchi za Afrika Mashariki.

Wanaokwenda Rwanda wanapata visa baada ya kuwasili nchini na utaratibu huo unaiwezesha nchi hiyo kuongeza idadi ya watalii, kuongeza shughuli za biashara, kuvuta wawekezaji na kuongeza ajira.

Utaratibu huu wa kuondoa vikwazo vya kusafiri pia uko kwenye nchi nyingi za Afrika zikiwamo za kikanda.

Tunaamini   hatua ya Rais Kenyatta ni mwendelezo mzuri katika jitihada zinazofanywa na Jumuiya za kikanda za kuwaondolea wananchi wake na ni ukweli usiopingika kuwa sasa kuna mwingiliano wa kifamilia katika nchi za Afrika na hata nje ya bara hili.

Mbali na uhuru alioutoa kwa nchi za EAC, kiongozi huyo pia amefungua milango kwa raia wengine wa Afrika walio nje ya EAC kwamba sasa watapata viza katika kituo watakaotumia kuingia nchini Kenya tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Umoja

Kimsingi tunakubaliana na Rais Kenyatta kwamba uhuru wa watu kwenda popote umekuwa ndio msingi mkuu wa udugu na umoja wa Waafrika na kwamba dunia ya sasa imejielekeza katika kufungua milango ya kiuchumi kwa kushirikiana na wengine.

Mwezi ujao viongozi wataridhia uamuzi wa kuunda eneo huru la biashara la utatu wa Comesa, EAC na SADC baada ya safari ndefu ya kuanzisha eneo hili iliyoanza Oktoba 2008. Uamuzi huo utawezesha wafanyabiashara wa nchi hizo kufanya biashara kwa urahisi. Pia uamuzi huo utarahisisha uandaaji wa programu za pamoja zitakazochangia kuleta maendeleo ya viwanda, kuratibu na kuwianisha mipango kabambe ya uendelezaji wa miundombinu ya kikanda uchukuzi, mipango kabambe ya nishati  na kuharakisha uanzishwaji wa  miradi ya pamoja katika nyanja a kiteknolojia ya mawasiliano (Tehama) na kubuni taratibu za pamoja  za kugharimia uendelezaji wa miundombinu.

Tunaamini kilichofanywa na Rais Kenyatta kitawasaidia wadau kwenye utatu wa COMESA, EAC na SADC  na pia ni mwanzo mzuri wa nchi nyingine katiKa jumuiya za kikanda kuiga mfano huo wa kurahisisha zaidi ushirikiano wa wananchi wao kwa kuwaondolea vikwazo visivyo vya lazima ilimradi sheria zinafuatwa.