http://www.swahilihub.com/image/view/-/3887460/medRes/2050277/-/2m6w0d/-/kesa.jpg

 

Hongera HESLB kwa kukubali rufaa

Kalamu

Baadhi ya wahitimu wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari Jangwani 

Na TAHARIRI YA MWANANCHI

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  09:03

Kwa Muhtasari

Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya wanafunzi 2,679 waliopata mikopo ya jumla ya TSh9.6 bilioni baada ya kukamilisha uchambuzi rufaa walizokata kupinga kunyimwa mikopo.

 

BODI ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya wanafunzi 2,679 waliopata mikopo ya jumla ya TSh9.6 bilioni baada ya kukamilisha uchambuzi rufaa walizokata kupinga kunyimwa mikopo.

Kwa mujibu wa HESLB, wanafunzi 1,847 kati ya hao walioshinda rufaa ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya Sh6.84 bilioni.

HESLB imesema wanafunzi 832 ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita.

Bodi hiyo imesema kuwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya Sh2.76 bilioni na kwamba fedha zimeshapelekwa vyuoni. Kukamilika kwa rufaa zao kunafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa jumla ya Sh108 bilioni kwa mwaka 2017/18 hadi sasa na bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/18 ni  Sh427.54 bilioni.

Tunapenda kuipongeza bodi ya mikopo kwanza kwa kuweka mfumo huo wa kupata maoni ya wanafunzi ambao hawakuridhika na wachambuzi walivyofikia uamuzi wa kuwapa mikopo.

Tunaamini kuwa mfumo huo ni wa wazi na unafuata haki, hivyo wale ambao hawakushinda rufaa zao walistahili kupata mikopo na wale ambao hawakushinda hawakustahili.

Kitendo cha kuruhusu rufaa ni kizuri kwa kuwa kinaipa  bodi nafasi nzuri ya kupitia upya uchambuzi wake wa  wake wa wanafunzi wanaostahili kupata na wasiostahili, kuangalia dhaifu ulipotokea na kutathmini kama umekuwa wa mara kwa mara ili kuchukua hatua za kurekebisha na pia inajemga Imani kwa wanafunzi kuwa wakati mwingine hunyimwa mikopo kimakosa na hivyo wanaweza kukata rufaa.

Pia, uamuzi wa kuweka hatua ya kukata rufaa inamaanisha kuwa wanafunzi wnapata uzofu wa jinsi ya kuingiza taarifa zao wakati  wakiomba mikopo kwa kuwa pengine wengine hunyimwa kutokana na kutoweka vizuri taarifa zao pamoja na vielelezo, hivyo wanapokata rufaa hupata fursa zaidi ya kurekebisha maombi yao.

Kukubali rufaa zaidi ya 2,600 kunamaanisha kuwa wakati bodi inapotangaza orodha ya kwanza ambayo hulalamikiwa kwa kuwa na idadi ndogo, hakumaanishi kuwa ni mwisho au ina upungufu wa fedha bali baadhi hukosa kutokana na kasoro au udhaifu wa kupitia vizuri maombi.

Wanafunzi hawana budi kuwa makini katika ujazaji wa taarifa zao wakati wanapoomba mikopo ili kupunguza rufaa ambazo pia hutumia rasilimali nyingi za Serikali wakati wa kuzipitia.

Pia tunaishauri bodi iendelee kuweka mifumo mizuri ya ushirikishwaji wa wanafunzi katika kuhakiki taarifa zao ili kujenga imani zaidi kwa wananchi kwamba hata kidogo kinachopatikana kinatolewa kwa nia ambazo ni za haki na uwazi.

Bodi haina budi pia kutafuta vyanzo zaidi vya fedha kwa ajili ya kuongeza kiwango cha kukopesha wanafunzi kinachotolewa  kwa mwaka kwa kuwa mahitaji ni mengi lakini wanufaika ni wachache.

Kutegemea ruzuku pekee ya Serikali kutaifanya bodi kuwasaidia wanafunzi wachache  na kusababisha wengi  ambao hawana uwezo kushindwa kuendelea na massomo na hivyo kushndwa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa kwa kutumia ujuzi wao ambao wangeupata vyuoni.

Kama tulivyoishauri bodi, Serikali haina budi pia kuangalia jinsi ya kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Ruzuku pekee haiwezi kutosheleza mahitaji ya wanafunzi kwa kuwa ni wengi.

Serikali inaweza kujadiliana na taasisi za fedha kuangalia jinsi zinavyoweza kushiriki katika utoaji wa mikopo.