Hili la visimbuzi Serikali iliangalie upya

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Tuesday, December 5  2017 at  10:01

Kwa Muhtasari

Serikali imefanya mambo kadhaa katika sekta ya habari, ikiwamo kuanzisha sheria ya habari ya mwaka 2016.

 

SERIKALI imefanya mambo kadhaa katika sekta ya habari, ikiwamo kuanzisha sheria ya habari ya mwaka 2016.

Uanzishwaji wa sheria hiyo umeweka wigo mpana wa upatikanaji wa habari ukizingata matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki ya uhuru wa waandishi wa mawazo kwa Watanzania.

Ni ndani ya Katiba hiyo ibara ya 18(2) inaeleza kuwa “Kila raia ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala mbalimbali ya jamii.”

Serikali mara zote inasimamia msingi huu wa Katiba na ndiyo maana ikatoa fursa ya kuwapo kwa vyombo vingi vya habari na pia uhuru mkubwa kwa wananchi wake kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, uwepo wa taarifa kwamba takriban theluth moja ya watumiaji wa visimbuzi hawatumii tena vifaa hivyo kutazama runinga kikiwa ni kiwango kikubwa kuwahi kurekodiwa ndani ya miaka mitano iliyopita inatatiza upatikanaji wa habari.

Mwenendo huo unatajwa kupaa kwa kasi ndani ya miaka mitatu iliyopita inahatarisha upatikanaji wa habari kwa wananchi kupitia runinga na hivyo kuwaweka katika mazingira magumu ya kujua nini kinachoendelea sanjari na kutopata habari zinazoweza kuathiri au kuwa na msaada katika maisha yao.

Uchambuzi wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2017 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) umebaini kuwa idadi ya visimbuzi vinavyonunuliwa inaongezeka kila mwaka lakini ukuaji huo unaathiriwa na kazi ya kupaa kwa visimbuzi visivyotumika kwa muda mrefu.

Takwimu hizo zinabainisha kuwa hadi kufikia Desemba 2016 Tanzania ilikuwa na visimbuzi 1.7 milioni.

Hata hivyo watumiaji 500,000 hawavitumii kwa wakati huo sawa na asilimia 29.4 ya visimbuzi vyote vilivyokuwa vimenunuliwa. Idadi ya watu wenye visimbuzi lakini hawavitumii ilianza kupanda miaka miwili iliyopia kutoka asilimia sifuri mwaka 2014 hadi asilimia 29.4 mwaka 2016 huku baadhi ya wananchi walieleza kuwa ukata umesababisha kutotumia vifaa hivyo vya dijitali.

Mwaka 2014 visimbuzi vyote vilivyokuwapo nchini vilikuwa vinafanya kazi.

Ikiwa sababu kubwa ya mwananchi kuweza kumudu gharama za visimbuzi  ni ukata hata vile ambavyo ‘bando’ lake la chini linapatikana kwa bei ndogo, basi Serikali inapaswa kuliangalia kwa jicho la tatu suala hili ambalo ni la kitatiba.

Ni wazi kwamba watoa huduma ya habari kwa kutumia visimbuzi wanawajibika kujiendesha kibiashara lakini pia kwa kuwa na haki ya wananchi kupata habari, chombo pekee kinachoweza kuwawezesha kupata haki hiyo ni Serikali.

Ni vyema Serikali ikaangalia namna inavyoweza kulishughulikia suala hili ama kwa kuwapunguzia kodi watoa huduma ili baadhi ya ‘chaneli’ za runinga ziendelee kupatikana bila malipo au itoe ruzuku kwa watoa huduma hao mahsusi kwa ajili ya ‘chaneli’ hizo.

Wakati moja, kati ya mambo hayo mawili likifanyiwa kazi wananchi waachiwe haki yao ya kikatiba ya kupata habari bure kupitia ‘chaneli’ hizo hususan zile za Kitanzania.

Tahariri ya Mwananchi,

Mwananchi Communications Limited (MCL)

S.L.P. 19754 Dar es Salaam-Tanzania

SIMU +255222450875 au +255754780647