http://www.swahilihub.com/image/view/-/3967920/medRes/1669486/-/psi9j3z/-/kil.jpg

 

Hili la madini ni funzo kwa Bunge letu

Nehemiah Osoro

Mwenyekiti wa Kamati ya Madini Profesa Nehemiah Osoro (aliyesimama) akifuatiwa na Spika wa Bunge Job Ndugai, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na baadaye Rais Magufuli. Picha/MWANANCHI 

Na MHARIRI – MWANANCHI

Imepakiwa - Wednesday, June 14  2017 at  11:04

Kwa Mukhtasari

Juzi Kamati ya pili ya Rais iliyokuwa ikichunguza masuala ya  kiuchumi na kisheria kuhusu mchanga wa madini uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi yakiwamo makontena 277 yaliyozuiliwa na Serikali bandarini imebainisha dosari kadhaa katika Sheria ya Madini na mikataba iliyoingiwa kwa ajili ya kuchimba rasilimali hiyo na kutoa mapendekezo kadhaa.

 

JUZI Kamati ya pili ya Rais iliyokuwa ikichunguza masuala ya  kiuchumi na kisheria kuhusu mchanga wa madini uliokuwa unasafirishwa nje ya nchi yakiwamo makontena 277 yaliyozuiliwa na Serikali bandarini imebainisha dosari kadhaa katika Sheria ya Madini na mikataba iliyoingiwa kwa ajili ya kuchimba rasilimali hiyo na kutoa mapendekezo kadhaa.

Moja ya mapendekezo hayo 21 ambayo yote yalikubaliwa na Rais John Magufuli inataka sheria itamke bayana kuwa mikataba yote ya uchimbaji mkubwa wa madini isiwe siri na lazima iridhiwe na Bunge kabla ya kuanza kutekelezwa.

Madai ya uwazi katika mikataba hiyo yamekuwa na muda mrefu ambayo yamewafanya baadhi ya wabunge ama kuchukuliwa hatua za kinidhamu au baadhi ya vikao wakati wa upitishwaji wa sheria.

Machi 1997 Bunge lilipitisha sheria mbili kwa mpigo kwa hati ya dharura. Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali za fedha ya 1997 na Sheria ya Uwekezaji Tanzania 1997.

Hata hivyo, Sheria ya Marekebisho mbalimbali za fedha ya 1997 ilipingwa vikali kwa maelezo kuwa itafuta au itapunguza kiasi kikubwa cha kodi kinachostahili kulipwa na kampuni za madini.

Kama ambavyo Sheria ya Madini ya mwaka 1998 nayo imekuwa ikipigiwa kelele kwamba inampa uwezo mkubwa mmiliki rasilimali hiyo adhimu.

Na juzi kamati ya Rais chini ya Profesa Nehemiah Osoro ilibaini kasoro hiyo na kupendekeza kwamba Serikali kupitia wataalamu wabobezi katika majadiliano ya mikataba  wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini na kufanya majadiliano na kampuni za madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa taifa.

Sheria ya Uwekezaji nayo imekuwa ikidaiwa kuwapa uhuru uliopitiliza wawekezaji kama ambavyo Kamati ya Profesa Osoro imebaini na kupendekeza  kwamba sheria iweke kiwango maalumu cha asilimia ya hisa ambazo zitamilikiwa na Serikali katika kampuni zote za madini nchini.

Itakumbukwa pia kwamba mwaka 2007 aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe alihukumiwa kutohudhuria vikao vya Bunge kwa muda wa miezi mitatu kuanzia Agosti 2007 baada ya kudaiwa  alikidanganya chombo  hicho cha kutunga sheria kwa kumtuhumu aliyekuwa Waziri ya Nishati na Madini Nizar Karamagi kuhusu mkataba wa madini aliotia saini akiwa hotelini huko London, Uingereza.

Hata hivyo, leo hii Kamati ya Profesa Osoro imependekeza kuwa Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa  mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini na watumishi wengine wa Serikali na watu wote  waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji  madini, utoaji  wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.

Tunadhani kwa mapendekezo haya  na hayo ambayo yamekuwa yakijitokeza katika Bunge ni darasa tosha kwa Mhimili huo kujitathmini katika jukumu lake la utungaji wa sheria na kuisimamia Serikali.

Wabunge na  viongozi wa taasisi muhimu kwa Taifa hawana budi  wanapojadili masuala mbalimbali ya nchi kuondoa hisia za kisiasa  katika kupitisha au kuamua mambo, bali waongozwe na hoja wakiweka mbele maslahi ya taifa.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

Tanzania.